Skip to main content

Kenya: Dhuluma kwenye oparesheni ya kuwafurusha watu katika msitu wa Mau

Koma kutumia nguvu za kupita kiasi; zingatia kanuni zilizowekwa

Hii ni picha ya mwezi Juni 2019. Inaonyesha kijiji cha Gorofa eneo la Nkoben, mojawapo ya makao ya sasa ya wale waliofurushwa kutoka msitu wa Mau Julai 2018. HRW/Namwaya

(Nairobi) — Serikali ya Kenya bado kuanzisha uchunguzi kuhusu dhuluma zinazofanywa na maafisa wa usalama wanaoendesha oparesheni ya kuwaondoa maelfu ya watu katika msitu wa Mau - Oparesheni iliyoanza Julai mwaka 2018. Shirika la Human Rights Watch limesema leo. Mwezi Agosti 2019, serikali ilitangaza mpango wa kuwaondoa watu 60,000 katika msitu huo. Serikali yafaa kuhakikisha maafisa wa polisi hawatumii nguvu zinazokiuka sheria na vilevile iwape watu wanaofurushwa kipindi cha kuondoka katika ardhi za msitu huku ikifidia hasara wanayopata jinsi sheria za Kenya na za kimataifa zinavyoagiza.

Mpango wa kuwaondoa watu katika ardhi zinazotambuliwa na serikali kuwa msitu ni sehemu ya juhudi za serikali za kuokoa msitu wa Mau ili usiharibiwe kabisa. Serikali ya Kenya imesema msitu huo unakabili tishio la kuangamizwa kutokana na watu kuhamia mwituni, kukata miti na kufanya shughuli pale kinyume cha sheria. Mpango wa sasa wa kuwaondoa watu mwituni unawalenga watu wanaoshi katika eneo la Maasai Mau, sehemu moja ya msitu wa Mau inayosimamiwa na serikali ya kaunti ya Narok chini ya kanuni ya udhamini wa ardhi ya Mau. Shirika la ulinzi wa Misitu la Kenya linasimamia sehemu nyengine 21 za msitu huo.

“Katika juhudi za kuokoa msitu wa Mau, serikali imewafukuza watu kwa njia za dhuluma, bila kuzingatia sheria huku ikishindwa kuzingatia masharti iliyoweka yenyewe,” amesema Otsieno Namwaya, mtafiti mkuu, ukanda wa Afrika, shirika la Human Rights Watch. “Licha ya kuwa juhudi za kusitawisha misitu ni mpango mwema, njia ambayo serikali inaitumia kuwaondoa wakazi kwenye msitu inaibua shaka nyingi kuhusu iwapo serikali inatii haki za watu hao.”

Mwezi Juni, Shirika la Human Rights Watch liliwahoji watu 67 katika maeneo ya Maasai Mau na Narok, wakiwemo wale waliokuwa wamefukuzwa msituni, makundi ya wanaharakati wa usitawishaji mazingira, polisi, na maafisa wa serikali. Watafiti walipata kwamba mapema mwezi Julai 2018, maafisa waliojumuisha walinzi wa misitu, wale wa huduma kwa wanyamapori, polisi wa utawala walipelekwa katika msitu wa Maasai Mau kule upande wa Narok ambapo katika oparesheni walitumia nguvu za kupita kiasi kuziondoa jamii zinazoishi katika ardhi zinazotambuliwa kuwa za msitu.

Juni 2019; Mabaki ya makao yaliyoteketezwa ya mmoja wa wale waliofurushwa kutoka msitu wa Mau Julai 2018. © HRW/Namwaya

Karibu watu tisa, wakiwemo watoto wawili, walifariki wakati wa oparesheni hiyo. Maafisa hao wa usalama waliwapiga watu, wateketeza nyumba, wakaharibu mimea, na kuwaacha maelfu bila makao wakilala nje kwenye kibaridi kikali. Karibu watu wanne hawajulikani walipo, nazo familia zinasema hazijapokea usaidizi wowote kutoka kwa polisi hasa kuhusu kuwatafuta jamaa zao ambao hawajulikani walipo.

Katika karibu sehemu tatu hivi, watu hao waliofukuzwa msituni walisonga na kusalia kando kando ya msitu, huku wakijenga makao ya muda tu, wengi wakijenga katika maeneo ya Masaita, Gorofa na katika vijiji vya Chepalungu pale Nkoben, kaunti ya Narok. Viongozi wa jamii walisema maafisa wa serikali waliwafukuza tena mwezi Desemba, katika oparesheni iliyodaiwa kuwa ya kukomesha jaribio lao la kurejea msituni. Walinda usalama waliharibu makao yao ya muda pale Gorofa, Masaita na Chepalungu. Hata hivyo baadaye familia hizo ziliweza kujenga upya vibanda vya muda katika maeneo hayo tena.

Maafisa wa serikali wameshawaambia kwamba yafaa sasa warejee katika maeneo yao asili waliyotoka. Watu hao walisema walitoka kaunti za Bomet, Kericho na vilevile Narok na kujenga makao katika ardhi za msitu wa Mau. Wapo walionunua ardhi hizo na hata kupata stakabadhi rasmi za umiliki kwa hivyo wamekuwa wakiishi pale kwa zaidi ya miaka 30.

Serikali bado kuchunguza vifo, majeruhi na dhuluma nyengine, licha ya familia karibu 30 kutoa habari kwa vituo vya polisi vya kaunti ya Narok. Karibu maafisa wawili wakuu katika kaunti hiyo wamefichua kwamba taarifa rasmi ya kutoa maelezo kwa serikali ilielezea kuwepo dhuluma, ikiwemo kuharibu makao, mimea ya chakula, na maghala ya chakula, huku wakazi wakitendewa unyama. “Idadi ya nyumba zilizoteketezwa ama idadi ya watu waliojeruhiwa imo kwenye taarifa rasmi ya maelezo ya serikali, lakini hatuwezi kuisambaza kwa yeyote,” Afisa mmoja wa serikali alisema.

Maafisa wa serikali wanasema mipango mipya ya kuwaondoa watu, inawajumuisha wale wenye hati-miliki za ardhi na wale wasiokuwa nazo. Serikali imepata idhini ya Mahakama kutupilia mbali hati-miliki za ardhi, ikidai kwamba licha ya kuwa ni hati halali, zinahusu ardhi iliyotolewa kinyume cha sheria. Aidha inaarifia pia kwamba baadhi ya hati hizo zilitolewa kwa njia ya ufisadi iliyo kinyume cha sheria. Maafisa wapelelezi wa makosa ya uhalifu mjini Narok waliliambia Shirika la Human Rights Watch kwamba walikuwa wakiwachunguza maafisa wa serikali, waliohudumu awali na sasa, na watawashtaki wale wanaopatikana wamehusika katika utoaji ardhi kinyume cha sheria na utoaji wa hati- miliki kwa ardhi kama hizo.

Mapema mwezi Agosti, wizara ya Ardhi ilipiga marufuku hati-miliki 1274 kabla mpango wa kuwafurusha wakazi msituni kuanza. Familia zenye hati-miliki sasa zimewasilisha kesi Mahakamani mjini Nakuru, lakini maafisa wa serikali wanasema yeyote aliyeshusika katika kunyakua ardhi katika msitu wa Mau awe na hati- miliki ama la ataondolewa.

Wale watu wanaoishi katika makao yaliyo kando kando ya msitu walisema saa kumi na mbili asubuhi Julai tarehe 7 mwaka 2018, zaidi ya walinda usalama 100 wenye silaha, wakiwa wa Idara ya walinzi wa Misitu, Huduma ya wanyama pori, Kundi la usalama la kaunti ya Narok na maafisa wa idara ya mambo dharura Rapid Deployment Unit ya polisi wa utawala waliletwa katika eneo la kando kando ya msitu lialokaribiana na vijiji vya Nkoben kama vile Chepalungu, Gorofa na Masaita, upande wa Narok wa msitu wa Maasai Mau. Wakazi walisema polisi walivamia maboma ya watu, wakafyatua risasi angani kuwatisha wakazi, wakawapiga na kuwafukuza wakazi, wakaiba, wakateketeza nyumba, na kumfukuza yeyote aliyefika kujaribu kuokoa mali yake na mimea.

Hapa na pale, walinda usalama walitumia misumeno ya umeme kuangusha nyumba huku wengine wakiziteketeza tu. Waathiriwa walisema walinda usalama waliwapiga watu wakitumia vipande vya miti, au kuwagonga kwa bunduki zao na kuwajeruhi mamia. Wapo waliotiwa nguvuni huku wengine wengi wakizuiliwa muda wote wa oparesheni iliyochukua siku tatu.

 “Niliposikia kwamba kuwafukuza watu kumeanza, niliondoka kanisani na kwenda kuangalia nyumba yangu,” alisema mtu mmoja wa umri wa miaka 41 “Polisi walinizuia njiani, wakaanza kunipiga. Walikuwa wakimpiga yeyote aliyekuwa akijaribu kuifikia nyumba yake.”

Shirika la Human Rights Watch lilithibitisha na kurekodi vifo vya watu tisa. Hata hivyo viongozi katika jamii walikisia kwamba karibu watu 30 walifariki. Katika kijiji cha Kararet, wakati walinda usalama waliwafukuza wakazi wote kutoka mbuga binafsi ya Enakishomi, mwanamke wa umri wa miaka 45- mama ya watoto tisa, ambaye alikuwa akifukuzwa na polisi, aliteleza na kuanguka kwenye mtaro akiwa na mtoto mdogo msichana wa umri wa miaka mitano mgongoni. Msichana huyo mdogo kwa jina Sharon Chepkoech, alifariki wiki nne baadaye kutokana na majeruhi aliyoyapata.

Watu wawili, mmoja akiwa jirani ya mwathiriwa na mwengine jamaa yake, waliiambia Human Rights Watch kwamba watu wawili walijinyonga. Miili yao ilipatikana ikiwa bado kwenye Kamba za kujinyongea. Walijinyonga punde walipofahamu kwamba wamepoteza yote waliyomiliki.

Familia ya mtu mmoja ambaye amekuwa hajulikani alipo tangu oparesheni hiyo ianze ilisema miezi kadhaa baadaye, walipata mabaki ya mwili wa mtu waliyeamini alikuwa ndiye jamaa yao mahala ambapo walikuwa wamefukuzwa. Lakini familia hiyo ilisema upasuaji wa maiti kwa uchunguzi haukuwa umefanywa kuthibitisha iwapo alikuwa ndiye au alikuwa nani haswa. Katika eneo la Reiyo, mbuga iliyokuwa imetokana na ugawaji wa sehemu ya msitu wa Mau katika miaka ya 70, watafiti walipata mabaki ya mwanamke asiyejulikana. Wakazi walisema mwanamke huyo alifariki wakati wa oparesheni. Mabaki ya mwili wake yalikuwa bado pale msituni.

Kenya iliidhinisha kanuni za kuwahamisha watu kutoka maeneo fulani mwaka 2009, miaka mitatu baada ya oparesheni nyengine ya kuwahamisha watu kutoka msitu wa Mau. Oparesheni hiyo ilisimamishwa na agizo la Mahakama. Kwa mujibu wa kanuni hizo wale wanaohamishwa wanafaa kupewa notisi mapema kabisa, miezi mitatu kabla siku ya kuondoka. Yafaa notisi hiyo ichapishwe kwenye gazeti rasmi la serikali na kupewa watu wanaolengwa huku kila mmoja akipewa nakala. Iwapo ni vigumu kuwapa kila mmoja yafaa nakala ya notisi hiyo iwekwe mahala pa umma ambapo kila mtu ataisoma.

Kanuni hizo hutaka serikali kuhakikisha kwamba hakuna mtu ataachwa bila makao. Aidha hutaka kuwepo mashauriano ya kutosha baina ya jamii zilizoathirika na serikali ili kupata njia za kuwasiliana vyema kuhusu mpango mzima wa kuwapa makao na kuwafidia walioathirika.

Maafisa wa serikali walisema walitoa kipindi cha notisi cha kutosha, ikiwemo kufanya mikutano ya umma na jamii zilizolengwa mwezi mmoja kabla kuanza oparesheni. Lakini watu waliohojiwa walisema hawakujua kwamba serikali ilikuwa na mpango wa kuwafurusha Mau.

Juni 2019; Waathiriwa wa mpango wa kuwafurusha watu Mau wakiwa katika kambi ya Masaita. Walifurushwa kutoka msitu wa Mau Julai 2018. © HRW/Namwaya

Kati ya watu tuliowahoji hakuna aliyelipwa fidia ama kupewa makao mapya. Nao maafisa wa serikali katika kaunti ya Narok walisema hakuna mipango iwe ya kuwapa makao mapya ama kulipa fidia. Walisema hata wale walio na hati- miliki za ardhi hawatafidiwa kwa sababu walipewa ardhi ambayo ni sehemu ya msitu ambayo haikufaa kupewa watu itumiwe. Agosti tarehe 18, waziri wa mazingira, Keriako Tobiko aliitaja hatua ya watu kupata ardhi katika msitu wa Mau kuwa kosa la jinai (uhalifu) kwa hivyo wahusika hawafai kulipwa fidia: “Huwezi kuwalipa watu kwa kuhusika kosa la uhalifu. Tuseme wazi kwamba hata serikali inaonyesha huruma. Hali haswa ikizingatiwa serikali ingewafunga jela wahusika.”

Chini ya sheria za kimataifa, kuwafukuza watu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, na nchi zafaa kuchukua hatua zote zifaazo kujiepusha na oparesheni za kuwafukuza watu kutoka eneo fulani. Nchi huwa na wajibu wa kuhakikisha wale wanaofukuzwa kutoka mahala fulani wanalipwa fidia kwa hasara iwe wana hati- miliki za ardhi ama la. Serikali yafaa iheshimu haki za mtu kumiliki mali na haki za familia ama jamii iliyomiliki ardhi. Kunapotokea visa vya watu kufukuzwa, kwa sababu zisizoweza kuepukika mfano kwa sababu za manufaa kwa jamii nzima, serikali yafaa izingatie kanuni za kimataifa zinazoongoza oparesheni kama hizo kama vile kuwajibikia dhuluma zinazotokea na kujiepusha na oparesheni za kibaguzi huku haki za wanyonge zikilindwa.

Serikali ya Kenya yafaa kuhakikisha kwamba dhuluma ambazo zimetokea wakati wa kuwafurusha watu kutoka msitu wa Maasai Mau mwaka 2018 zinachunguzwa na waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria. Yafaa pia kuhakikisha kwamba mipango inayoendelea ya kuwaondoa watu inafanywa kwa njia zinazoheshimu kanuni za kitaifa na za kimataifa.

“Serikali ya Kenya yafaa kuhakikisha kwamba oparesheni ya kuwaondoa watu msituni kufanikisha mpango wa kusitawisha misitu inafanywa kwa njia ya utu na inayofwata sheria ifaavyo,” Alisema Namwaya. “Serikali yafaa ishughulikie ukiukaji wa haki wa awali kabla kuendelea na oparesheni ya kuwaondoa watu msituni Mau, ili oparesheni zote ziwe zinatimiza kanuni za kimataifa na za kitaifa.”

Ili kupata maelezo zaidi kuhusu hali haswa na masimulizi ya waaathiriwa, hebu fwata anwani hizi za mitandao.

Ramani hii inaonyesha msitu wa Mau, Eneo la Nkoben katika upande wa Maasai Mau ulioathirika kwa oparesheni ya kuwaondoa watu ya 2018.

© 2019 John Emerson/Human Rights Watch

Historia ya kuwafukuza watu kutoka msitu wa Mau.

Mwanzo mwanzo kabisa msitu wa Mau ulikuwa na ukubwa wa hekari zaidi ya 400,000. Naibu kamanda wa kaunti ya Narok, anasema, eneo kuu la Mau lenye sehemu 22 zinazosambaa katika kaunti saba za Kenya, ndilo eneo la msitu ambalo ni kubwa sana nchini Kenya. Vile vile Mau ndilo eneo la chemchemi ya maji ambalo ni muhimu sana katika eneo la Rift Valley na Magharibi ya Kenya. Msitu wa Mau ndio chanzo cha maji kwa karibu mito 12 ambayo hunyunyiza maji yake katika maziwa matatu- Victoria- ziwa la pili kuu duniani la maji yasiyo ya chumvi, ziwa Nakuru na ziwa Naivasha. Kufungamana na haja ya kujitolewa kujali mazingira, ili kushiriki katika harakati za kupunguza athari za gezi za sumu angani serikali ya Kenya imekuwa ikiwafukuza watu kutoka msitu wa Mau tangu mwaka 2004. Hatuo hiyo ni moawapo ya njia za kusitawisha msitu huo. Zimekuwa juhudi za kurejesha ardhi za msitu ambazo zimenyakuliwa. Wanaharakati wa usitawishaji mazingira na maafisa wa wizara ya ardhi wanakisia kwamba ardhi zilizonyakuliwa ni takriban hekari 40,000.

Maafisa wa serikali ya Kenya wamesema wameshangazwa na viwango na kasi ya watu kupata ardhi katika msitu wa Mau na uharibifu wa jumla wa msitu huo. Maafisa wa serikali na wafanyakazi wa kundi la kusitawisha mazingira linalohudumu katika eneo la Narok wamesema kwamba utafiti wao umeonyesha kwamba, watu kuishi Mau kinyume cha sheria na uharibifu wa msitu wa Mau umekuwa ukibadilisha jiografia nzima ya Mau na hivyo kusababisha vipindi virefu vya kiangazi, mito kukauka na wanyama kufa katika mbuga ya Maasai Mara.

Karibu asilimia 40 ya msitu leo hii imeharibiwa kwa ukataji miti na watu kuishi kwenye ardhi za msitu. Serikali inasema zaidi ya watu 50,000 wamejipatia ardhi katika msitu kinyume cha sheria tangu mwaka 1974. Kwa mujibu wa kundi la wasitawishaji mazingira linalohudumu Narok, baadhi ya watu hao wameweza kupata hati- miliki za ardhi wakisaidiwa na maafisa serikalini walio wafisadi. “Siku hizi kukinyesha, tunashuhudia mafuriko, viwango vya mvua ni vya juu sana na mvua ikiisha hupotea kabisa,” afisa mmoja wa kundi hilo la wasitawishaji mazingira anasema. “Wakati wa kiangazi cha majuzi mwaka 2009 na 2019, mto Mara na mito mingine katika eneo la Mau ilikauka kabisa. Msitu wa Mau ungekuwa jinsi ulivyokuwa miaka 50 iliyopita, mito hiyo isingekauka kabisa.”

Afisa wa wizara ya ardhi katika kaunti ya Narok alisema serikali inanuia kurejesha ardhi ambayo wakazi waliipata kinyume cha sheria, katika sehemu ya 22, Maasai Mau, ya msitu wa Mau upande wa kaunti ya Narok. Serikali ya Kenya ilitoa ardhi ya msitu kwa makundi ya wanambuga – ardhi za hekari kati ya 200-250 kwa shughuli za kilimo na za kibiashara, ambazo zinaidhinishwa na sheria za Kenya, na kwa watu binafsi – kati ya mwaka 1973 na 1985. Hatua hii ilifwatiwa na mpango mwengine wa ugawaji ardhi za msitu mwaka 2001. Lakini maafisa wa wizara ya ardhi wanasema baadhi ya makundi ya wanambuga yalisongesha mipaka kinyume cha sheria hadi kuingia katika msitu ama kuzigawa ardhi hizo na kuwapa watu, badala ya makundi, jinsi masharti yalikuwa yametaka.

Tangu mwaka 2004, serikali ya Kenya imekuwa ikijaribu kusitawisha msitu wa Mau. Kati ya mwaka 2004 na 2006 watu 100,000 waliondolewa huku oparesheni ikiwa yenye dhuluma nyingi. Haya ni kwa mujibu wa shirika la Amnesty International tawi la Kenya na Tume ya taifa ya Haki za binadamu KNCHR. Mahakama kuu mjini Nakuru ilikomeshwa oparesheni hiyo kufwatia ombi la watu saba waliokuwa na hati –miliki, licha ya serikali kusema kwamba ilikuwa imezipiga marufuku. Mahakama ilisema serikali haina nguvu za kisheria za kupiga maruku hati-miliki bila idhini ya korti.

Mwaka 2018 serikali iliomba idhini ya mahakama kupiga marufuku hati -miliki za baadhi ya watu wanaoishi msitu wa Mau ikisema ardhi wanazomiliki pale msituni zilipatikana kinyume cha sheria. Mahakama ilitoa idhini mwezi Juni mwaka 2019, ikaipa serikali ruhusa ya kupiga marufuku hati- miliki kabla oparesheni mpya ya kuwaondoa watu. Kulingana na maagizo ya mahakama oparesheni ya kuwaondoa watu itashirikisha wote wakiwemo wenye hati-miliki. Serikali imeliambia shirika la Human Rights Watch kwamba itawafukuza wote waliopata ardhi kinyume cha sheria wawe na hati-miliki ama la.

Tarehe 7, mwezi Julai, 2018, serikali ilianza awamu ya kwanza ya kuwaondoa watu katika ardhi za msitu wa Mau. Awamu ya pili iliratibiwa kufanyika mwaka 2019, lakini viongozi katika jamii za eneo la Rift Valley na wanasiasa wameionya serikali dhidi ya kuwafukuza watu kabla kesi iliyowasilishwa mahakamani Nakuru isikizwe na kuamuliwa. Kesi hiyo ilikuwa ya kupinga mpango mpya wa kuwafukuza watu Mau, mpango wa 2018.

Sera za serikali ya Kenya kuhusu ardhi zimechangia pakubwa katika watu kunyakua ardhi za msitu katika muda wa miaka 50 iliyopita, imesema ripoti ya mwaka 2010 ya jopo- kazi lililochunguza swala la msitu mzima wa Mau.Ardhi hizo zimenyakuliwa kupitia hatua za serikali kuziondoa baadhi ya ardhi miongoni mwa ardhi umma za misitu, serikali kutenga ardhi za misitu kwa kazi fulani fulani, na kuwapa watu fulani ardhi mara nyingi kwa njia zilizo- kinyume.

Hatua ya serikali ya kutenga sehemu ya ardhi za msitu na kuyapa makundi ya wanambuga kati ya mwaka 1973 na 1985 huku watano kati ya wanambuga hao wakisongesha mipaka yao na kuingilia misitu ni mfano hai. Watano hao ni Sisian, Enkaroni, Enosokon, Anakishomi na Reiyo, ambao kwa ujumla waliongeza maeneo waliyopewa kwa hekari 1,807 zaidi. Haya ni kwa mujibu wa maafisa katika wizara ya ardhi. Mwaka 2001, serikali ilichukua ardhi nyengine iliyokuwa imetambulika kuwa ya msitu wa Mau ya ukubwa wa hekari 61,587 na kuwapa watu binafsi. Tangu mwaka 2001, jamii za watu zimeingilia na kuchukua ardhi ya ukubwa wa hekari 29,000. Katika kipindi hicho hicho, maafisa wa serikali walitoa ardhi kinyume cha sheria ya ukubwa wa hekari 17,000 katika eneo la upande wa Maasai la msitu wa Mau.

Mpango wa kuwafukuza watu mwituni Mau wa mwaka 2018

Mwezi Juni 2019, Human Rights Watch ilitembelea kambi za watu waliokuwa wameondolewa katika ardhi za Mau, Narok, na kuwahoji watu 67 wakiwemo waathiriwa wa oparesheni ya kuwafukuza watu, viongozi katika jamii, baadhi ya walioshuhudia, wasitawishaji mazingira, maafisa wa Huduma ya wanyama pori, Huduma ya walinzi wa misitu ya Kenya, maafisa tawala katika serikali ya taifa, wizara ya ardhi, wizara ya mazingira na wapelelezi wa polisi. Human Rights Watch imeshirikiana kwa karibu na mashirika rafiki katika eneo la Narok ili kuwapata watu waliofukuzwa Mau na vilevile viongozi katika jamii. Hatimaye tumelinganisha habari tuliyopewa na habari waliyonayo maafisa wa serikali na maafisa wa polisi. Watafiti wa Human Rights Watch walilenga zaidi ukiukaji wa haki ambao umefanywa wakati wa oparesheni ya kuwafurusha watu kutoka Maasai Mau ya mwezi Julai 2018, katika kaunti ya Narok.

Vifo, watu wasiojulikana walipo

Human Rights Watch imepata kwamba karibu watu tisa walifariki huku wengine wasijulikane walipo kufwatia oparesheni ya kuwafukuza watu kutoka msitu wa Mau. Walioshuhudia na waathiriwa walisema kuwa walinda usalama kwenye oparesheni walifyatua risasi angani kutisha, wapo waliowalenga risasi watu waliokuwa wakitoroka, lakini wengi waliokufa walikuwa ni wale walioanguka wakati wakitoroka oparesheni. Mwezi Juni 2019, watafiti waliona mabaki ya miili wa mwanamume na mwanamke. Watu walioshuhudia oparesheni walisema miili hiyo ilikuwa ya watu waliofariki baada ya kupigwa risasi na polisi na kuachwa hapo.

Jamaa mmoj wa waathiriwa alisema tarehe 8 Julai, 2018, Sharon Chepkoech wa umri wa miaka 5 alianguka kutoka kwa mgongo wa mamaye wa umri wa miaka 26, huku mamaye akitoroka oparesheni ya kuwafukuza watu. Walinda usalama walikuwa wameharibu nyumba yao na kubomoa ghala lao la chakula. Mtoto Sharon alifariki katika kambi ya Masaita wiki moja baada ya kuanguka. Jamaa yake alisema.

Katika kisa kingine, mtu wa umri wa miaka 39- alisema mamaye wa umri wa miaka 52, Elizabeth Tuwei, alifariki katika hospitali ya Tenwek, kaunti ya Bomet mwezi Septemba 2018, baada ya kupelekwa punde baada ya oparesheni ya kuwafukuza watu Mau. “Walinda usalama waliokuwa wakiendesha oparesheni walikuja na misumemo ya umeme, ambayo walitumia kuharibu kila kitu, ikiwemo maghala ya chakula, mimea ya chakula mashambani na pia kuangush nyumba,” alisema Richard Ng’eno, mwanawe Elizabeth. “Mamangu alipatwa na mshituko akaanguka na kupoteza fahamu mwezi Julai wakati oparesheni ilianza. Tukamkimbiza katika hospitali ya Tenwek lakini alifariki”. Mwathiriwa mwengine, Richard Tanui, jirani ya Elizabeth Tuwei, alikuwa akitoroka walinda usalama alipoanguka katika mtaro katika kijiji cha Oruwuit na kufariki papo hapo, jamaa zake walisema.

Jamaa wa mwanamke wa umri wa miaka 20 Sharon Ng’etich na msichana wa miaka 12 Mercy Chepkoech, aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi ya Reiyo, wote wakiwa wa kambi ya Chepalungu, walisema wawili hao hawajaonekana tangu ile siku ya oparesheni. Mumewe Sharon alisema: “Mke wangu aliathirika vibaya kisaikolojia na oparesheni hiyo, na alitoweka tu wakati oparesheni ilikuwa bado inaendelea. Aliniachia watoto watatu na hadi leo hatujamwona.”

Manusura mmoja alisema, tarehe 7 Julai, katika kijiji cha Lebekwet, kundi la kuendeleza oparesheni, lililowajumuisha polisi wa utawala na maafisa huduma kwa wanyama pori, walimfwata mwanamume wa umri wa miaka 24, Emmanuel Sigei, na kuanza kumpiga “Walimpiga kwenye shingo, mgongoni na kiunoni kwa kutumia kipande cha mti hadi akapoteza fahamu. Halafu wakachimba shimo na kutaka kumzika na hali alikuwa hai. Walifikiria alikuwa amefariki. Lakini watu wakapiga kelele na kuwafanya wakome. Tangu siku hiyo hakuna mtu amemwona Sigei tena. Huenda alifariki.

Wengine waliofariki alikuwemo Gideon Kipkoech, aliyekuwa katika umri wa miaka ya 30, alikuwa mlemavu aliyekosa chakula hadi akafa baada ya walinda usalama kumburura kutoka nyumbani kwake na kumwacha nje ya nyumba kwa siku kadhaa. Samuel Pere, wa jamii ya Maasai akiwa katika umri wa miaka ya 50, alifariki mwezi Septemba,2018, wakati wa fujo baina ya jamii ya Kalenjin, waliopinga kufurushwa kwa watu, na Maasai, waliounga mkono oparesheni hiyo. Wamaasai wanasema kukauka kwa mito kumekuwa kukisababisha vifo vya wanyama katika mbuga maarufu ya Maasai Mara, hali ambayo inaathiri sekta ya utalii. Wanasema sekta hiyo ndiyo muhimu sana kwa jamii ya Maasai katika kaunti ya Narok kwa sababu inachangia pakubwa katika mapato yao ya kifedha. Miili mingine miwili ya watu waliofariki wakati wa oparesheni ilikuwa bado kuchukuliwa katika msitu wakati Human Rights Watch ilizuru eneo hilo.     

Kuwapiga watu na kuiba

Wote waliohojiwa walisema kuwa ushirikiano wa walinda mbuga za wanyama pori, walinzi wa misitu, kundi la usalama la serikali ya kaunti na polisi wa utawala waliyavamia maboma ya watu saa kumi na mbili asubuhi kwa siku tano mfululizo, wakafyatua risasi angani kuwatawanya watu, kuwapiga watu, kuteketeza nyumba za wakazi, wakaharibu mimea ya chakula, na kuiba bidhaa za kinyumbani katika nyumba za watu na chakula kwenye maghala. Hata hivyo maafisa wa serikali wamekanusha habari hizi wakisema oparesheni haikuwa yenye dhuluma wala kufanywa kwa nguvu.

Mhudumu mkuu katika Huduma ya wanyama pori, Dickson Ritan, aliyekuwa kiongozi wa oparesheni ya kuwaondoa watu Mau alisema: “Utaratibu ulifanywa kwa njia tulivu. Watu hawakufukuzwa. Waliombwa tu kuondoka wenyewe na kazi hii ilichukua siku tatu. Tuliwasaidia watu kubeba vitu vyao kutoka kwenye nyumba zao.” Naibu kamishna wa kaunti ya Narok, Arthur Bunde, aliyekuwa miongoni mwa kundi la kufanya oparesheni, alisema mpango huo kwa kiwango kikubwa ulikuwa wa amani, ni wale waliokataa kutii maagizo ndio waliondolewa kwa nguvu. Hapakuwa na visa vya walinda usalama kuiba mali ya watu.

Waathiriwa wote 67 tuliowahoji, wakiwemo wale waliokuwa wamenusurika oparesheni bila kupigwa na kujeruhiwa, walisema walinda usalama walitumia nguvu za kupit kiasi ikiwemo kuwapiga watu risasi. Mwanamume mmoja wa umri wa miaka 35 katika kambi ya Masaita, alisema wakati walinda usalama walivamia nyumba yake tarehe 8 July, walivunjavunja duka lake na kuliharibu. Alisema waliteketeza nyumba zake, wakaharibu mimea ya chakula, wakampiga yeye na mamaye. Mamaye, Ruth Sigei Laboso, wa umri wa miaka 55, alianguka na kuvunjika mguu alipokuwa anajaribu kutoroka, Akasema.

Babu mmoja wa umri wa miaka 93 alisema polisi walivamia boma lake katika kijiji cha Ororuit tarahe 8 mwezi Julai, wakampiga yeye na watoto wake 10, wakateketeza nyumba tatu, wakaharibu nguo na mimea ya chakula. Polisi walimpiga mmoja wa watoto wake, Bernard Kiprotich, wa umri wa miaka 30, wakitumia kipande cha mti wakampiga kwenye kisogo, wakamjeruhi vibaya. Walimpokonya Kiprotich shilingi 30,000 (USD300) bila kuzirejesha. Kiprotich alitoa taarifa ya kisa hicho katika kituo cha polisi cha Malelo lakini polisi bado kuanzisha uchunguzi wowote.

Karibu watu 30 waliohojiwa wote walisema kundi la walinda usalama walioendesha oparesheni waliiba mali na vifaa vya kinyumbani, waliharibu maghala ya chakula huku wakiiba baadhi ya chakula. Julius Bor, wa umri wa miaka 48 alisema polisi waliteketeza ghala lake la chakula lililokuwa na magunia 30 ya mahindi, magunia 150 ya mahindi, 15 ya viazi, na tatu ya vitunguu. Watu watatu tuliowahoji, mmoja katika eneo la Gorofa, wengine katika eneo la Chepalungu, walisema walinda usalama kwenye oparesheni walichinja mbuzi kondoo na ng’ombe na kuandaa karamu siku za oparesheni.

Kukosa kufwata kanuni za kuwahamisha watu

Shirika la Human Rights Watch limepata kwamba serikali ya Kenya imeshindwa kutii na kuheshimu sheria za hapa nchini na zile za kimataifa, zinazosema kwamba waathiriwa wote wa mipango ya kuwahamisha watu wana haki ya kufidiwa na vilevile kupewa makao mapya. Maafisa wa serikali katika kaunti ya Narok wamewaambia watafiti wa Human Rights Watch kwamba serikali haitawalipa fidia ama kuwapa makao mapya waathiriwa, kwa sababu walikuwa wanaishi katika ardhi za umma zilizotengwa kuwa msitu.

Mbali na hayo, serikali haikutoa muda wa kutosha kwa watu hao kuondoka msituni. Maafisa wa serikaliwalisema waliwatangazia watu hao mwezi mmoja kabla ya kuanza oparesheni na baadaye wakawapa notisi ya wiki mbili. Hata hivyo, kanuni za kuwahamisha watu kutoka eneo fulani hutaka muda wa notisi kuwa siku 90, huku notisi ikitolewa moja kwa moja kwa kila mtu anayelengwa. Wote tuliowahoji wamesema watu hao hawakujua kwamba oparesheni ya kuwaondoa msitu yaja.

Kanuni za kuwaondoa watu katika eneo fulani hutaka maafisa wa serikali kufanya mashauriano baina ya serikali na walengwa ili mpango wa kuondolewa ujadiliwe, wazungumzie kuondolewa pale walipo huku wakiwapa habari zote muhimu kuhusu eneo watakalokwenda na fidia watakayolipwa. Kanuni hizo zinasema: “Serikali itahakikisha kwamba, kukitokea ukosefu wa kuelewa kuhusu ni wapi wanaohamishwa watakwenda, makundi na jamii zinazohamishwa na kundi linaloendesha oparesheni ya kuzihamisha, basi kutofautiana huko kutafikishwa mbele ya kamati maalum ya usuluhishi inayojumuisha wawakilishi wa jamii zinazolengwa kuhamishwa, maafisa wa wizara ya ardhi , wawakilishi wa kundi la kuongoza oparesheni ya kuwafurusha, na mwakilishi wa Tume ya taifa kuhusu haki za binadamu.”

Kanuni hizo hutaka serikali ichukue hatua thabiti kuhakikisha kwamba hapatokei hali ya watu kupokonywa mali yao au kupoteza mali wakati wa kuondolewa pale wanapoishi. Mali inayoachwa nyuma wakati wa kuhamishwa pia yafaa ilindwe isiharibiwe au kuchukuliwa na kutumiwa na watu wengine.

Lakini waathiriwa wa mpango wa kufurushwa katika msitu wa Mau walisema hakuna hata mmoja amelipwa fidia huku maafisa husika wakiwa bado kuandaa orodha ya wale waliofurushwa kwa lengo la kufidiwa ama kupewa makao mapya. Tangu July 2018, waziri wa Mazingira Keriako Tobiko amekuwa akisema na kurejelea kwenye vyombo vya habari kwamba hakuna hata mmoja kati ya waliofurushwa mwituni atalipwa fidia kwa sababu wote walikuwa wameingilia ardhi ya serikali na kuanza kuishi.

“Badala ya kutafuta pesa za kuwafidia ama kuwapa makao, tunataka warejee kule walitoka. Baadhi yao tayari wamerejesha hati-miliki kwa hiari na kurejea kule walitoka,” alisema Arthur Bunde, naibu Kamishna wa kaunti ya Narok.

Ukosefu wa kuwajibikia dhuluma na ukiukaji haki

Hata kama vyombo vya habari vya Kenya vimekuwa vikiangazia pakubwa dhuluma zinazotokea kwenye oparesheni za kuwafurusha watu Mau, baadhi ya watu wamesema walitoa habari za kupigwa na uharibifu wa mali kwa polisi, lakini Human Rights Watch imepata kwamba serikali ya Kenya ingali kuanzisha uchunguzi wowote. Afisa wa ngazi za juu serikalini akizungumza akiwa Narok alisema baada ya oparesheni hiyo serikali ilifanya uchunguzi, uliojumuisha mambo mengi ikiwemo “nyumba ngapi ziliteketezwa na ziliteketezwa wapi” Lakini serikali bado haijatoa ripoti hiyo kwa umma.

Afisa wa polisi wa ngazi za juu katika kaunti ya Narok anayehudumia idara ya upelelezi wa jinai CID alisema kwamba, hata kama amepewa jukumu la kuongoza kundi la kuchunguza mambo yanayohusu kuwafurusha watu kutoka msitu wa Mau, hawajashughulikia dhuluma dhidi ya watu wakati wa oparesheni. Afisa wa Huduma ya wanyama pori mjini Narok ambaye amehusika katika kuwafurusha watu kutoka msitu huo alisema serikali haijachunguza dhuluma kwa sababu hazikuwepo. “Hakuna mtu ameripoti dhuluma zozote zile, iwe mauaji ama kupigwa. Utaratibu wa kuwaondoa watu umefanywa kwa amani. Maafisa wetu waliandamana tu nao wakiondoka msituni.”

Karibu watu 57 tuliowahoji walielezea jinsi walinda usalama kwenye oparesheni waliiba vitu nyumbani kwao na chakul kwenye maghala yao na kuwavuruga watu. Karibu watu 30 walisema wametoa taarifa rasmi kwa polisi, ikiwemo kuhusu vifo vilivyotokana na oparesheni hiyo. Taarifa hizo zimetolewa kwa vituo vya polisi lakini hapajakuwa na uchunguzi wowote.

Polisi wameshindwa kuingilia kati vurugu za kijamii zilizosababishwa na mpango wa kuwafurusha watu Mau. Jamii ya Maasai inayounga mkono mpango wa serikali kusitawisha msitu wa Mau, ikiwemo hatua za kuwafukuza watu mwituni, huku jamii ya Kalenjin, ikiwa ndiyo iliyoingia mwituni tangu mwaka 1974, inapinga mpango wa serikali. Karibu familia mbili za kimaasai, ikiwemo moja iliyopoteza jamaa yao wakati wa vurugu za kijamii mwezi Septemba, ilisema polisi wameshindwa kuanzisha uchunguzi wa vurugu hizobaina ya jamii hizo licha ya kuwa familia zilizoathirika zimetoa taarifa rasmi katika vituo vya polisi.

Familia ya William Pere, ambaye aliuawa kati kati ya mwezi Septemba katika msitu wa Mau, alipokuwa amekwenda kurejesha mifugo wake wakati vurugu zilianza, imesema imeandikisha taarifa rasmi katika vituo vya polisi vya Gorofa na Lulung’a. Licha ya kuwa maafisa wa polisi katika kituo cha Lulung’a kuwa eneo la kufanyika mkasa, hapajakuwa na uchunguzi zaidi na hakuna mshukiwa ametiwa nguvuni kufwatia uhalifu huo.

 

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country