Tangu kuchaguliwa kwa Rais John Magufuli Desemba 2015, Tanzania imeshuhudia kuporomoka kwa wazi katika masuala ya uhuru wa kujieleza, kujumuika na kukusanyika. Kauli za uvunjifu wa haki zinazotolewa na viongozi zimeendelea kuambatana na kutekelezwa kwa sheria kandamizi na kunyanyaswa na kukamatwa kwa waandishi wa habari, wanasiasa wa upinzani na wakosoaji wa serikali. Kujikosoa na hofu ya kuadhibiwa kumezuia ukosoaji wa serikali. Wanawake na wasichana, hasa wanafunzi wenye watoto wanaotaka kuendelea na masomo, wameendelea kukumbana na sera za kibaguzi. 

Uhuru wa Kujieleza

Mwezi Machi, Tanzania ilipitisha kanuni za maudhui ya kimtandao ikiwa ni sehemu ya Sheria ya Mawasiliano ya Posta na Kielektroniki, ambazo zimeipa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (MUMT/TCRA) mamlaka mapana ya kutoa leseni kwa maudhui ya kimtandao, ikiwa ni pamoja na blogu, ambazo hivi sasa zinatakiwa kulipa ada ya hadi Dola 900 ($900), kitu ambacho ni kikwazo kwa wengi. Kutokutii ni kosa la jinai. 

Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015 imeendelea kuminya uhuru wa watu kujieleza na haki ya faragha. Mwezi Machi, mwanafunzi Abdul Nondo alishtakiwa kwa kuchapisha taarifa ya uongo baada ya kutuma ujumbe wa whatsapp kwa wanafamilia na marafiki kwamba ametekwa. Nondo alisema watekaji wake walimshutumu kwa kutumiwa na wabunge wa upinzani na wanaharakati kuandaa maandamano ya wanafunzi. Aliachiwa kwa dhamana, na hadi wakati wa uandishi wa ripoti hii, kesi yake ilikuwa bado inaendelea. Wakati wa nyuma, Nondo alikuwa mkosoaji wa vitendo vya askari polisi hasa wakati wa maandamano ya Februari ambapo mwanafunzi aliuwawa. Polisi walikanusha kwamba alitekwa. Novemba 5, Nondo aliachiwa huru na mahakama. 

Mwishoni mwa mwaka, Bob Chacha Wangwe alikuwa amekata rufaa kuhusiana na hukumu yake ya mwaka 2017 juu ya kuchapisha taarifa za uongo chini ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao ambapo katika ukurasa wake wa Facebook aliukosoa mwenendo wa uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika mwaka 2015. Mahakama jijini Dar es Salaam ilimuhukumu kifungo cha mwaka 1.5, au kulipa faini ya Shilingi milioni 5 za Kitanzania (US$2,185). 

Mwezi Juni, mahakama iliwaachia huru Maxence Melo na Micke William, waanzilishi wa mtandao maarufu wa kufichua taarifa nyeti Jamii Forums, ambapo walishtakiwa kwa kosa la kukaidi amri ya polisi iliyowataka kuwapatia majina halisi ya watumiaji wa mtandao wao kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Kimtandao. Mashtaka mawili, ya kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa Tanzania chini ya kanuni za Maudhui ya Kimtandao na kwa kukwamisha upelelezi chini ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao, zilikuwa bado zinaendelea hadi wakati wa uandishi wa ripoti hii.

Mwezi Januari, TCRA ilivitoza faini vituo vitano vya luninga kiasi cha shilingi milioni 60 za Kitanzania ($27,000) kwa kurusha matangazo yaliyohusu mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, ambapo kituo hicho kilishutumu maafisa wa usalama wa serikali kuwanyanyasa wakati wa uchaguzi mdogo Novemba 2017. Mamlaka ya Mawasiliano ilidai kwamba maudhui yalikuwa ya “kichochezi” na kinyume na Sheria ya Utangazaji. 

Mwezi Agosti 8, polisi walimkamata Sitta Tumma, mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima baada ya kuripoti polisi kutawanya mkutano wa chama cha upinzani Tarime. Aliwekwa kizuizini kwa usiku mmoja lakini hakushtakiwa. Katika tukio tofauti siku hiyo hiyo jijini Dar es Salaam, polisi wa kutuliza ghasia walimpiga Silas Mbise, mwandishi wa habari wa michezo, tukio lililorekodiwa katika video, huku akionekana amelala chini akiwa ameinua mikono hewani. 

Mwezi Septemba, bunge lilipitisha marekebisho ya sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 na kufanya kuchapisha takwimu zozote pasipo ruhusa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (OTT/NBS) kuwa kosa la jinai na kuzuia usambazwaji wa takwimu zinazolenga “kukanusha, kupotosha au kukosoa” takwimu za OTT/NBS. Utekelezwaji wa sheria hii unaweza kuzuia uchapishwaji wa halali wa tafiti binafsi kutoka idara mbalimbali. 

Wanachama wa vyama vya upinzani wamekumbatana na kukamatwa kwa mara kwa mara na mashtaka ya jinai kwa kuikosoa serikali. Joseph Mbilinyi, mbunge wa Mbeya, na Emmanuel Masonga, ofisa wa chama, walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela mwezi Februari kwa “kumtukana” Magufuli wakati wa mkutano wa kisiasa wa hadhara. 

Tarehe 21 Juni, Mahakama ya Afrika Mashariki iliiamuru Tanzania kulifungulia gazeti la wiki, Mseto, ambalo mnamo mwaka 2016 aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Nape Nnauye, alitoa amri ya kufungiwa kwa gazeti hilo baada ya kuwa limeripoti tuhuma za rushwa katika kampeni za urais za Magufuli. 

Uhuru wa Kukusanyika

Tarehe 9 Machi, Magufuli aliapa kupambana na maandamano yoyote ambayo serikali itayaona kuwa si halali. Kabla ya maandamano ya kitaifa ya tarehe 26 April yaliyoitishwa na mwanaharakati Mtanzania aishie Marekani Mange Kimambi, Kamanda wa Polisi Dodoma Gilles Muroto aliwaambia waandishi wa habari kwamba waandamanaji “watapata tabu sana” na kwamba “watapigwa kipigo cha mbwa koko.” Maandamano hayakufanyika. 

Maandamano ya kisiasa yalisababisha kukamatwa kwa wanachama wengi wa upinzani. Mwezi Machi, polisi iliwakamata na kuwashtaki wabunge wa CHADEMA Freeman Mbowe, Vincent Mashinji, John Mnyika, Peter Msigwa, Esther Matiko, Salum Mwalimu, na baadae Halima Mdee, kwa kushiriki katika maandamano yasiyo halali jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe alishtakiwa kwa “kueneza chuki na uvunjifu wa amani na uasi” inaripotiwa kwa kusema wakati wa mkutano huo kwamba Magufuli hata dumu kama rais kwa muda mrefu. 

Kupotea na Kushambuliwa Kisiasa

Ndani ya wiki mbili, watu wasiojulikana waliwauwa kikatili maofisa wa CHADEMA, katika mashambulio yalioonekana kuwa ya kisiasa. Februari 13, mwili wa Daniel John, afisa wa kata ya Hananasif Kinondoni jijini Dar es Salaam, ulikutwa ufukweni huku ukiwa na majeraha ya kukatwa na panga kichwani. Tarehe 23 Februari, Godfrey Luena, diwani wa kata ya Nemawala ya Morogoro, alikutwa amekufa nje ya nyumba yake. Luena alikuwa afisa wa haki za binadamu pia akifuatilia kesi za dhuluma ya ardhi. Wakati polisi wanasema uchunguzi unaendelea, hakuna aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo. 

Mwezi Juni, polisi walisema hapatakuwa na uchunguzi zaidi kuhusiana na kuuwawa kwa Akwilina Akwilini, mwenye umri wa miaka 21, aliyepigwa risasi akiwa ndani ya basi mwezi Februari wakati polisi wakitawanya maandamano ya CHADEMA. 

Polisi hawajakamata mtu yeyote yule kuhusiana na matukio mawili ya mauaji ya mwaka 2017 ambayo yalizuia ukosoaji mkubwa. Mnamo Septemba 2017 watu wasiojulikana walimmiminia risasi mbunge wa upinzani Tundu Lissu, mkosoaji maarufu wa serikali ya Magufuli, nje ya nyumbani kwake makao makuu ya nchi Dodoma. Mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Azory Gwanda amepotea, na inahofiwa kuwa amefariki dunia, tangu Novemba 2017. Inaripotiwa kwamba Gwanda alikuwa akifanyia kazi habari ya mfululizo wa mauaji Kibiti, kusini mwa Dar es Salaam. 

Wakimbizi

Januari 23, serikali ilitangaza kujiondoa kutoka mpango wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia wakimbizi ambao unatoa suluhisho la kudumu kwa wakimbizi ikiwa ni pamoja na kuwapa uraia (ujulikanao kwa Kiingereza kama Comprehensive Refugee Response Framework(CRRF)) kwasababu za “kiusalama na kukosa pesa”, na kusimamisha zoezi endelevu la kuwajumuisha wakimbizi katika jamii za wenyeji. Serikali ilisema pia kwamba haitatoa kipaumbele kwa maombi mapya ya kuomba hifadhi nchini. Kati ya Septemba 2017 na mwisho wa mwezi Julai 2018, mamlaka nchini Tanzania na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) waliwezesha kurudishwa kwa Warundi 40,000 tu nchini kwao, huku lengo la mwezi Machi likiwa kurudisha wakimbizi 2000 kwa wiki. Hata hivyo, tangu mwishoni mwa mwaka 2017, UNHCR ilieleza wasiwasi wake juu ya sababu mbalimbali zinazofanya maisha ya wakimbizi kuwa magumu na mwezi Agosti ikaisukuma serikali ya Tanzania kuhakikisha kwamba wakimbizi hawashurutishwi kurudi nyumbani kwao. 

Haki za Watoto

Wasichana nchini Tanzania bado wanakumbana na unyanyasaji katika elimu kufuatia katazo la Magufuli la mwaka 2017 kwa wanafunzi wajawazito shuleni na wale waliojifungua. Maofisa wengi wa shule za sekondari huendesha vipimo vya mimba vya lazima kama mojawapo ya hatua za kinidhamu kuwafukuza wanafunzi wajawazito shuleni. 

Adhabu za viboko bado ni tatizo kubwa katika shule za Tanzania. Mwezi Agosti, kijana wa miaka 13 alifariki dunia baada ya kuchapwa vikali na mwalimu wake. 

Haki za Wanawake

Mwezi Septemba, serikali ilitangaza kuondoa jumbe za elimu za uzazi wa mpango zinazofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID). Magufuli amedai kwamba wanawake wanapaswa kuachana na njia za uzazi wa mpango, na kwamba elimu juu ya uzazi wa mpango si ya lazima, na kwamba watu wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii tu kuzitunza familia zao. 

Maelfu ya wanawake wa Kitanzania wanaofanya kazi za ndani Mashariki ya Kati wanakumbana na ukiukwaji wa haki za ajira wa hali ya juu na unyanyasaji wa aina nyingine. Tanzania haina muongozo wowote wa kisheria  kuwalinda wafanyakazi hawa wahamiaji dhidi ya kuajiriwa katika aina za ajira za unyanyasaji nje ya nchi, kitu ambacho kinasaidia kunyanyaswa kwa wafanyakazi hawa. 

Utambulisho wa Kijinsia na Mwelekeo wa Kingono

Sheria ya Tanzania inaamuru adhabu ya hadi kifungo cha maisha jela kwa kosa la kufanya ngono ya hiari ya watu wa jinsia moja. Msako wa Wanawake wanaofanya mapenzi na wanawake, wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, wanaovutiwa kimapenzi na jinsia zote mbili na watu wenye jinsia tofauti na asili (LGBT) ulianzishwa na serikali ya Magufuli mnamo Julai 2016 umeendelea kwa kasi. Tarehe 31 Oktoba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alitangaza mpango wa kuwakamata washukiwa wote wa mapenzi ya jinsia moja na kuwafanyia uchunguzi wa lazima wa njia ya haja kubwa na kuwapatia ushauri wa kubadilika. Siku nne baadae, Wizara ya Mambo ya Nje ilitoa taarifa ikisema kwamba Makonda alikuwa akiwasilisha “maoni yake binafsi na si msimamo wa serikali” na kuahidi “kuendelea kulinda,  na kuheshimu” haki za binadamu zinazotambulika kimataifa. 

Washirika wa Kimataifa

Tanzania inaendelea kuwa sehemu ya muhimu katika jitihada za Umoja wa Mataifa za ulinzi wa Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ni mwenyeji wa mahakama za Afrika Mashariki na ile ya Haki za Binadamu na Watu ya Afrika zilizopo jijini Arusha. 

Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Uingereza na Uholanzi, washirika wa kimatafa wa Tanzania, wameendelea kukaa kimya katika kuikosoa serikali dhidi ya mwendelezo wa uminywaji wa uhuru wa kujieleza na kukusanyika na utekelezwaji wa sheria kandamizi. 

Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam ulieleza wasiwasi wake kuhusiana na mashumbulio ya kisiasa, mapungufu katika chaguzi ndogo, na “kuporomoka kwa haki za kiraia na binadamu,” kufuatia kukamatwa na kunyanyaswa kwa wanawake wanaofanya mapenzi na wanawake, wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, wanaovutiwa kimapenzi na jinsia zote mbili na watu wenye jinsia tofauti na asili. 

Mwezi Oktoba, Benki ya Dunia iliikosoa serikali juu ya marekebisho ya sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 kwa kuwa kinyume na viwango vya kimataifa. 

Mwezi Novemba, Denmark ilitangaza kwamba ingesitisha msaada wa Dola milioni 10 kwa Tanzania kwasababu ya “kauli za kinyanyasaji zisizokubalika dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja” zilizotolewa na afisa wa serikali, anaeaminika kuwa ni Makonda.