(Dar Es Salaam) – Watoto wenye umri mdogo wa hadi miaka minane wanafanya kazi katika migodi midogo midogo ya dhahabu ya Tanzania, ikiwa na hatari kubwa kwa afya zao na hata maisha yao, shirika la Human Rights Watch imesema katika ripoti iliyotolewa leo. Serikali ya Tanzania inapaswa kukomesha ajira kwa watoto katika uchimbaji mdogo mdogo wa dhahabu, ikiwa ni pamoja na katika migodi isiyo rasmi, na isiyo na leseni, na Benki ya Dunia na nchi wahisani wanapaswa kuunga mkono juhudi hizi.
Ripoti yenye kurasa 96, “Kazi ya Sulubu yenye Sumu: Ajira kwa Watoto na Kujiweka Wazi kwa Zebaki katika Migodi Midogo Midogo ya Dhahabu ya Tanzania,” inaelezea jinsi gani maelfu ya watoto wanafanya kazi katika migodi midogo midogo ya dhahabu yenye leseni na isiyo na leseni Tanzania, nchi ya nne kwa ukubwa kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika. Wanachimba na kupekesha mashimo marefu , yasiyo imara, wakifanya kazi chini ya ardhi kwa kupeana zamu kwa hadi masaa 24, na kusafirisha na kutwanga mifuko mizito ya mawe ya dhahabu. Watoto hawa wanakuwa katika hatari ya kujeruhiwa kwa mashimo kuporomoka na ajari zinazoweza kutokana na vifaa wanavyotumia, vile vile matatizo ya kiafya ya muda mrefu kutokana na kujiweka wazi kwa zebaki, kuvuta vumbi, na kubeba mizigo mizito. Kijana mdogo wa miaka 17 aliyenusurika katika ajali ya shimo aliiambia shirika la Human Rights Watch, “Nilidhani nimekufa, niliogopa sana.”
“Vijana wadogo wakike na wakiume wa Kitanzania wanashawishika kujiingiza katika uchimbaji wa dhahabu wakitumaini kupata maisha bora, lakini baadae wanajikuta wamekwama katika mzunguko mbaya wa hatari na kukata tamaa,” alisema Janine Morna, mtafiti wa haki za watoto wa shirika la Human Rights Watch “Tanzania na wahisani wanahitaji kuwatoa watoto hawa katika migodi na kuwaingiza shuleni ao katika mafunzo ya ufundi stadi.”
Watoto wengi wanaofanya kazi za uchimbaji ni yatima au wale wanaoishi katika mazingira hatarishi ambao hawana mahitaji ya msingi na msaada. Shirika la Human Rights Watch iligundua pia kwamba wasichana wadogo wanaoishi katika migodi au maeneo yanayoizunguka migodi wanakabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na vishawishi vya kujiingiza katika biashara ya ngono. Baadhi ya wasichana wanakuwa wahanga wa utumikishwaji wa biashara ya ngono na hivyo kuwa hatarini kuambukizwa virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa.
Shirika la Human Rights Watch ilitembelea migodi 11 katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Mbeya, na kufanya mahojiano na watu zaidi ya 200, ikiwa ni pamoja na watoto 61 wanaofanya kazi katika machimbo madogo madogo ya dhahabu. Ajira kwa watoto katika kazi za hatari za uchimbaji ni moja kati ya namna mbaya kabisa za ajira kwa watoto chini ya makubaliano ya kimataifa, ambayo Tanzania ni mwanachama ya makubaliano hayo.
“Katika makaratasi, Tanzania ina sheria madhubuti sana zinazokataza ajira kwa watoto katika uchambaji madini, lakini serikali imefanya kidogo sana katika kutekeleza sheria hizo,” alisema Morna. “Wakaguzi wa kazi wanahitaji kutembelea mara kwa mara migodi yote, ile yenye leseni na isiyo na leseni, na kuhakikisha kwamba waajiri wanapata vikwazo kwa kutumia ajira kwa watoto.”
Watumishi watoto, pamoja na wale wanaoishi maeneo ya karibu na migodi, wapo katika athari ya kudhurika na zebaki. Zebaki hushambulia mfumo mkuu wa fahamu na inaweza kusababisha ulemavu wa maisha kwa watoto, ambao miili yao inayoendelea kukua inaathirika kirahisi zaidi kwa metali nzito. Wachimbaji, pamoja na watoto, wanachanganya zebaki pamoja na mawe ya dhahabu zilizopondwa na kuichoma aloi ya zebaki (gold-mercury amalgam) ili kuiachia dhahabu, wakijiweka wazi kabisa na harufu kali ya moshi wa sumu wa zebaki. Hata watoto wadogo kabisa ambao hawafanyi kazi huwa wanakuwepo wakati wa zoezi hili, ambalo nyakati zingine hufanywa nyumbani.
Watu wazima wengi na wachimbaji watoto hawafahamu hatari hizi za kiafya. Wahudumu wa afya hawana mafunzo na hawana vifaa vya kutibia na wanakosa zana za uchunguzi au kutibu sumu ya zebaki. Sheria na harakati zilizopo juu ya zebaki zimeshindwa kwa kiasi kikubwa sana kupunguza matumizi ya zebaki.
Tanzania imesaidia utengenezaji wa mkataba wa kimataifa wa kupunguza kujiweka wazi kwa zebaki duniani kote, ambao zaidi ya serikali 140 walikubaliana nao mnamo tarehe 1 Januari 2013. Mapatano ya Minamata juu ya Zebaki (The Minamata Convention on Mercury), yaliyopewa jina la eneo la Japan lililokumbwa na janga la sumu ya zebaki takriban nusu karne iliyopita, makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa maazimio Oktoba eneo la karibu na Minamata.
“Tanzania imesaidia kupatikana kwa Mapatano ya Minamata juu ya Zebaki,” alisema Morna. “Na sasa ili kulinda azma ya watu wake na ukuwaji wa sekta yake ya uchimbaji, inahitaji kuwa mstari wa mbele kulinda watoto wake – kwa kuwalinda, kuwapima na kuwatibu watoto hao kwa kujiweka wazi na zebaki na kuwaondoa katika migodi.”
Kufanya kazi katika migodi kunaivuruga elimu ya watoto. Watoto wanaofanya kazi machimboni nyakati zingine hawahudhurii darasani au wanaacha shule kabisa. Waalimu waliwaambia Shirika la Human Rights Watch kuwa mahudhurio ya shuleni na ufaulu wa darasani vilishuka mara tu mgodi uliopofunguliwa eneo la jirani. Lakini zaidi pia, vijana wengine wanajitafutia ajira za kudumu, ikiwa ni pamoja na machimboni, kwasababu wamekosa fursa za kujiunga na shule za sekondari au mafunzo ya ufundi stadi.
Kijana mwenye umri wa miaka15,wilaya ya Geita alivyoelezea kwa ufupi madhara ya uchimbaji madini katika maisha yake: “Ni vigumu kuchanganya uchimbaji na shule. Sipati muda wa kwenda mafundishoni (ambayo hufanyika mwishoni mwa wiki). Nawaza machimbo tu, yananichanganya….siku moja….niliugua (kwa ajili ya machimbo na kutohudhuria darasani). Nilihisi maumivu mwili mzima.”
Serikali ya Tanzania inapaswa kupanua zaidi upatikanaji wa elimu ya sekondari na mafunzo ya ufundi stadi na kuboresha ulinzi wa watoto, aseme shirika la Human Rights Watch . Serikali na wahisani wanapaswa kutoa msaada wa kifedha na kisiasa kwa mkakati mpya juu ya watoto walio katika mazingira hatarishi na kuwajumuisha yatima waishio maeneo ya migodini katika mpango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Tanzania wa ruzuku na utoaji wa pesa kwa watu waishio katika mazingira hatarishi.
Benki ya Dunia na wahisani wengine katika sekta ya madini wanapaswa pia kuunga mkono hatua za ukomeshwaji wa ajira kwa watoto migodini na kupunguza kujiweka wazi kwa zebaki kwa watoto na watu wazima, aseme shirika la Human Rights Watch . Kwa mfano, wanapaswa kuwasaidia watoto kuhama kutoka kazini katika migodi isiyo na leseni na kuingia shuleni, na kuhakikisha kwamba migodi mipya inayopewa leseni haitumii ajira kwa watoto. Mradi wa sasa wa dola milioni 55 wa Benki ya Dunia kusaidia sekta ya madini hautatui tatizo la ajira kwa watoto moja kwa moja.
Sekta ya madini ina wajibu wa kuhakikisha hainufaiki kwa namna yoyote ile kutokana na ajira kwa watoto iliyokinyume na sheria, aseme shirika la Human Rights Watch . Wakati huo huo wauzaji wa dhahabu waliohojiwa na shirika la Human Rights Watch nchini Tanzania hawakuwa na utaratibu wowote ule wa kuzuia mzunguko wa upatikani wa dhahabu iliyochimbwa na watoto.
Wauzaji wadogo wadogo mara zote hununua dhahabu moja kwa moja kutoka machimboni na katika miji iliyo na machimbo halafu huiuza kwa wauzaji wakubwa Tanzania. Nyakati zingine dhahabu hii hupita kwa washenga wengi kabla haijawafikia wauzaji wakubwa wanaouza dhahabu nje ya nchi. Kwa mujibu wa serikali ya Tanzania, wachimbaji wadogo wadogo walitengeneza takribani tani 1.6 za dhahabu mnamo mwaka 2012 – iliyokuwa na thamani ya karibu dola milioni 85.
Maeneo makubwa ambayo dhahabu ya wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzania huelekea mara nyingi ni pamoja na nchi za Muungano wa Falme ya Kiarabu (UAE). Dhahabu pia husafirishwa kwenda Uswisi , Afrika Kusini, China na Uingereza.
“Iwe kwa kiwango kikubwa au kidogo, nchini Tanzania ao dunia nzima, biashara ni lazima iache matumizi haramu ya ajira kwa watoto katika upatikanaji wa dhahabu yao,” amesema Morna. “Kwa wale wenye nguvu ya ununuzi, wanaushawishi mkubwa kwa wauzaji wa dhahabu. Wanapaswa kuitumia kuwalinda watoto na kuwalinda watumiaji kununua dhahabu itokanayo na ajira kwa watoto.”