Skip to main content

Tanzania

Matukio ya 2022

Mwanaume wa Kimaasai akiwa na mifugo yake (haionekani pichani) ikinywa maji katika kijiji cha Msomera huko Handeni, Tanzania mnamo Julai 15 2022. Mnamo Juni 2022, Tanzania ilianza kuwahamisha jamii ya wafugaji wa Kimaasai kutoka katika eneo maarufu la hifadhi ya Ngorongoro kwenda Handeni, wilaya iliyopo kilomita 600 (maili 370) kusini, kitendo ambacho wanaharakati wa haki wamekielezea kama uhamishwaji uliokiuka sheria.

© 2022 Photo ya AFP

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeondoa marufuku zilizowekwa kwenye magazeti, ikasitisha katazo la muongo mmoja la kuzuia wanafunzi wajawazito na kina mama vijana kuhudhuria shule na kuwaachia wanasiasa wa upinzani waliokuwa kizuizini. Hata hivyo, Serikali imeendelea kuwakamata wafuasi wa vyama vya upinzani. Mamlaka bado hazijaweza kufanya uchunguzi wowote wa maana kufuatia unyanyasaji mkubwa ulioghubika uchaguzi wa 2020 na bado hazijafanya marekebisho ya sheria lukuki zinazozuia haki ya uhuru wa kujieleza. Serikali imewahamisha kwa nguvu jamii za wafugaji za Wamasai licha ya mapingamizi kutoka kwa wanajamii, vikundi na jamii ya kimataifa.

Uhuru wa Kujieleza na Vyombo vya Habari

Pamoja na hatua nzuri zilizochukuliwa kwa kuondoa marufuku zilizowekwa kwa baadhi ya magazeti, vyombo vya habari vimeendelea kukabiliana na vikwazo vikali.

Mnamo Februari 10, Waziri wa habari aliondoa marufuku iliyoweka kwa magazeti ya Mseto, Mawio, Mwanahalisi na Tanzania Daima ambayo yalifungiwa kufuatia kuchapisha makala zilizomkosoa Hayati Rais John Magufuli. Tangu mwaka 2015 mamlaka zimekuwa zikisitisha leseni za magazeti kutokana na kuchapisha maudhui yanayokosoa serikali, mara nyingi wakirejea Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya 2016.

Mnamo Julai Mosi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilisimamisha chombo cha habari cha mtandaoni DarMpya kwa kushindwa kuhuisha leseni yake, hii ni baada ya chombo hiki kuchapisha habari ya maandamano ya Juni 17 Dar es Salaam dhidi ya tuhuma za kuingiliwa na Kenya wakati serikali ilipokuwa inawahamisha jamii za wafugaji wa Kimaasai kaskazini mwa Tanzania. Vyombo vya habari viliripoti kuwa DarMpya ilibadilisha jina na kuitwa ZamaMpya mwezi Agosti baada ya TCRA kukataa kuidhinisha maombi yake ya kuhuisha leseni.

Bado haijulikani mahali alipo mwandishi wa habari za uchunguzi Azory Gwanda ambaye alichukuliwa nyumbani kwake Kibiti na watu wasiojulikana mnamo Novemba 2017 wakati akifanya uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Mamlaka bado hazijafanya uchunguzi wa maana kufuatia kupotea kwake licha ya kuwepo kwa shinikizo kutoka kwa wanaharakati wa ndani na vyombo vya habari.

Wapinzani wa Serikali

Mnamo Machi 4, mamlaka zilimwachia Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha siasa cha Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani Tanzania baada ya kuwa mahabusu kwa zaidi ya miezi saba kwa tuhuma za ugaidi. Polisi walimkamata Mbowe na wanachama wengine 11 mnamo Julai 2022 Mwanza walipokuwa wamepanga kufanya mkutano kujadili mabadiliko ya katiba ambayo chama hicho kinasema inampa madaraka makubwa raisi.

Mnamo Mei 25, polisi mkoani Manyara waliwakamata na kuwaweka kizuizini kwa muda wanachama 20 wa baraza la vijana Chadema waliokuwa katika kikao kuhusu mabadiliko ya katiba. Katika taarifa waliyotoa, Chadema waliwashutumu polisi kuwa waliwapiga baadhi ya viongozi wa baraza la vijana wakiwa kizuizini.

Haki za Watoto

Mnamo Machi 8, serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia walichapisha makubaliano yao ya kurekebisha Mpango wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari Tanzania ambao uliahidi hatua mpya ya kuondoa marufuku ya kwenda shule dhidi ya wanafunzi ambao ni wajawazito au ni kina mama na kuwahakikishia haki yao ya kupata elimu. Serikali iliweka ahadi ya kuondoa “vipimo vya mimba visivyo vya hiari ,” utaratibu ambao umekuwa ukitekelezwa kwa lazima katika shule nyingi za sekondari na kutumika kufukuza wanafunzi wajawazito. Mageuzi haya bado hayakuwa yametekelezwa wakati wa uandishi wa taarifa hii.

Sheria ya Elimu bado inaruhusu wanafunzi kufukuzwa ikiwa wameolewa au wakitenda “kosa linaloenda kinyume na maadili,” ambayo imekuwa ikitumika huko nyuma kufukuza wanafunzi ambao ni wajawazito, walioolewa au ambao ni kina mama.

Mnamo Septemba 15, Kamati ya Wataalam wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto waligundua kwamba Tanzania inakiuka haki ya wasichana wajawazito na kina mama vijana kupata elimu, afya, faragha na maslahi yao kwa ujumla kupitia vipimo vya mimba vya lazima shuleni na kuwafukuza wasichana wajawazito na walioolewa.

Serikali pia bado haijaharamisha ndoa za utotoni licha ya uamuzi wa  2016 wa Mahakama Kuu wa kurekebisha Sheria ya Ndoa kwa kuongeza umri wa kisheria wa kuoa au kuolewa kuwa miaka 18 kwa wasichana na wavulana.

Haki za Ardhi

Kufuatia migogoro ya muda mrefu ya ardhi kaskazini mwa mkoa wa Arusha, katikati ya 2022 serikali iliendelea na mpango wake usio wa hiari na kuwaondoa kwa lazima jamii ya wafugaji ya Wamasai kutoka katika maeneo ya mbuga yaliyotengwa huko Ngorongoro licha ya mapingamizi kutoka kwa wanajamii, ukosoaji mkubwa kutoka jumuiya za kimataifa na amri ya mahakama yam waka 2018 iliyopinga kuondolewa kwa Wamaasai. Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa walionya kwamba vitendo vya serikali ni sawa na kuwaondoa kwa lazima na kuwahamisha watu bila ridhaa jambo ambalo linakatazwa na sheria za kimataifa.

Mamlaka nchini Tanzania zilitishia kukamata na “kuwawajibisha” watu ambao walikuwa wanapinga zoezi la kuhamishwa. Mamlaka pia zilitangaza mpango wa siku 10 wa opereshani maalumu kuondoa “wahamiaji haramu” wote kufuatia tuhuma kuwa wafugaji kutoka Kenya wamevuka mipaka kinyume cha sheria kuhodhi maeneo. Wamaasai wanapatikana Kenya na Tanzania.

Mamlaka zilitishia na kukamata watu kwa kutoa maoni juu ya zoezi la uhamishwaji na tarehe 10 Juni vyombo vya ulinzi vilipiga mabomu ya machozi wanajamii waliokuwa wanapinga. Polisi waliwakamata na baadae kuwafungulia mashitaka wanajamii 23 kwa tuhuma za kumuua askari polisi Garlius Mwita tarehe 10 Juni.

Mwelekeo wa Kijinsia na Utambulisho wa Jinsia

Mamlaka zimeendelea kutumia Sheria ya Masharti Maalumu ya Makosa ya Kujamiiana ya 1998 kutoa adhabu ya hadi kifungo cha maisha kwa watu wazima wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja kwa maridhiano, huku mamlaka zikiendelea kuweka vikwazo kwa mashirika yanayohamasisha haki na afya za wasagaji, mashoga, wenye jinsia mbili na waliobadili jinsia (LGBT).

Septemba 11, Waziri wa Habari, Nape Nnauye alisema kwamba watu watakaopatikana wakisambaza maudhui yanayohusu mapenzi ya jinsia moja mtandaoni watakumbana na “adhabu kali.” Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) ya 2020 inakataza “kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja,” ambayo yanajumuisha uchechemuzi wa haki za LGBT. Wanaokiuka kanuni hizi wanaweza kupigwa faini au kuhukumia kifungo kuanzia mwaka mmoja hadi mitano gerezani.