Katika juma lililopita, Polisi wa Tanzania wamewakamata kiholela wanachama na wafuasi 375 wa chama kikuu cha upinzani nchini humo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Miongoni mwao ni aliyekuwa mgombea urais Tundu Lissu, mwenyekiti wa chama Freeman Mbowe, kiongozi wa tawi la vijana John Pambalu, na baadhi ya waandishi wa habari. Ukamataji huo umefanyika kabla ya mipango ya chama ya kuadhimisha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana Agosti 12 jijini Mbeya.
Agosti 11, polisi walitangaza kuzuia tukio hilo kwa sababu lililenga “kuvunja amani”. Walinukuu kauli ya hivi karibuni kutoka kwa mratibu wa uhamasishaji wa tawi la vijana la Chadema ambayo ilirejea maandamano ya hivi karibuni yaliyoongozwa na vijana katika nchi jirani ya Kenya. Hata hivyo mamlaka ziliruhusu kufanyika kwa maadhimisho mengine ya Siku ya Kimataifa ya Vijana yaliyoratibiwa na chama tawala siku mbili zilizopita huko Zanzibar.
Polisi walisema kuwa Agosti 13 walimwachia Lissu, Mbowe na viongozi wengine wa chama bila ya mashtaka ya jinai baada ya kuhojiwa. Lakini hiki kilichofanyika ni ishara mbaya ikiwa Tanzania inajiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Wakati Samia Suluhu Hassan alipochukua ofisi kufuatia kifo cha ya Rais John Magufuli mwezi Machi 2021, alichukua hatua kadhaa kuboresha rekodi ya Tanzania ya haki za binadamu. Mashambulizi ya haki za msingi yalikithiri chini ya Magufuli, ikiwa ni pamoja kuwafanyia vurugu upinzani karibu na uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2020.
Hata hivyo, hakujawa na muendelezo mzuri. Mwezi Julai 2021, polisi walimkamata Mbowe na wanachama wengine 11 wa Chadema kabla ya mkutano wa kujadili maboresho ya katiba ya nchi. Mbowe alishikiliwa kwa mashitaka ya ugaidi na kuwekwa kizuizini kwa miezi saba kabla ya kuachiwa. Mwaka 2023, mamlaka ziliwakamata na kuwatisha wakosoaji wengi wa mkataba wa serikali kuhusu usimamizi wa bandari za nchi. Serikali pia bado haijashtaki mwana usalama hata mmoja kwa mauaji ya angalau watu 14 na majeruhi wengine 55, pamoja na kuwapiga wafuasi wa upinzani, huko Zanzibar wakati wa uchaguzi wa mwaka 2021
Haki ya uhuru wa kushirikiana na wengine na kukusanyika kwa amani zimelindwa na katiba ya Tanzania na mikataba na kikanda na kimataifa ambayo nchi imeiridhia. Mamlaka zinapaswa kuachana na mienendo hii na kuhakikisha wapinzani wa kisiasa na wakosoaji wengine wa serikali wanafurahia haki hizi za msingi.