Skip to main content

Tanzania: Ukiukaji wa Polisi, Mateso yanazuia huduma za Virusi Vya UKIMWI (VVU)

Watu walio katika hatari kubwa walazimika kwenda mafichoni kutokana na ubaguzi na kushambuliwa.

(Dar es Salaam) – Watanzania walio katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa VVU hukumbana na dhulumanyingi za polisi na mara nyingi hawawezi kupata usaidizi wanapokuwa waathiriwa wa uhalifu, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch na Shirika la “Wake Up and Step Forward Coalition” (WASO) yasema katika ripoti iliyotolewa leo.

Katika ripoti yenye kurasa 98 iliyopewa kichwa, “Tuchukulie kama wanadamu’: Ubaguzi dhidi ya wafanyakazi wa ngono, waliowachache kijinsia (LGBTI), na watumiaji wa dawa za kulevya nchini Tanzania,” inaeleza ukiukaji kama mateso, ubakaji, kushambuliwa, kukamatwa kiholela, na kunyang’anywa pesa. Mashirika haya yaligundua kwamba hofu ya kukiukwa inawalazimu wafanyakazi wa ngono; watumiaji wa dawa za kulevya; na wanawake wanaofanya mapenzi na wanawake, wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, wanaovutiwa na jinsia zote mbili, wanaotamani kubadilisha jinsi zao, na watu wenye jinsia mbili (LGBTI) kwenda mafichoni mbali na huduma za kinga na matibabu. Makundi haya yalifanya utafiti wao kutoka mwezi wa Mei 2012 hadi Aprili 2013, na yaliwahoji wanachama 121 wa makundi yaliyo katika hatari kubwa, pamoja na maafisa wa serikali ya Tanzania, wahudumu, na wasomi.

"Serikali ya Tanzania imeahidi katika maandishi kupunguza unyanyapaa dhidi ya makundi yaliyo katika hatari, lakini ahadi hiyo haina maana kama polisi wanawabaka, wanawanyanyasa na wanawakamata mara kwa mara," alisema Neela Ghoshal, mtafiti katika Programu inayolenga haki za waliowachache kijinsia (LGBTI) katika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch. "Sera ya serikali kuhusu VVU haiwezi kufanikiwa ikiwa polisi wanawafukuza mbali watu ambao programu za afya ya umma zinahitaji zaidi kufikia."

Mashirika haya mawili pia yalirekodi dhuluma mbalimbali dhidi ya makundi yaliyo katika hatari zaidi, ikiwa ni pamoja na kunyimwa huduma, unyanyasaji kwa njia ya matusi, na ukiukaji wa faragha katika sekta ya huduma za afya. Sera ya Tanzania kuhusu VVU/ UKIMWI inatoa wito kuwepo kwa juhudi za kupunguza unyanyapaa dhidi ya makundi yaliyotengwa, na mamlaka zimechukua baadhi ya hatua kufanya hivyo. Lakini mashirika ya Human Rights Watch na WASO yalitambua kesi nyingi ambapo wafanyakazi wa afya waliwafukuza wafanyakazi wa ngono, watu wa LGBTI na watumiaji wa dawa za kulevya kutoka vituo vya afya bila kuwahudumia, au kuwaaibisha hadharani.

 

Makundi haya pia yalirekodi juu ya watoto kunyanyaswa kingono. Ni marufuku kwa watoto kushiriki katika kazi ya ngono, lakini badala ya kuwalinda watoto hawa na kuwapa misaada, makundi haya yaligundua kuwa, polisi huwabaka, huwanyanyasa kingono, na huwapiga bila kuogopa kuchukuliwa hatua. Katika kisa kimoja, msichana mwenye umri wa miaka 12 anayefanya kazi ya ngono Mbeya alibakwa na kundi la maafisa wa polisi. Polisi wanaowanyanyasa watoto hawa wanapaswa kuchunguzwa na kushitakiwa.

Makundi haya yalibaini kuwa makundi ya usalama na yasiyo ya serikali, hasa Sungu Sungu, kundi la kujihami, pia yanahusishwa katika mashambulizi dhidi ya makundi yaliyo hatarini, mara nyingi yakiendesha shughuli zao kimabavu.

Ukiukaji huu wa haki za binadamu unachangia mazingira ambapo wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, wanaotamani kubadilisha jinsia zao, wafanyakazi wa ngono, na wanaojidunga dawa za kulevya wanazidi kukosa imani katika serikali. Hofu yao hukwaza juhudi za afya ya umma ambazo hutegemea ushirikiano na ubia kati ya serikali na makundi muhimu ambayo yako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa VVU.

Sera ya Tanzania kuhusu VVU inaahidi, miongoni mwa mikakati mingine, kuongeza upatikanaji wa kinga dhidi ya VVU na huduma kwa makundi muhimu; kujenga ubia na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayowakilisha makundi haya yaliyotengwa, na kufanya kazi inayolenga kuafikia uhalalishaji wa kazi ya ngono na mienendo ya mapenzi ya jinsia moja. Hata hivyo, kama ilivyogunduliwa na shirika la Human Rights Watch na WASO, mikakati hii imefanywa shingo upande.

Wanachama wa makundi yaliyo katika hatari kubwa pia hunyimwa habari kuhusu VVU. Kampeni za uhamasishaji wa umma kuhusu VVU kwa kiasi kikubwa zinawalenga tu wapenzi wa jinsia tofauti pekee. Mashirika mengi ya kijamii huamini kuwa hayawezi kutoa huduma kwa makundi yaliyoharamishwa, yakihofia kuwa kufanya kazi na makundi haya, kwenyewe, ni kinyume cha sheria. Watu wa LGBTI na wafanyakazi wa ngono wanasema kwamba hawawezi kuunda vikundi vyenye uanachama unaotambuliwa kisheria na kujisajili na serikali. Katika mwaka wa 2011, polisi walimkamata na kumpiga mwanaume mmoja anayefanya mapenzi na wanaume jijini Dar es Salaam kwa sababu alijaribu tu kuandaa warsha ya wanaume wanaofanya ngono na wanaume.

Sheria ya Tanzania huadhibu kosa la kufanya ngono ya hiari baina ya wanaume kwa kifungo cha miaka 30 gerezani, mojawapo ya adhabu kali zaidi kwa kosa la mapenzi ya jinsia moja kote ulimwenguni. Katika kisiwa kinachojitawala cha Unguja, sheria inaharamisha mahusiano kwa hiari ya kingono kati ya wanaume, kwa adhabu ya hadi miaka 14 gerezani, na kati ya wanawake kwa adhabu ya hadi miaka 5 gerezani. Hakuna mtu ambaye ameshtakiwa kwa kosa la mapenzi ya jinsia moja katika miaka ya hivi karibuni, lakini sheria inachangia kutengwa kwa watu wa LGBTI. Kazi ya ngono imeharamishwa Tanzania Bara na Unguja, sawia na umilikaji na utumiaji wa hata kiasi kidogo cha dawa za kulevya.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI (UNAIDS) linasema uharamishwaji wa makundi maalum unawalazimisha kwenda mafichoni na mbali na huduma za VVU, hivyo kusababisha kutengwa, kubaguliwa, na kushambuliwa zaidi. Tume ya Kimataifa Kuhusu VVU na Sheria (The Global Commission on HIV and the Law), tume ya wataalam iliyoundwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo (UNDP), pia linatoa wito kuhalalishwa kwa kazi ya ngono na mwenendo wa mapenzi ya jinsia moja miongoni mwa watu wazima wanaofanya hivyo kwa hiari.

Kuharamishwa kwa mahusiano ya hiari ya kingono miongoni mwa watu wazima ni kinyume cha baadhi ya haki za binadamu zinazotambuliwa kimataifa, zikiwemo haki ya faragha na kutobaguliwa. Kuharamishwa kwa ubadilishanaji hiari wa huduma za ngono ili kupata pesa miongoni mwa watu wazima, kama katika kisa cha kufanya kazi ya ngono kwa hiari miongoni mwa watu wazima, pia ni kinyume na haki ya faragha, ikiwa ni pamoja na uhuru wa mtu binafsi.

Rais Jakaya Kikwete anapaswa kulaani hadharani dhuluma za polisi, ubaguzi katika sekta ya afya, na aina nyingine zozote za ubaguzi dhidi ya wafanyakazi wa ngono, watumiaji wa dawa za kulevya, na watu wa LGBTI, mashirika ya Human Rights Watch na WASO yalisema. Polisi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinapaswa kutoa huduma kwa watu wote wanazozihitaji.

Mabunge ya Tanzania na Unguja yanapaswa kuhalalisha mienendo ya ngono kati ya watu wa jinsia moja na kazi ya ngono kwa hiari inayowashirikisha watu wazima, na kubadilisha sheria kuhusu dawa za kulevya ili kuhakikisha kwamba sheria hizo zinaambatana na haki za binadamu.

Wafadhili wanapaswa kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa kwa madhumuni ya kuzuia VVU/ UKIMWI na matibabu nchini Tanzania zinajumuisha fedha zinazolenga hasa mahitaji ya kiafya ya makundi haya maalum, na kuunga mkono ukuaji wa mashirika ya umma yanayowawakilisha.

"Kama Tanzania kweli imejitolea kushughulikia VVU/UKIMWI miongoni mwa makundi  maalum, inahitaji mpangilio unaojikita katika utaratibu wa haki," Ghoshal alisema. "Polisi na wafanyakazi wa afya wanapaswa kutoa ulinzi na matibabu kwa makundi yaliyo hatarini, badala ya kuweka mfano wa chuki na ulokole."

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country