(Nairobi) – Yamkini watu sita wameuawa kwenye oparesheni za polisi zilizojaa ukatili katika siku 10 za mwanzo wa kafyu ya nchini Kenya iliyotangazwa tarehe 27 mwezi Machi mwaka 2020. Kafyu hiyo ilitangazwa ili iwe hatua ya kuzuia kuenea kwa maradhi ya homa ya mapafu almaarufu Korona, shirika la Haki la Human Rights Watch limesema leo.
Maafisa wa polisi, bila sababu zozote, waliwafyatulia watu risasi, wakawapiga wakiwa sokoni au wakiwa njiani wakirudi nyumbani kutoka kazini hata kabla kuanza rasmi kwa kafyu. Vilevile maafisa wa polisi waliingia kwenye maboma ya watu kwa lazima na kwenye maduka yao. Zipo habari za polisi kuwapora raia pesa zao au hata kuiba chakula katika maeneo mbali mbali ya Kenya. Kufuatia ukosoaji mwingi kutoka kwa makundi mbali mbali ikiwemo shirika la Human Rights Watch, Rais Uhuru Kenyatta aliomba msamaha kufuatia ukatili huu huku akikiri kwamba polisi walitumia nuguvu kupita kiasi, lakini hakutoa maagizo polisi wakomeshe ukatili mwingi na ukiukaji wa haki.
“Inashangaza kwamba raia wamekuwa wakipoteza maisha na njia zao za kujitafutia mapato wakati wa oparesheni za polisi zinazodaiwa kuwa za kuwalinda wasiambukizwe maradhi,” amesema Otsieno Namwaya, mtafiti mkuu, tawi la Afrika, shirika la Human Rights Watch. “Ukatili wa polisi sio tu kwamba u kinyume cha sheria; vilevile unavuruga na kuharibu kampeni ya kukabili ueneaji wa virusi vya Korona.”
Kati ya tarehe 29 mwezi Machi na tarehe 14 mwezi Aprili, shirika la Human Rights Watch limeendesha utafiti wake ambapo liliwahoji watu 26 kwa njia ya simu. Watu hao 26 walijumuisha mashahidi, jamaa za waathiriwa na vilevile waathiriwa wenyewe wa dhuluma za polisi wakati wa kafyu katika kaunti za Nairobi, Mombasa, Kwale, Busia, Kakamega, Mandera na Homa Bay. Mahojiano hayo yanafichua dhuluma za polisi dhidi ya wakazi wa kaunti hizo.
Tarehe 25 mwezi Machi, Rais Kenyatta alitangaza kafyu ya kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri akisema ingeanza tarehe 27 mwezi Machi. Tangu mwanzo ilionekana wazi kwamba polisi walitekeleza agizo la kafyu kwa njia mbaya tena yenye vurugu na dhuluma. Katika eneo la kati la Nairobi, maafisa wa polisi waliwakamata watu kwenye barabara za jiji, waliwachapa, wakawapiga mateke, na kuwakusanya watu pamoja, na hivyo kuchangia katika kueneza virusi vya Korona. Katika mtaa wa Embakasi mashariki ya Nairobi, polisi walililazimisha kundi la watu waliokuwa wametoka kazini wakielekea nyumbani kupiga magoti barabarani. Polisi waliwachapa na kuwapiga mateke, watu walioshuhudia waliliarifu shirika la Human Rights Watch.
Jijini Mombasa, tarehe 27 mwezi Machi, zikiwa zimesalia saa mbili kabla kuanza kwa kafyu , maafisa wa polisi waliwarushia vitoza machozi watu wakiwa kwenye kundi wakiwa wanajiandaa kupanda feri waelekee nyumbani kutoka kazini. Waliwavamia na kuanza kuwachapa kwa fimbo zao huku wakiwagonga kwa bunduki. Waliwapiga mateke, makofi na kuwalazimisha waketi wakifinyana pamoja huku wengine wakilala juu ya wenzao. Picha za Video za televisheni za Kenya na hata zile ziliwekwa kwenye mitandao ya jamii, zilionyesha kwamba polisi hawakuwa wakivaa barakoa na vifaa vingine ambavyo wizara ya afya imesema viwe vinavaliwa na wakenya wakiwa nje kwenye shughuli zao.
Shirika la Human Rights Watch limepata maelezo yanayosimulia visa kama hivyo kutoka pande mbali mbali za nchi. Polisi walitekeleza agizo la kafyu kwa njia zenye dhuluma na ukatili mwingi huku wakiwapiga watu risasi, wakiwachapa na kuwapora watu pesa. Ukatili huo ulisababisha vifo vya yamkini watu sita.
Tarehe 31 mwezi Machi, ukiwa usiku wa manane katika mtaa wa Kiamaiko eneo la Eastlands, maafisa wa polisi walimpiga risasi Yassin Hussein Moyo, wa umri wa miaka 13. Walioshuhudia walisema risasi ilimpiga tumboni na akafa papo hapo. Babaye kijana huyo, Hussein Moyo, aliviambia vyombo vya habari vya Kenya kwamba wakati risasi ilimpiga mwanawe alikuwa kwenye sebule ya nyumba yao katika orofa ya tatu usiku wa manane akiwa na nduguze.
Mamlaka ya kutathmini utendakazi wa polisi nchini Kenya- IPOA, tarehe 2 mwezi Aprili ilisema imeanzisha uchunguzi kwenye mauaji ya Moyo. Hata hivyo, ahadi kama hizo zimekuwapo wala hazijawahi kufuatiwa na vitendo ili polisi waliohusika dhuluma wachukuliwe hatua za kisheria. Mwaka 2017, mamlaka ya IPOA iliahidi kuanzisha uchunguzi wa mauaji ya mtoto mdogo kwa jina Samantha Pendo aliyeuawa mjini Kisumu,- Alikuwa wa umri wa miezi 6. Jijini Nairobi wakati huo kulikuwa na mauaji mengine ya msichana wa umri wa miaka 9 kwa jina Stephanie Moraa. Aliuawa wakati wa vurugu za uchaguzi mkuu wa mwaka huo- 2017. Kufikia sasa hakuna polisi amefikishwa kortini na kushtakiwa kwa mauaji hayo au mauaji mengine ya zaidi ya watu 100 ambayo shirika la Human Rights Watch limeyafanyia utafiti na kunakili kwamba yalifanyika wakati huo.
Katika kaunti za Busia na Kakamega, magharibi ya Kenya, maafisa wa polisi waliwapiga watu na kuwafyatulia risasi. Wakazi waliliambia shirika la Human Rights Watch kwamba katika visa vingi ukatili huo, uliosababisha vifo na majeraha mabaya, ulifanywa kabla ya saa za kafyu.
Tarehe 1 mwezi Aprili, saa sita adhuhuri katika kaunti ya Kakamega, polisi wakitekeleza agizo la kupiga marufuku masoko ya reja reja walifika wakiwa kwenye malori yao katika markiti ya Mumias na kuanza kuwapiga watu, wakawapiga mateke huku wakiwafyatulia risasi wauzaji bidhaa. Wauzaji watatu kwenye soko hilo waliliambia shirika la Human Rights Watch kwamba Idris Mukolwe, wa umri wa miaka 45 muuzaji wa nyanya, alifariki baada ya kugongwa na kichupa cha gesi ya kutoza machozi ambacho polisi walimrushia. Muuzaji mmoja alisema:
“Tulikimbia baada ya polisi kufika, lakini waliturushia vitoza machozi. Kichupa kimoja cha gesi hiyo kikamgonga Mukolwe na kulipukia usoni mwake. Alianza kushindwa kupumua huku polisi wakimcheka, halafu tulipoenda kumsaidia, polisi hao wakaturushia vitoza machozi ikabidi tutoroke.”
Tarehe 30 mwezi Machi, kwenye soko hilo hilo polisi walimpiga risasi muuzaji mwengine wa bidhaa wa umri wa miaka 24 kwa jina Grace Muhati. Walimfyatulia risasi wakimlenga haswa . Wauzaji wenzake kwenye soko hilo walimkimbiza katika hospitali kuu ya kaunti ya Kakamega, alitibiwa na kufikia sasa anaendelea kupata nafuu. Jamaa wa familia yake alisema Madaktari walitoa risasi mbili mwilini mwake.
Shirika la Human Rights Watch limethibitisha kwamba polisi walimuua mtu mwengine Kakamega na kuongeza idadi ya waliouawa kuwa watu wawili. Jamaa huyo alipigwa hadi kufa. Aidha mtu wa tatu aliuawa katika kaunti ya Homa Bay, magharibi ya Kenya, huku watu wengine wawili wakiuawa katika kaunti ya Kwale, eneo la pwani.
Serikali ya Kenya yafaa kuanzisha uchunguzi wa haraka kwenye visa vya polisi kuwapiga watu risasi, kuwapiga kwa rungu zao na kuwadhulumu kwa njia nyengine na kuwajeruhi vibaya. Serikali ya Kenya yafaa kuwachukulia hatua za kisheria polisi watakaopatikana kuhusika, limesema shirika la Human Rights Watch. Kulingana na sheria za Kenya na vilevie sheria za kimataifa, polisi wanaruhusiwa kutumia nguvu iwapo hawana njia nyengine lakini iwe katika kuokoa maisha.
Kenya ina historia ndefu ya maafisa wake wa polisi kutumia nguvu za kupita kiasi wakati wa oparesheni za kukabili makosa, iwe katika mitaa ya watu wa mapato ya chini au kila wanapohitajika kukomesha maandamano, mara nyingi husababisha vifo vya kiholela ambavyo vingezuiwa. Mwezi Februari, shirika la Human Rights Watch lilirekodi visa vinane vya mauaji yanayofanywa na polisi. Visa sita vilifanyika wakati wa maandamano ya amani. Kisa kimoja kilikuwa katika mtaa wa Majengo ambapo raia waliandamana kukosoa mauaji ya mwanamume wa umri wa miaka 24. Kisa kingine kilikuwa katika mtaa wa Kasarani ambapo raia waliandamana kulalamikia hali mbaya ya barabara katika maeneo ya Majengo, Kasarani na Mathare. Hapakuwa na sababu ya kutosha ya mauaji hayo.
Mwezi Februari mwaka 2018, mashirika ya kutetea haki za binadamu ya nchini Kenya na ya kimataifa, likiwemo shirika la Human Rights Watch, yalirekodi zaidi ya visa 100 vya polisi kuwaua waandamanaji wa vyama vya upinzani wakati wa uchaguzi wa urais wa mwaka 2017. Mwezi Juni mwaka 2016, shirika la Human Rights Watch lilipata kwamba yamkini watu watano walifariki huku 60 wakijeruhiwa kwa risasi katika eneo la Nyanza wakati polisi walikuwa wakiwazuia waandamanani waliokuwa wakishinikiza kuteuliwa makamishna wapya wa tume ya uchaguzi nchini Kenya.
Licha ya kuwa visa vingi vya mauaji yanayofanywa na polisi vimerekodiwa vyema na taasisi za serikali na vilevile mashirika ya haki za binadamu, maafisa wa polisi na idara nyengine za usalama nchini Kenya hawajawahi kuchukuliwa hatua za kisheria za kufaa. Hata taasisi yenye jukumu la kuchunguza utendakazi wa polisi, Mamlaka ya IPOA haijafanikiwa kuwashtaki polisi. Wachunguzi wa makosa ya polisi wanaonekana kulenga zaidi kesi moja ama mbili zilizoibua hisia kali kote nchini huku wakipuuza kesi nyengine. Wakuu wa polisi na Mamlaka ya kuchunguza utendakazi wa polisi kwa pamoja wana jukumu la kuhakikisha kwamba mauaji ya sasa na ya awali yamechunguzwa kwa kina na wale wote waliohusika mauaji hayo wameshtakiwa kwa mujibu wa sheria za Kenya, shirika la Human Rights limesema.
“Serikali ya Kenya yafaa ihakikishe kwamba maafisa wa polisi hawatumii nguvu ya kupita kiasi na kwamba kafyu iliyotolewa kukabili ueneaji wa maradhi ya Korona inakuwa na umuhimu kwa wananchi wa Kenya,” Amesema Namwaya. “Serikali ya Kenya yafaa ifwatilie kwa karibu ahadi zote ambazo hutolewa na hivyo kuchunguza mauaji na dhuluma nyengine ili kuwachukulia hatua za kisheria polisi waliohusika.”
Ili kupata mengi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu ambao shirika la Human Rights Watch limetafiti na kurekodi, tafadhali angalia hapo chini.
Mauaji wakati wa kafyu/vifo
Tangazo la kuanza kafyu nchini Kenya likiwa na lengo la kukabili ueneaji wa maradhi ya Korona lililianza kutekelewa tarehe 27 mwezi Machi. Katika siku za kwanza 10, polisi walitumia nguvu za kupita kiasi kote nchini, wakasababisha vifo vya watu yamkini sita huku wakiwajeruhi wengine wengi, shirika la Human Rights Watch limepata hayo. Jumla ya watu 26 ambao shirika la Human Rights Watch liliwahoji walikuwamo waathiriwa wa ukatili wa polisi, wale walioshuhudia maovu hayo wenyewe, jamaa za waathiriwa wakiwemo wale waliouawa, wanaharakati waliokuwa wakiwatafutia waathiriwa na familia zao haki.
Calvin Omondi wa miaka 23, Tarehe 27 Machi, kaunti ya Homa Bay, Magharibi ya Kenya
Mtu mmoja wa Rachuonyo kaunti ya Homabay magharibi ya Kenya aliyeshuhudia,alisema Omondi, ambaye alikuwa mwendeshaji bodaboda, alifariki tarehe 29 mwezi Machi katika hospitali ya Level four ya Rachuonyo mjini Oyugis kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya polisi kumpiga vibaya tarehe 27 mwezi Machi wakati wa mwanzo wa kafyu. Jamaa wa Omondi walisema alikuwa akirudi nyumbani kwake karibu saa moja hivi usiku zikiwa saa ambazo kafyu ilikuwa inaanza. Walisema kundi la maafisa wa polisi lilimshambulia katika markiti moja Homabay na kumfanya apoteze mwelekeo akiwa juu ya pikipiki yake. Hata hivyo kamanda wa polisi wa eneo hilo, Esau Ochorokodi, aliviambia vyombo vya habari kwamba polisi hawakuhusika katika kifo chake na kwamba Omondi akiendesha pikipiki alipoteza mwelekeo akaanguka huku akigonga kichwa chake kwenye miamba ya daraja.
Hamisi Juma Mbega wa- miaka 49, Tarehe 28 mwezi Machi, kaunti ya Kwale, eneo la Pwani
Jamaa yake na wanaharakati wawili wa kupigania haki za binadamu walisema dakika chache kabla saa moja usiku, Juma, wa umri wa miaka 49 aliyekuwa afisa wa polisi awali ambaye sasa alikuwa akifanya biashara ya bodaboda alijitolea kumsafirisha mwanamke mjamziito akiwa ameanza kupata machungu ya uzazi kumpeleka katika hospitali ya Mwahima kaunti ya Kwale eneo la pwani. Jamaa yake walisema alikuwa njiani akirudi nyumbani kwake katika kijiji cha Zibani eneo bunge la Matuga, kundi la maafisa wa polisi, lilimsimamisha likaanza kumpiga na kumgonga kwa bunduki. Jamaa yake mmoja, kwa jina Omar Abdallah Raisi, alisema polisi walianza kwa kumrushia Juma, baba ya watoto wanne, kitoza machozi, akiwa katikati ya barabara katika eneo la Mkunamnazi, Likoni: “Akiwa kwenye pikipiki yake alipoteza mwelekeo na kuanguka. Polisi hao sasa walianza kumpiga, wakamjeruhi vibaya na kumwacha hapo akiwa hali mahtuti.”
Moyo wa miaka 13, tarehe 31 Machi, kaunti ya Nairobi
Polisi walimpiga risasi tumboni Yassin, akiwa amesimama kwenye sebule ya nyumba yao katika orofa ya tatu usiku na akafa papo hapo.
Eric Ng’ethe Waithugi, wa miaka 23, Tarehe 1 mwezi Aprili, kaunti ya Kwale, eneo la Pwani
Watu wawili walioshuhudia na mwanaharakati mmoja wa haki za bianadamu, walisema zaidi ya maafisa 20 wa polisi walimpiga hadi kufa Eric Ng’ethe, wa umri wa miaka 23, aliyekuwa akifanya kazi ya uhasibu katika kilabu moja mjini Ukunda, kaunti ya Kwale. Kisa kilifanyika karibu saa moja hivi usiku wa tarehe 1 mwezi Aprili. Mtu mmoja aliyeshuhudia kisa hicho alisema Ng’ethe alikuwa kazini, lakini akiwa na vijana wengine wakaamua kujifungia kwenye kilabu saa za kafyu zilipokuwa zinakaribia. Polisi hao walirusha kitoza machozi ndani ya kilabu wakavunja mlango, na kuanza kumpiga Ng’ethe na watu wengine 11 waliokuwa ndani ya kilabu hiyo. Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Msambweni, Nehemiah Bitok, aliviambia vyombo vya habari vya Kenya kwamba Ng’ethe alifariki wakati wa kundi la watu lililokuwa ndani ya kilabu lilikuwa likiwatoroka polisi baada ya kukataa kutii amri ya kufungua mlango wa kilabu hiyo.
Yusuf Ramadhan Juma, wa miaka 35, Tarehe 1 mwezi April, kaunti ya Kakamega, eneo la Magharibi
Familia ya Ramadhan Juma, aliyekuwa na matatizo ya akili, ilisema aliondoka nyumbani jioni ya tarehe 1 mwezi Aprili na hakurudi. Jamaa yake mmoja wa familia hiyo alisema keshoye asubuhi walimtafuta na kumpata katika hospitali kuu ya kaunti ya Kakamega akiwa na majeraha. Walikisia kwamba majeraha hayo yalitokana na kichapo cha polisi wakati wa kafyu usiku ule. Juma alifariki muda mfupi baada ya familia yake kumpata. Kamanda wa polisi katika eneo la kati la Kakamega, David Kabena, aliviambia vyombo vya habari kwamba polisi hawakuhusika katika kifo cha Juma: “Tumesikia kwamba mwathiriwa alikuwa na matatizo ya akili,” alisema Kabena. “Labda alitembea kule nje akigusa mali ya wenyewe ndipo akapigwa na watu ambao hawakujua kwamba alikuwa mgonjwa wa akili.”
Idris Mukolwe, wa miaka 45, Tarehe 1 mwezi April, kaunti ya Kakamega, Magharibi ya Kenya
Jamaa zake na wauzaji wenzake wa bidhaa katika soko la Mumias waliliambia sharika la Human Rights Watch kwa njia ya simu kwamba Mukolwe, aliyekuwa muuzaji wa nyanya, alirushiwa kitoza machozi na maafisa wa polisi waliokuwa wakiwafukuza wauzaji kutekeleza marufuku dhidi ya masoko ya reja reja iliyokuwa imetolewa na serikali ya kaunti ya Kakamega. Muuzaji mmoja kwenye soko hilo alielezea jinsi Idris alishindwa kuamuka baada ya kugongwa na kichupa cha kitoza machozi, akajikokota hadi akasimama, huku maafisa wa polisi wakimkejeli na kumcheka. Alipoteza fahamu muda mfupi baadaye na kufariki, walisema wauzaji kwenye soko hilo.
Kuwachapa watu na kuwapora
Shirika la Human Rights Watch pia lilirekodi visa vya watu kupigwa vibaya huku wengine wakiporwa. Waathiriwa wawili wa kichapo cha polisi walisema, Tarehe 28 mwezi Machi, maafisa saba wa polisi waliingia kwenye ploti ya milango saba hivi kwa kulazimisha katika mtaa wa Kayole iliyokuwa na duka na kilabu katika eneo la Matopeni. Walimtoa nje mwenye ploti jamaa mlemavuwa umri wa makamo kwa kumburura kutoka kwenye ploti hiyo na kuanza kumchapa yeye na mkewe. Waathiriwa wa kichapo hicho walisema baadhi ya polisi walivunja milango ya nyumba kwenye ploti hiyo na kuanza kuwachapa wakazi wengine. Mwathiriwa mmoja alisema: “Walitupiga kuanzia saa mbili usiku hadi saa nne halafu wakaanza kuchukua vifaa vya thamani, hasa vya elektoroniki kutoka kwenye nyumba, kwenye kilabu na madukani.”
Katika kisa kingine, mtu wa umri wa makamo katika mtaa wa Kipevu, kaunti ya Mombasa, alisema kwamba tarehe 1 mwezi Aprili alikutana na kundi la maafisa wa polisi ikiwa karibu saa moja usiku kwenye duka moja la kuuza bidhaa za chakula si mbali sana na kwake nyumbani. Alisema polisi wawili walimkabili na kuanza kumpiga kwa mijeledi mieusi. “Wote walianza kunicharaza mijeledi” akasema
“Baadhi yao walinigonga kwa rungu zao huku wengine wakinipiga mateke na ngumi. Singejua walikuwa wangapi. Wengine walikuwa wakiwapiga watu wengine waliokuwa karibu nami. Ilikuwa karibu saa moja na dakika ishirini hivi usiku.”
Mwanamume mwengine wa umri wa miaka 26, wa eneo la Mwangulu mtaa wa Lungalunga mjini Mombasa, alisema kwamba tarehe 2 mwezi Aprili polisi waliingia kwenye ua wa boma lake ikiwa karibu saa moja na dakika 20 hivi usiku na kuanza kumcharaza mijeledi. Alikuwa ametoka nje ya nyumba yake kwenda msalani katika ua wa boma lake alipovamiwa na kuanza kupigwa. Polisi hao wakimpiga walikuwa wakisema amekiuka agizo la kafyu wala hakufaa kuwa nje ya nyumba yake wakati kama huo. Kichapo hicho kilimpa majeraha kwenye mgongo, mikononi na kwenye shingo.
Katika mtaa wa Easteigh jinni Nairobi, mfanyabishara wa umri wa makamo alisema kwamba polisi walimpiga na kumweka kwenye buti ya gari lake na kuliendesha gari hilo mtaani kwa muda wa saa tatu na kumwachilia tu alipowapa hongo ya shilingi 2000 (karibu dola 20 hivi za Amerika).
Katika kaunti ya Mandera eneo la kaskazini la Kenya, mtu mmoja wa umri wa miaka 35 alisema polisi wa akiba, kitengo cha polisi wanaoajiriwa kutoka miongoni mwa raia ambao hupewa mafunzo na maafisa haswa wa polisi ili wasaidie kulinda sheria vijijini kote nchini, waliingia kwenye gari lake kwa lazima na kuanza kuliendesha wakampeleka hadi katika kituo cha polisi, wakati huo muda wa kafyu ukiwa bado kufika- ilikuwa imesalia saa moja kabla kuanza kafyu. Polisi hao walianza kumpiga alipowauliza kwanini walikuwa wamemkamata kabla saa za kafyu. Jamaa huyo alitutumia picha zake zikionyesha majeraha kwenye miguu mikono na mgongoni.
Katika kaunti ya Busia, wakazi walisema maafisa wa polisi wamekuwa wakitekeleza maagizo ya kafyu ikiwa mchana tu. Wamesema polisi hao huvamia maboma ya watu wanaoandaa pombe na kuanza kuwatia watu nguvuni halafu baadaye wanawaachilia baada ya kupewa hongo ya kati ya shilingi 2,000 na 5,000 (dola 20 na 50 za Amerika) kulingana na maelewano. Katika kijini kimoja si mbali na na mji wa Busia, mtu mmoja wa huduma za bodaboda wa umri wa miaka 27 alisema alasiri ya tarehe 29 mwezi Machi, maafisa wa polisi walimsimamisha na kuanza kumpiga bila sababu yoyote. Alisema alipata majeraha mabaya kwenye mwili mzima.