Kukosekana kwa uwajibikaji kwa maofisa usalama kutokana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikatili na kuwafukuza watu kutoka katika makazi yao, bado ni suala kubwa sana nchini Kenya, pamoja na ahadi ya Rais Uhuru Kenyatta kushughulikia masuala haya muhimu, ikiwa ni pamoja na yale ya nyuma ambayo yaliwahi kuchafua uwezo wa Kenya kufanya uchaguzi kwa Amani. Mamlaka za Kenya zilishindwa kuchunguza vya kutosha unyanyasaji wa maofisa wa usalama, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikatili na kusababisha watu kukimbia makazi yao, na kuwawajibisha wanaohusika.
Japo maofisa wakuu wa serikali, ikiwa ni pamoja na Rais Kenyatta, waliahidi hadharani kuheshimu uhuru wa kujieleza na wa habari, mazingira ya kazi kwa bloga, waandishi wa habari na wanaharakati bado yamebaki kuwa ni ya hatari ikiwa ni pamoja na askari polisi kuwatisha waandishi wa habari na wanabloga, na kuwakamata na kuwaweka kizuizini waandishi wa habari na wanaharakati.
Mjini Lamu, maofisa wa usalama wa Kenya waliwanyanyasa na kuwaweka kizuizini wanaharakati waliokuwa wakielezea masuala ya uminywaji wa haki yaliyokuwa yakihusiana na miradi mikubwa ya maendeleo ya miundombinu, wakiwashutumu wengine kuwa ni magaidi. Mamlaka za Kenya pia zimeendelea kufanya unyanyasaji wakiwaondoa watu jamii ya Kimasai kutoka msitu wa Mau.
Mwezi Januari, wanamgambo wenye silaha walivamia DusitD2, hoteli iliyopo magharibi mwa Nairobi, wakiua si chini ya watu 24. Al Shabab, kikundi cha wanamgambo wa Kiisalmu chenye makazi yake nchi ya jirani ya Somalia, kilikiri kuhusika na shambulio hilo.
Ukosefu wa Uwajibikaji katika Makosa Makubwa
Pamoja na uwekwaji wa kumbukumbu na uchunguzi wa vurugu zilizotokea katika uchaguzi wa mwaka 2017/2018, ambapo watu zaidi ya 100 waliuwawa, serikali bado haijamshitaki ofisa usalama yeyote aliyehusika na mauwaji hayo. Uchunguzi wa serikali katika mauaji ya mtoto wa miezi tisa Samantha Pendo wa Kisumu na mtoto wa miaka tisa Stephanie Moraa wa Nairobi uligundua kwamba si chini ya makamanda watano wa polisi wa ngazi ya juu walihusika na ukatili, lakini mamlaka bado hazijamshikilia yeyote yule kwa mauaji hayo na unyanyasaji mwingine katika kipindi cha uchaguzi.
Pamekuwa hakuna maendeleo yoyote yale katika upepelezi au kushikiliwa kwa yeyote yule juu ya vurugu zilizotokea katika uchaguzi wa mwaka 2007/2008 ambapo takribani watu 1,100 waliuwawa.
Mwaka 2015, Rais Kenyatta alitangaza mipango ya kuanzisha mfuko wa msaada wa Ksh10 billion (takribani dola milioni $100) kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki, ikiwa ni pamoja na wale wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008, lakini hakuanzisha mfuko huo hadi mwezi Aprili na hadi wakati wa kuandika ripoti hii hakuna ambaye amelipwa.
Kenya bado haijawatoa watuhumiwa watatu wanaotakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kwa madai ya kuvuruga ushahidi katika kesi zinazohusiana na vurugu za uchaguzi wa mwaka 2007/2008. Kesi zingine za ICC dhidi ya Kenyatta, Makamu wa Rais William Ruto, na mtangazaji wa zamani Joshua arap Sang, zilikwama kutokana na shutuma za kuvurugwa kwa ushahidi na kukosekana kwa ushirikiano na serikali.
Mamlaka bado haijachunguza mauaji mengi yaliyofanyika kwenye makazi yasiyo rasmi ya Nairobi. Mwaka 2018, Mamlaka Huru ya Uchunguzi wa Polisi au ijulikanavyo kama Independent Policing Oversight Authority (IPOA), taasisi ya kiraia ya kuwajibisha polisi, iliviambia vyombo vya habari kwamba ilikuwa inachunguza mauaji 243 yaliyofanywa na polisi, lakini taasisi hiyo inaonekana ilielemewa na idadi ya kesi na kuhujumiwa na kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa polisi. Taasisi hiyo iliweza kuwatia hatiani maofisa watatu tu tangu ilipoanza kufanya kazi mwaka 2012, kwa mujibu wa vyombo vya habari.
Unyanyasaji wa Vikosi Vya Usalama
Mwezi Julai 2019, Human Rights Watch iligundua kwamba askari polisi wa Kenya iliua si chini ya wanaume na wavulana 21 katika makazi yasiyo rasmi ya jiji la Nairobi, bila kuwa na sababu yoyote, wakidai kwamba watu hao walikuwa ni wahalifu. Watetezi wa haki za binadamu katika eneo hilo wanaamini kwamba, kutokana na visa wanavyovifahamu na vile vilivyoripotiwa na vyombo vya habari, askari polisi wamewauwa watu wengine wengi zaidi mwaka uliopita. Mwezi Oktoba 2018, gazeti la Daily Nation liliripoti kwamba polisi waliua si chini ya watu 101 jijini Nairobi na zaidi ya watu 180 nchini Kenya katika kipindi cha miezi tisa pekee.
Mwezi Februari, mwanaharakati wa Kenya, Caroline Mwatha Ochieng, aliyekuwa akifanya kazi na wenzake ya kutunza kumbukumbu ya mauaji yaliyosababishwa na polisi katika makazi yasiyo rasmi, alikutwa ameuwawa katika mazingira ya kutatanisha ambapo polisi wanasema kifo chake hakihusiani na kazi aliyokuwa akiifanya, kama wasemavyo wanaharakati.
Mwezi Novemba, video ilikuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii ikionyesha polisi akimpiga mwanafunzi mwandamanaji katika kampasi ya chuo kikuu Nairobi, ikaibua hasira kwa umma juu ya matumizi ya nguvu za kupindukia yanayofanywa na jeshi la polisi.
Mwezi Disemba 2018, Human Rights Watch ilitoa ripoti ikiorodhesha vitendo vya udhalilishaji, vitisho na manyanyaso mengine kwa wanaharakati wa mazingira wapatao 35 katika mji wa Lamu katika kipindi cha miaka mitano. Maofisa wa usalama mjini Lamu wamevunja maandamano, kudhibiti mikutano ya umma na kutishia, kukamata na kuwashitaki wanaharakati kwa makosa mbalimbali, ikiwemo ugaidi.
Wanaharakati wamekuwa wanapinga madhara ya kimazingira na ya kiafya yatokanayo na miradi mbalimbali iliyohusiana na mradi wa usafiri wa bandari ya Lamu-Sudani Kusini-Ethiopia ( Lamu Port-South Sudan-Ethiopia Transport corridor (LAPSSET)). LAPSSET, mradi mkubwa wa miundo mbinu unaopangwa kutekelezwa Afrika Mashariki unajumuisha bandari mjini Lamu, viwanja vitatu vya ndege vya kimataifa, barabara na reli, majiji ya burudani na mtambo wa nishati wa makaa ya mawe.
Udhalilishaji Wakati wa Kuwaondoa Watu kwenye Ardhi Yao
Mamlaka zimefanya udhalilishaji wa hali ya juu wakati wakiziondoa jamii katika eneo la msitu wa Masai Mau, ambao mamlaka zinasema walivamia eneo la msitu huo. Kuondolewa huku kwa nguvu ambako kumekuwa kukifanyika tangu mwaka 2014, kumekuwa kwa kidhalilishaji zaidi mwezi Julai na Disemba mwaka 2018, wakati ambapo maafisa wa usalama waliwapiga watu, wakachoma nyumba moto na kuharibu mazao, huku wakiwaacha maelfu ya watu bila makazi wakati wa kipindi cha baridi. Human Rights Watch walikuta si chini ya watu tisa, ikiwa ni pamoja na watoto, waliouwawa wakati wa kuondolewa kwa watu hao na wengine wanne ambao hadi leo haijulikani walipo.
Mamlaka bado hazijachunguza udhalilishaji huu, na mwezi Agosti walitangaza mipango kuanza kwa awamu ya pili ya uondoaji wa kundi lingine la watu lililo bado likiishi katika msitu huo. Miongozo ya Kenya na ile ya kimataifa juu ya kuwaondoa watu inawataka mamlaka kutoa muda wa kutosha, na kuwapatia fidia au makazi mapya wale waliondolewa. Waliondolewa na jamii ambazo bado zipo katika msitu huo wa Mau walipeleka pingamizi lao mahakamani juu ya uhalali wa kutolewa katika eneo hilo mwaka 2018 na kutaka uondoshwaji huo usimamishwe.
Uhuru wa Kujieleza na wa Vyombo Vya Habari
Baraza la Habari la Kenya liliripoti kwamba mwezi Mei 2017 na Aprili 2018, palikuwa na si chini ya matukio 94 ya udhalilishaji wa waandishi wa habari na wanabloga nchini Kenya, idadi kubwa kuwahi kutokea. Mara nyingi katika visa hivyo, polisi, na nyakati zingine, raia walio na mahusiano na wanasiasa, waliwatisha na kuwashambulia wanaharakati na waandishi wa habari walio kazini. Mamlaka zilishindwa kuchunguza vya kutosha au kumuwajibisha yeyote kwa mashambulio, udhalilishaji, na vitisho dhidi ya waandishi wa habari.
Polisi wamevuruga na kupiga marufuku maandamano, kuwakamata na kuwashikilia wanaharakati, kinyume na katiba inayotoa haki ya kuandamana. Julai 19, polisi waliwapiga bomu la machozi na kuwashikilia wanaharakati watatu waliokuwa wakiandamana katika jiji la Nairobi kwa ajili ya amani ya Sudani Kusini. Wanaharakati hao waliachiwa huru baadae bila mashtaka yoyote yale. Julai 21, polisi waliwakamata wanaharakati 12 wa haki za binadamu kwa kufanya mkutano wa hadhara kujadili masuala yanayoikabili shule ya jamii katika eneo la Mathare la Nairobi. Baadae waliachiwa bila mashtaka yoyote.
Mwezi Machi, serikali ilichapisha mswada mpya, Mswada (Marekebisho) wa Utulivu wa Jamii, 2019, ukitaka kubadilisha sheria iliyopo ili kuwafanya waandaji wa maandamano na mikutano ya hadhara kuwa wahusika pale panapotokea upotevu wa maisha au uharibifu wa mali na kuwataka kulipa fidia kwa wale walioathirika na maandamano. Ikiwa mswada huu utapitishwa, sheria mpya itadhibiti maandamano na uhuru wa watu kujieleza, kinyume na katiba, inayotoa haki hizi.
Mamlaka zilijaribu kuleta hatua kali za kitawala zinazodhibiti uhuru wa watu kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari. Mwezi Mei, Bodi ya Filamu ya Kenya (Kenya Film Classification Board) mamlaka ya udhibiti ya serikali, ilichapisha kanuni mpya na adhabu kali kuhusiana na kupiga video na kuonyesha filamu. Hata hivyo kanuni hizi zilitolewa baada ya malalamiko kutoka kwa umma.
Utambulisho wa Kijinsia na Ulengwa wa Mapenzi
Mwezi Mei, Mahakama Kuu ilithibitisha vipengele vya sheria ya adhabu vinavyotoa adhabu kwa mahusiano ya mapenzi ya hiari ya jinsia moja kwa hadi miaka 14 jela. Makundi matatu ya wanaharakati wa wasagaji, wasenge, na waliobadilisha jinsia (LGBT) wamekata rufaa kupinga uamuzi huo.
Mahakama ya Rufaa ilipitisha hukumu mbili zilizothibitisha haki za watu wa LGBT, moja ikihusu haki ya uhuru wa kukusanyika, na nyingine ikiruhusu mwanamke aliyebadili jinsia kubadili jina lake pia na kuondoa alama na kipengele cha jinsia kutoka katika cheti chake cha kumaliza shule.
Wakimbizi na watafuta hifadhi ambao ni LGBT kutoka nchi jirani wanakumbana na mashambulizi katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma na katika mitaa ya Nairobi mjini. Mwezi Juni, waliwarudisha kwa nguvu kundi la LGBT la wanaotafuta hifadhi kutoka Nairobi kurudi Kakuma, mbali kukiri kwa shirika la UNHCR kwamba haliwezi kuwalinda wakiwa kambini. Kutokana na uanaharakati wa makundi ya wenye jinsia mbili, mwezi wa Agosti Kenya ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kuweka kipengele cha jinsia mbili katika sensa yake.
Wadau Muhimu wa Kimataifa
Wakiwa na wanajeshi wake ambao bado wapo Somalia na Sudani ya Kusini, Kenya bado ni mbia muhimu, na inaendelea na juhudi zake za kupambana na ugaidi, katika ukanda huo. Hata hivyo, mwaka 2019, mivutano kati ya Kenya na Somalia iliyotokana na ugomvi wa mipaka wa majini katika eneo lenye hifadhi kubwa ya mafuta katika bahari ya Hindi – ugomvi utakao amuliwa na Mahakama ya Ushuluhishi ya Kimataifa – ulionekana kuongezeka. Mwezi Februari, Kenya, kwa mara ya tatu ndani ya miaka saba, ilitishia kuifunga kambi ya wakimbizi ya Daadab ifikapo mwezi Agosti kwa sababu za kiusalama.
Mwezi Mei, Kenya iliwakatalia wabunge watatu wa Somalia na waziri mmoja kuingia nchini kwa hati za kusafiria za Somalia, kitendo kilichopelekea uhasama wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili na kuongeza hali ya kutoaminiana na kuelewana. Viongozi wa Somalia walioonyesha pasi za kusafiria zisizo za Somalia wenyewe waliruhusiwa kuingia nchini.