Skip to main content

(Nairobi) – Ndoa za utotoni ndani ya Tanzania inapunguza upatikanaji wa eliumu kwa wasichana na inawaweka hatarini kupata madhara makubwa, Human Rights Watch imesema kwenye ripoti iliyotolewa leo. Human Rights Watch imenukuu kesi ambapo wasichana wenye umri wa hata miaka saba wanaolewa. Serikali inapaswa kuweka miaka 18 kuwa umri mdogo kwa wasichana na wavulana kama hatua ya kwanza katika kutokomeza ndoa za utotoni na kuboresha maisha ya wasichana na wavulana.  

Ripoti hiyo ya kurasa 75, “‘Hakuna Jinsi’: Ndoa za Utotoni na Ukiukwaji wa Haki za Binadamu ndani ya Tanzania,” imenukuu jinsi ndoa za utotoni zinavyozuia upatikanaji wa elimu kwa wasichana, na kuwaweka hatarini kufanyiwa unyanyasaji na ukatili – ikiwemo kubakwa ndani ya ndoa- na hatari ya afya ya uzazi.  Human Rights Watch imepima mapengo kwenye mfumo wa hifadhi ya mtoto ndani ya Tanzania, ukosefu wa hifadhi kwa wahanga wa ndoa za utotoni, na vipingamizi vinavyowakabili wasichana wakijaribu kupata haki, pamoja na mapungufu kwenye sheria zilizopo na mipango ya serikali kupambana na ndoa za utotoni.

“Kwa bahati mbaya rasimu ya mwisho ya katiba ya Tanzania haijaweka umri mdogo wa ndoa,” amesema Brenda Akia, mtafiti wa haki za wanawake Human Rights Watch na mwandishi wa ripoti hiyo. “Serikali ya Tanzania inapaswa kuonyesha kuongoza kwenye ndoa za utotoni kwa kufanya miaka 18 kuwa umri mdogo kwenye Sheria ya Ndoa na kutoa hifadhi imara zaidi dhidi ya ndoa za watoto.”
 

Ripoti hiyo ya Human Rights Watch imejikita kwenye mahojiano ya kina na wasichana na wanawake 135 kwenye wilaya 12 za Tanzania, pamoja na watumishi wa serikali, wanaharakati wa mahalia na watumishi wa mashirika ya kimataifa.

Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971 imeweka umri mdogo wa kuoa kuwa miaka 18 kwa wavulana na miaka 15 kwa wasichana kuolewa kwa ridhaa ya wazazi. Pia inaruhusu wasichana na wavulana kuoa na kuolewa wakiwa na miaka 14 kwa ruhusa ya mahakama. Bunge Maalum la Katiba, lililopewa kazi ya kuandika katiba mpya, imekosa fursa ya kuweka umri mmoja mdogo wa kuoa au kuolewa  kwenye rasimu yake ya mwisho Oktoba 2014, Human Rights Watch imesema.

Serikali ya Tanzania imepanga kufanya mapitio ya Sheria ya Ndoa, kutokana na mapendekezo kutoka kwa Tume ya Marekebisho ya Sheria ya Tanzania , na itakamilisha nyaraka ya serikali kwa ajili ya maoni ya wananchi baada ya kumalizika kwa mchakato wa mapitio ya katiba.

Ingawa kiasi cha ndoa za utotoni ndani ya Tanzania kimepungua miaka ya karibuni, bado kimebaki kuwa juu kwa viwango visivyokubalika, Human Rights imesema. Wanawake wanne kati ya 10 wa Kitanzania wanaolewa kabla ya kutimiza miaka 18, kwa mujibu wa takwimu za serikali.

Anita, mwenye miaka 19, alilazimishwa na baba yake kuolewa akiwa na miaka 16, akiwa anasoma kidato cha pili. “Baba yangu hakuwa na pesa ya kunisomesha,” amesema. “Kisha nikagundua alikuwa amekwisha pokea mahari ya ng’ombe 20 kwa ajili yangu.”

Judith alikuwa na miaka 14 na anafanya kazi kama mfanyakazi wa nyumbani alipoolewa ili kutoka kwenye unyanyasaji na utumikishwaji aliofanyiwa na mwajiri wake. “Mfanyakazi wa ndani wa kiume kwenye nyumba niliyokuwa ninafanya kazi aliniomba anioe,” amesema. “Nilikubali- kwa sababu niliona ndoa kama njia yangu ya pekee kutoka kwenye mateso ya bosi wangu.”

Wasichana waliiambia Human Rights Watch kwamba familia zao ziliwalazimisha kuolewa ili wapate mahari. Kwa sababu hawakuthamini elimu ya mabinti zao, na kwa sababu wasichana walikuwa na mimba au familia zao ziliogopa kuwa wangepata mimba na kuleta aibu kwenye familia. Wasichana wengine waliona ndoa kama njia ya kutoka kwenye umaskini, ukatili, utekelezaji au utumikishwaji wa watoto.

Sera za kibaguzi na zisizo wazi na utendaji wa serikali unawezesha ndoa za utotoni, na kudhoofisha kwa kiasi kikubwa elimu na fursa za wasichana, Human Rights Watch imesema. Shule nyingi za Tanzania zina vipimo vya mimba vya lazima. Pia serikali inaruhusu shule kuwafukuza au kukatisha masomo ya wanafunzi walioolewa au wanafunzi wanaofanya makosa dhidi ya “maadili mema,” ambayo yanatambulika kwa wingi kujumuisha ngono kabla ya ndoa.

Mtihani wa Serikali wa Kuhitimu Elimu ya Msingi, ambao unaamua mwanafunzi gani anaweza kuendelea na shule ya sekondari, pia unawaweka wasichana hatarini kuingia kwenye ndoa za utotoni, Human Rights Watch imebaini.

Salia J., 19, alilazimishwa kuolewa akiwa na miaka 15 baada ya kufeli mtihani wa kuhitimu. “Baba yangu aliamua kunitafutia mwanaume wa kunioa kwa sababu nilikuwa ninabaki nyumbani sifanyi chochote,” amesema.

“Vipimo vya mimba vya lazima na kuwafukuza wasichana wenye mimba na walioolewa shule inakiuka sana haki zao, hasa ya kupata elimu, “Akia amesema. “Serikali inapaswa kufuta kanuni zake za kibaguzi na kuwawezesha wasichana wenye mimba na waliozaa kuendelea na elimu yao.” 

Ndoa za utotoni zinawaweka wasichana na wanawake hatarini zaidi kufanyiwa ukatili wa kijinsia, Human Rights Watch imesema. Wasichana wanaokataa ndoa au wanaojaribu kukataa wamesema familia zao ziliwashambulia na kuwafanyia unyanyasaji wa maneno au kuwafukuza. Wale wanaoshindwa kutoroka ndoa wamesema waume wao waliwapiga na kuwabaka na hawakuwaruhusu watoe uamuzi wowote kwenye nyumba kuhusu maisha yao.

Idadi kubwa ya wale waliohojiwa wamesema waume wao waliwatelekeza na kuwaacha wawatunze watoto bila msaada wowote wa kifedha. Katika matukio mengine, wasichana walifanyiwa ukatili na unyanyasaji mikononi mwa wakwe zao. Wasichana wanaotoka kwenye makabila ya Kimasai na Kigogo wamesema walilazimishwa kukeketwa ili kuwaandaa kwa ajili ya ndoa.

Serikali inapaswa kufanya kazi ili kufanya maboresho ya sheria za ndoa na talaka, ikiwemo kuweka umri mdogo wa ndoa kuwa miaka 18, Human Rights Watch imesema. Inapaswa kutunga sheria ya ukatili wa kijinsia ikiweka ukatili wa kingono ndani ya ndoa kuwa kosa la jinai na kuandaa mpango kazi wa kitaifa wa kuzuia na kushughulikia matokeo ya ndoa za utotoni.

Serikali inapaswa kutokomeza vipimo vya mimba shuleni, kuruhusu wasichana wenye mimba na walioolewa kubaki shuleni, na kuchukua hatua zote za muhimu kuwaruhusu watoto wote kuhudhuria shule ya sekondari bila kujali matokeo ya Mitihani ya Kuhitimu Elimu ya Msingi.

“Ndoa za utotoni zina athari mbaya za muda mrefu kwa wasichana na wanawake,” Akia amesema. “Serikali ya Tanzania inapaswa kuchukua hatua za papo ka hapo na za muda mrefu kutokomeza utendaji huo, na kuwapa wahanga msaada wa kisaikolojia, kijamii, na kiuchumi.”

 

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Region / Country