Mwezi Agosti Mwaka 2022, Kenya ilifanya uchaguzi wa urais uliofwatiwa na mzozo wa kupinga uchaguzi huo ulioelekezwa Mahakamani. Mgombeaji wa kiti cha urais wa upande wa upinzani Raila Odinga alipinga matokeo yaliyotangazwa. Mahakama ya juu ya Kenya ilitupa kesi hiyo kwa kukosa ushahidi na kumtangaza William Ruto kuwa mshindi. Ruto aliapishwa punde baadaye na akaunda serikali. Upande wa upinzani haukuridhishwa na uamuzi wa Mahakama hivyo ukaamua kuandaa maandamano. Licha ya Rais Ruto, wakati wa kampeni, kuahidi kutii haki za binadamu, mwelekeo wa utiifu wa Haki za kimsingi nchini Kenya umekuwa ukivurugwa mwaka mzima, tangu Ruto awe rais wa Kenya.
Mashirika ya Haki za Binadamu ya Kenya na yale ya Kimataifa yamekuwa yakilaumu idara ya polisi ya Kenya na taasisi nyingine za usalama kwa kuhusika kwenye ukiukaji wa haki za kimsingi. Ukiukaji huo unashirikisha kuwauwa watu kiholela. Mamlaka nchini Kenya imeshindwa kuhakikisha kwamba wahusika kwenye ukiukaji huu wanawajibikia makosa yao, vilevile imeshindwa kuanzisha uchunguzi dhidi ya maafisa wa polisi ambao walitajwa kwenye visa vya kukiuka haki wakati wa maandamano ya upinzani yaliyofanyika Mwaka 2023. Mkurugenzi wa Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP), alitangaza kuondoa mashtaka dhidi ya maafisa wakuu katika serikali, wakiwemo wale walioshutumiwa makosa ya ukiukaji wa Haki za Kimsingi. Hali hiyo inaweza kuwa na athari siku za usoni hasa kwenye juhudi za Kenya za kushughulikia mojawapo ya matatizo makuu yanayoikumba nchi ambayo ni watu kufanya makosa bila kuchukuliwa hatua za kiesheria.
Dhuluma kufanywa na polisi
Maafisa wa Polisi nchini Kenya walikabili maandamano yaliyoandaliwa na muungano mkuu wa upinzani, Azimio la Umoja kwa nguvu za kupita kiasi. Waandamanaji walishinikiza serikali ichukue hatua za kupunguza gharama ya maisha na vilevile kuchunguza madai ya udanganyifu kwenye uchaguzi mkuu wa Mwaka 2022. Mashirika ya Haki za Binadamu, Human Rights Watch na Amnesty International yalirekodi mauaji ya yamkini watu 16 huku waandamanaji wengi wakijeruhiwa baadhi wakiwa kwenye shughuli zao, huku polisi wakiwapiga risasi watu hata waliokuwa nyumbani kwao. Mbali na polisi kuendesha shughuli za kukomesha maandamano, yalikuwapo makundi ya watu waliojihami yasiyokuwa polisi, lakini yaliwakabili waandamanaji kwa niaba ya serikali.
Wakati wa maandamano ya Mwezi Machi, makundi yaliyojihami yalishambulia na kuiba kwenye kampuni zinazomilikiwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, na rais wa nne wa Kenya Uhuru Kenyatta, katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Serikali ilimshutumu Kenyatta ikidai alikuwa akifadhili maandamano hayo. Mwezi Julai makundi yaliyojihami yakishirikiana na maafisa wa polisi, yaliwapiga na kuwafyatulia risasi watu waliokuwa wakiandamana kwa amani kwenye barabara za jiji la Kisumu, Magharibi ya Kenya na jijini Nairobi, hasa kwenye makao ya watu wenye mapato madogo ya Kibera na Mathare. Kulikuwapo vilevile malalamiko kuhusu kuongezeka kwa dhuluma za kimapenzi kufanywa na maafisa wa polisi na wahusika wa dhuluma wasiokuwa polisi. Dhuluma za kimapenzi mara nyingi huandamana na misukosuko ya kisiasa nchini.
Kufikia wakati wa kuandaa ripoti hii Mamlaka ya kutathmini utendakazi wa Polisi nchini Kenya (IPOA) bado haikuwa imekamilisha uchunguzi wa vifo na madai ya polisi kutumia nguvu za kupita kiasi wakati wa kuwakabili waandamanaji. Kenya ina historia ndefu ya polisi kutumia nguvu za kupita kiasi dhidi ya waandamanaji kila msimu wa baada ya uchaguzi. Hali hii imekuwa ikirejelewa wakati matokeo ya uchaguzi yamepingwa. Hatua chache zimechukuliwa kuhakikisha kwamba wanaohusika makosa wanachukuliwa hatua kwa kuhusika dhuluma hasa zinazofanywa na polisi. Imekuwa ndiyo hali inayoikumba Kenya kila badaa ya uchaguzi tangu uchaguzi wa mwaka 2017, 2013, na 2007.
Kundi lenye itikadi kali za dini na makaburi ya jumla ya Malindi
Mwezi Aprili, serikali iligundua makaburi ya siri ya wafwasi wa “kundi la kidini la kufunga bila chakula” kwenye msitu katika eneo la Shakahola kilomita kadhaa kutoka mji wa mwambao wa pwani ya Kenya wa Malindi. Mamlaka nchini Kenya ilisema Mwezi Septemba Mwaka 2023 kwamba ilikuwa imechimbua makaburi kadhaa ya waathiriwa ikiwemo jumla ya maiti zaidi ya 400 ya wafwasi wa kundi hilo lenye itikadi kali za kidini. Waathiriwa wengi walikuwa wamenyongwa au kupigwa hadi kufa wala haikuwa kwamba wote walifariki kutokana na kufunga na kwenda bila chakula. Hata hivyo uchunguzi wa Shirika la Human Rights Watch umepata kwamba ni maiti 12 tu ndizo zimetambuliwa rasmi lakini hakuna maiti iliyorejeshewa familia husika ili kufanyiwa maziko rasmi.
Polisi walisema wamemtia nguvuni mhubiri aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo, Paul Makenzie, na yamkini wafwasi wake 37. Mawakili na Mashirika ya Haki ya Kenya yameelezea masikitiko katika ukiukaji wa haki za kimsingi wa watu ambao wameshikwa, kwa kushirikishwa na Mhubiri Makenzi. Mhubiri huyo amezuiliwa kwenye seli mara nyingi akiwa pekee kwa miezi kadhaa licha ya kwamba hajashtakiwa rasmi huku watuhumiwa wenzake wakinyimwa idhini ya kukutana na familia zao au hata mawakili.
Changamoto za uwajibikaji
Tangu Mwezi Septemba Mwaka 2022, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ametupa kesi kadhaa za ufisadi na zinazohusu ukiukaji wa Haki za Binadamu dhidi ya wandani wa rais Ruto, miongoni mwao wamo walioteuliwa kuwa mawaziri. Hali ya kuondoa kesi Mahakamani bila kufwata utaratibu wa kisheria ina uwezekano wa kuharibu juhudi za Kenya za kukabili ufisadi na ukiukaji mwingine wa Haki za binadamu. Baadhi ya watalamu wa maswala ya sheria wamesema serikali ya Kenya imeondoa karibu kesi 30 za watu wenye ushawishi mkubwa, kutoka kwenye utaratibu wa Mahakama, katika kipindi cha miezi saba tangu Rais Ruto achukue mamlaka nchini Kenya.
Miongoni mwa kesi zilizoondolewa Mahakamani zimo za watu wanaotuhumiwa makosa ya wizi wa mali ya umma, dhuluma za kimapenzi na mauaji kuwakabili watu hao ambao baadaye wameteuliwa kwenye nyadhifa za ngazi za juu serikalini.
Punde baada ya Ruto kuapishwa kuwa rais Mwezi Septemba Mwaka 2022, Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma alitangaza mpango wa kusuluhisha mambo nje ya Mahakama baina ya mbunge wa awali na mwanamke aliyekuwa amemshtaki kwa kujaribu kumbaka. Siku chache baada ya mwanamke huyo kuondoa kesi Mahakamani, Ruto alimteuwa mwanasiasa huyo kuwa waziri katika serikali yake. Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma (DPP) vilevile aliondoa kesi zingine dhidi ya mwanasiasa huyo, ikiwemo kesi zinazohusu ufisadi, uchochezi, na kutumia mamlaka vibaya.
Mwezi Oktoba, Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma vilevile aliondoa shutuma za ufisadi, dhidi ya mbunge wa awali wa Malindi ambaye baadaye rais alimteuwa kuwa waziri. Mwanasiasa huyo pamoja na wenzake wanane anakabiliwa na tuhuma za kuiba shilingi Milioni 19 (Dola za Amerika 155,700) kutoka hazina ya Maendeleo ya eneo bunga la Malindi (CDF). Hazina hiyo huwa chini ya serikali ya taifa. Mbunge huyo wa zamani alikuwa pia anakabiliwa na tuhuma nyingine za kunufaika mahala ambapo alifaa kushauri na kuongoza. Vilevile anatuhumiwa kunufaika kwa mali iliyopatikana kwa njia za uhalifu na ulanguzi wa pesa. Licha ya kuondolewa mashtaka, wenzake wanane kwenye kesi hiyo wangali wanakabiliwa kwa kesi mahakamani.
Tarehe 10 Novemba, Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma aliondoa kesi ya ufisadi dhidi ya mwanasiasa mmoja maarufu akiwa ameshtakiwa pamoja na watu wengine tisa. Afisi ya Mashtaka ilidai hapakuwa na ushahidi. Mwanasiasa huyo, Mwaka 2021, alituhumiwa madai ya kupata jumla ya shilingi Bilioni 7.3 (Dola za Amerika 62.8) kutoka kwa serikali kwa njia za udanganyifu. Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma ilidai kwamba tuhuma hizo zilikuwa zimeandaliwa kisiasa chini ya utawala wa serikali iliyopita kwa sababu mwanasiasa huyo alikuwa akiunga mkono kampeni za William Ruto kuwa rais. Mkuu wa Mashtaka ya umma vilevile alikomesha kesi za kuwaondoa nchini Kenya wanasiasa wengine wawili ili wajibu mashtaka nje ya nchi. Wanasiasa hao wawili walifaa kukabili mashtaka ya ufisadi na ulanguzi wa pesa nchini Uingereza. Serikali ilipuuza wito wa Mashirika ya Haki za binadamu na kukabili ufisadi na badala yake kutangaza mipango ya kubadilisha sheria ya Uongozi na maadili ili kuruhusu watu ambao wamepatikana na hatia ya ufisadi na makosa mengine ya uhalifu waendelee kushikilia nyadhifa zao katika afisi ya umma.
Miegemeo ya masuala ya kimapenzi na utambulisho wa kijinsia
Mwezi Februari, Mahakama ya Juu ya Kenya iliunga mkono maamuzi ya Mahakama kuu na Mahakama ya Rufaa iliyoagiza serikali kuisajili taasisi ya Kitaifa kuhusu masuala ya Ushoga na usagaji (National Gay and Lesbian Human Rights Commission (NGLHRC) kwamba liwe shirika la serikali. Mwaka 2013 Shirika la haki za mashoga (NGLHRC) lilikuwa limepinga uamuzi wa bodi ya usimamizi wa mashirika yasiyo ya serikali wa kuwanyima usajili nchini Kenya. Mahakama ilielezea hatua ya serikali ya kukataa kusajili shirika hilo, eti kwa sababu ya miegemeo ya wahusika ya kimapenzi, kuwa inayokiuka kanuni za katiba ya Kenya. Mwezi Septemba, Mahakama ilikataa rufaa iliyowasilishwa dhidi ya uamuzi huo kwenye uamuzi wa awali.
Rais Ruto alikosoa uamuzi wa Mahakama ya juu — uliokuwa umepokewa kwa hisia za kuupinga na malalamiko hapa na pale — akisema Kenya haitakubali mahusiano ya kimapenzi ya watu wa jinsia moja. Wakitumia hisia za umma dhidi ya uamuzi huo ili kujipa umaarufu wa kisiasa wanasiasa watatu walitisha kuwasilisha mswada bungeni wa kutafuta njia za kufanya mahusiano ya watu wa jinsia moja kuwa uhalifu nchini Kenya. Kifungu cha 162 cha Sheria za kutoa vifungo nchini Kenya kinayachukulia mahusiano kama hayo kuwa kosa linalofaa kuadhibiwa. Kifungu hicho kinasema “ushirikiano wa ngono unaokiuka uhalisia wa mwanadamu” utaadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka 14 gerezani, huku kifungu cha 165 kikitoa “shughuli za kimapenzi baina ya wanaume” kuwa zinazofaa kupewa hukumu ya hadi miaka mitano gerezani.
Haki za wanawake na wasichana
Dhuluma na tabia za kuwanyanyasa wanawake katika maeneo ya kazi zingalipo nchini Kenya, huku visa vikiripotiwa kwingi hasa miongoni mwa wanawake wanaohudumu kwenye biashara ndogo ndogo na shughuli za reja reja. Karibu asilimia 83 ya watu wanaofanya kazi nchini Kenya huhudumu kwenye sekta ya reja reja na juakali ambapo asilimia 89 ya wanawake huhudumu kwenye sekta ile. Kifungu cha 6 cha Sheria za kazi kuajiriwa na ajira (2007) kinakataza unyanyasaji wa kimapenzi katika maeneo ya kazini. Hata hivyo, sheria hiyo huwataka waajiri wenye wafanyakazi zaidi ya 20 kuandaa sera za kukomesha unyanyasaji wa kimapenzi kazini. Kenya iliunga mkono uanzishaji wa seria ya Shirika la Kimataifa la Leba inayohusu unyanyasaji na vurugu za kimapenzi (C190) lakini bado haijaidhinishwa kwenye sheria za Kenya. Sheria hiyo inahitaji kanuni kadhaa mwafaka za kukomesha unyanyasaji wa kimapenzi kazini ikiwemo vurugu za kimapenzi.
Mwezi Januari Mwaka 2023, Shirika la Takwimu la Taifa (Kenya National Bureau of Statistics) lilitoa ripoti ya Takwimu za Afya, viwango vya Maisha na hali Mwaka 2022. Ripoti hiyo ilithibitisha kuwepo ukosefu wa usawazishaji kwenye huduma za matibabu kwa akinamama na watoto. Ripoti hiyo ilitoa mfano kwamba, ni asilimia 69 pekee ya wanawake na wasichana kutoka familia za mapato ya chini wanaweza kuwafikia wahudumu wa afya wenye uwezo wakati wa kujifungua ikilinganishwa na asilimia 99 ya wanawake na wasichana kutoka mazingira ya uwezo wa kifedha. Hadi kufikia wakati wa kuandika ripoti hii, serikali bado haikuwa imetoa ripoti nzima.
Mwezi July Mwaka 2023, serikali ilitangaza Mwisho wa kampeni ya matatizo ya utatu (Triple Threat Campaign), iliyolenga kushughulikia mambo matatu yanayotishia afya ya wasichana hasa wenye umri wa kubalehe nchini Kenya: mimba za mapema, maambukizi mapya ya Ukimwi na vurugu za kimapenzi na unyanyasaji wa kijinsia. Hata hivyo, la kusikitisha ni kwamba kampeni hii haijavutia msukumo wowote wa kurekebisha sheria na sera zilizopo, zinazozuia wasichana wa umri wa kubalehe kupata huduma za masuala ya uzazi. Sera kama vile Sera ya Afya ya uzazi (2022-2032) na Sheria ya Watoto 2022 zilifaa kurekebishwa. Kampeni hiyo vilevile bado haijashughulikia marekebisho ya mitalaa ya elimu ya Kenya ili kuhakikisha kwamba inawapa vijana wa umri wa kubalehe mafunzo yafaayo ya uzazi wanayohitaji ili kujilinda kutokana na matatizo yanayoibuka. Na mwisho kampeni hiyo pia bado haijaishinikiza serikali kuhakikisha vijana na mashirika ya kijamii wanashirikishwa ifaavyo kwenye shughuli zinazoendelea za kurekebisha sera za Kenya za vijana na afya ya uzazi.
Mbali na hayo, serikali imeshindwa kuhakikisha kwamba wanawake na wasichana ambao ni waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi wanapata huduma za kutoa mimba zinazoidhinishwa kisheria kuendana na kanuni za katiba ya sasa. Kutokana na hali hii, waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi ambao hupata mimba bado hulazimika kutafuta njia zisizo salama za uavyaji.
Haki za wakimbizi
Katikati ya Mwaka 2023, serikali ya Kenya ilitangaza kuanzisha mpango wa miaka mingi wa “Shirika Plan” ili kuanzisha juhudi za kuwajumuisha wakimbizi kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi nchini Kenya. Mpango huo utabadilisha kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma kuwa makao rasmi nchini huku wakimbizi wakishirikiana na raia wa Kenya katika ujenzi wa uchumi katika maeneo wanayoishi. Wakimbizi hao, kwa mujibu wa mpango huo, wataruhusiwa kunufaika kwa huduma za serikali. Mpango huu ni tofauti na sera ya awali ya Kenya— ambayo ililenga zaidi kuwaweka wakimbizi kwenye kambi na kuwarejesha makwao baadaye. Palikuwa na vitisho vya mara kwa mara vya kufunga kambi hizo — lakini mpango wa sasa ni hatua mbele kwenye suala zima la haki za wakimbizi nchini Kenya. Kenya ina wakimbizi 636,000 kufikia Mwezi Julai Mwaka 2023.
Wahusika muhimu wa Kimataifa
Kenya imesalia kuwa mhusika mkuu wa kimikakati ambapo inaibuka kuwa ngome ya ukanda huu kwa jamii ya kimataifa kuhusiana na maswala mengi ya kimataifa. Kenya inachangia vikosi vya usalama kwenye kampeni za amani nchini Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Serikali ya Kenya ni mhusika mkuu kwenye mashauriano ya kutafuta amani na ukomeshaji wa mapigano kwenye mizozo ambayo imekuwa ikiendelea nchini Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ingawa mojawapo ya makundi yanayozozana yalimkataa Rais William Ruto kuongoza mashauri ya kutafuta amani ya Sudan kufuatia madai ya kuunga mkono upande mmoja kwenye mzozo, Ruto ameendelea kushinikiza kufanyika mazungumzo ya amani chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Maendeleo baina ya nchi (IGAD), ambayo yanatafuta amani Sudan kwa niaba ya Umoja wa Afrika.
Wahusika kadhaa wakuu wameshiriki kwenye juhudi za kukomesha tofauti za kisiasa baina ya rais Ruto na Odinga, ambaye ameongoza maandamano kadhaa ya kupinga serikali ya Ruto. Rais wa Tanzania Samia Suluhu na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa walianzisha mpango wa mazungumzo. Maandamano mwishowe yalikoma ambapo sasa mazungumzo yanaendelea kati ya upande wa serikali na upinzani – mazungumzo hayo yalianza baada ya aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo kufanya mikutano na Ruto na Odinga jijini Nairobi.
Mwezi Juni, Tume ya Umoja wa Ulaya na Kenya walimaliza majadiliano kuhusu uwezekano wa Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi ambao unashirikisha kujitolea kwa pande hizo mbili kusetiri masuala ya mazingira, haki za kazi na leba na haki za wanawake.