Skip to main content

Kenya

Matukio ya 2021

Wanachama wa mashirika kadhaa yanayohudumu katika eneo wakitembelea familia katika makazi ya Mathare jijini Nairobi na kutoa msaada wa barakoa na chakula kwa watu walioathirika kiuchumi kufuatia katazo la kutoka nje kutokana na Covid-19.

© 2020 Billy Mutai / SOPA Images/Sipa via AP Images

Mwelekeo wa masuala ya haki za msingi nchini Kenya unaendelea kuibua wasiwasi, huku serikali ikiendelea kushindwa kuhakikisha kwamba waliokiuka haki za kimsingi Mwaka 2021 wanachukuliwa hatua. Kenya inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu mwezi Agosti, 2022 na yafaa ikumbukwe kwamba ni nchi yenye historia ya vurugu misimu ya uchaguzi. Mfano, punde baada ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2017 polisi waliwakabili kwa ukatili wafwasi wa upinzani waliokuwa wakilalamikia kile walichokitaja kuwa wizi wa kura. Harakati za polisi zilisababisha mauaji ya watu zaidi ya 100 nchini Kenya. Licha ya hayo mamlaka nchini Kenya haijachukua hatua zozote za kuhakikisha maafisa wa polisi waliohusika wamechukuliwa hatua kufuatia dhuluma hizo na zile za awali.

Katikati ya Mwaka 2021, serikali ya Kenya iliagiza kambi za wakimbizi za Daadab na Kakuma zifungwe kufikia mwezi juni Mwaka 2022, hiyo ni licha ya hali ya maisha katika nchi ambapo wakimbizi hao walitoroka (Somalia na Sudan) haikuwa imebadilika- si vyema watu waliokimbia kurudi walikotoroka hali ikiwa ingali ilivyokuwa.

Janga linaloendelea la Korona (Covid-19) limewasababishia watu wengi maafa huku baadhi nchini Kenya wakifilisika. Idadi kubwa ya watu na hata familia zilipoteza njia za kujipatia riziki; wengi walifutwa kazi huku baadhi wakipoteza biashara zao kutokana na kukosa wateja kwa sababu ya masharti ya kuzuia ueneaji wa Korona.

Suala la polisi kuwaua watu badala ya kufuata mkondo uliowekwa na sheria, baadhi ya mauaji yakifanyika wakati wa kafyu, bado halijashughulikiwa hadi sasa. Taasisi mbili zinazofuatilia na kuchunguza utendakazi wa idara ya polisi; Mamlaka huru ya kutathmini utendakazi wa polisi (IPOA), na kitengo cha idara ya polisi kinachochunguza utendakazi mle ndani (PIAU), zimeshindwa kushughulikia suala hili. Hali hii inatokana na sababu mbali mbali ikiwemo ukosefu wa shinikizo kutoka kwa wakuu wa kisiasa serikalini na kwamba uchunguzi wa kina ufanywe ili wahusika kwenye visa vya mauaji yanayofanywa na polisi wachukuliwe hatua. Mamlaka ya IPOA ilianza kuhudumu nchini Kenya Mwaka 2012, miaka minane baadaye, IPOA imewafungulia mashtaka watu tisa tu. Tisa hao wametuhumiwa kwa makosa mbali mbali, mengi yakihusu mauaji- hii ni licha ya Mamlaka hiyo kuanza kuchanguza zaidi ya visa 500 kila mwaka

Dhuluma zinazofungamana na msimu wa janga la Korona (Covid-19)

Kwenye ripoti iliyotolewa mwezi Julai, 2021, ya uchunguzi wa athari za kiuchumi na kijamii za janga la Korona (Covid-19) kwenye mitaa ya watu wa mapato ya chini jijini Nairobi, Shirika la Human Rights Watch lilipata kwamba janga la Korona liliharibu njia za mapato za wengi huku maalfu ya familia zikipoteza riziki zao –biashara zilisambaratika, maduka yakafungwa kwa sababu ya kukosa wateja, wengi wakafutwa kazi huku wakiathirika kwa njaa na kufukuzwa katika makazi yao. Watoto walikosa chakula huku waliokuwa na mahitaji ya dharura ya matibabu wakikosa huduma hizo.

Mamlaka nchini Kenya ilionyesha uzembe kila mara maafisa walipohitajika kuwasaidia watu wasiojiweza na hasa makundi kama hayo kwenye mitaa ya watu wa mapato ya chini. Hali iliendelea hivyo na hata serikali ilipoanzisha mpango wa miezi minane wa kuwafadhili watu kwa pesa, haukuwa na manufaa kwa wengi – ulifanyika kwa muda mfupi. Walioanzisha mpango huo hawakutoa habari kuhusu nani alifaa kunufaika au uliwalenga akina nani, ama ni vipi waliofaa kusaidiwa walitambuliwa na kuorodheshwa au ni kwanini maalfu ya familia zilizofaa kusaidiwa ziliachwa nje.

Serikali ya Kenya, ikiwa na jukumu la kuhakikisha kwamba hakuna raia analala njaa, ilishindwa kuanzisha mpango wa kuwafadhili watu ambao ungemhakikishia kila mtu, sio wachache tu, viwango vya maisha vinavyowafaa wanadamu katika msimu mzima wa janga la Korona. Ni sehemu kidogo ya familia zenye mahitaji mengi jijini Nairobi zilizonufaika kwa mpango huo. Ni mpango uliotatizwa kwa ukosefu wa uwazi, pia ukaathirika kwa watu kuwasaidia marafiki zao. Aidha kulikuwa na suala la watu kuwasaidia watu wa ukoo wao na jamaa zao na kukawa na mapendeleo ya moja kwa moja. Maafisa nchini Kenya walithibitisha kwamba mpango huo uliwafikia watu 29,000 kati ya maboma zaidi ya 600, 000 katika mitaa minane ya watu wa mapato ya chini jijini Nairobi. Idadi hii ni takriban asilimia 4.8 pekee ya maboma yote yaliyohitaji usaidizi wa haraka na wa dharura.

Dhuluma zilizofanywa na vyombo vya usalama

Licha ya ukosoaji kutoka kwa umma maafisa wa polisi waliendelea kutumia nguvu za kupita kiasi kila walipokuwa wakitekeleza kanuni zilizokuwa zimetangazwa kukabili ueneaji wa virusi vya Korona mwaka 2021. Huku serikali ikiwa imeanza kufungua nchi kwa kupunguza masharti- isipokuwa kuendelea kwa kafyu ambayo baadaye iliyondolewa mwezi Oktoba, ukatili wa polisi uliendelea.

Agosti tarehe 1, 2021, polisi mjini Kianjokoma, kaunti ya Embu, eneo la mashariki ya Kenya, waliwazuilia ndugu wawili Emmanuel Marura Ndwiga, wa umri wa miaka 19, na Benson Njiru Ndwiga, wa umri wa miaka 22, wakiwatuhumu kwa kukiuka masharti ya kafyu –kwamba walifaa kuwa nyumbani kufikia saa nne usiku. Jamaa za wawili hao walipata maiti yao katika mochari ya eneo siku tatu baadaye. Maafisa wa polisi waliowatia nguvuni ndugu hao walidai kwamba walianguka kwenye gari lililokuwa likienda- hata hivyo ripoti ya upasuaji ilionyesha kwamba maiti za ndugu hao zilikuwa na majeraha ya kichwa na mbavu- kinyume cha madai ya polisi kwamba walianguka tu! Matokeo ya uchunguzi wa maiti yalisababisha maandamano ya kukosoa utendakazi wa polisi ambayo pia polisi waliyakabili kwa nguvu kupita kiasi ambapo pia walimuua mtu mmoja - Embu. Agosti tarehe 15, mkurugenzi wa idara ya mashtaka ya umma Noordin Haji aliwafungulia mashtaka maafisa sita wa polisi kwa makosa ya kuwaua ndugu hao wawili.

Kwenye visa vingine, mfano katika kisa kumhusu Robert Mutahi, maafisa wa polisi walikusanya pesa za hongo kutoka kwa watu waliokuwa wametiwa nguvuni kwa kupatikana wamekiuka masharti ya kafyu. Mutahi aliviambia vyombo vya habari kwamba polisi walimzuilia Agosti tarehe 12 na kumlazimisha kuwatumia pesa kwa njia ya simu. Maafisa hao watatu tayari wamefunguliwa mashtaka kwa tuhuma za wizi wa mabavu.

Haki za wakimbizi

Mwezi Machi, 2021, mamlaka nchini Kenya ilitoa makataa ya wiki mbili kwa shirika la umoja wa mataifa la wakimbizi UNHCR, kuandaa mpango ambao ungewezesha kufunga kambi za wakimbizi za Daadab na Kakuma, ikisema kulikuwapo tishio la usalama wa nchi kwenye kambi hizo. Kufikia Mwaka 2021 kambi hizo zilikuwa na watu zaidi ya 433,000 wote wakiwa wakimbizi wengi wao walikuwa raia wa somali na Sudan kusini.

Mwezi Aprili, serikali ilitangaza nia ya kufunga kambi zote mbili kufikia Juni, 2022, hatua hiyo ilifuatiwa na Shirika la UNHCR kupendekeza mpango uliofaa kutumiwa katika kuwarejesha wakimbizi makwao kwa hiari, baadhi ya “hatua za kuwarejesha katika nchi zisizo zao kutoka kambini,” ikiwemo “kuwapa nafasi wakimbizi ambao walitaka kuendelea kuishi Kenya hasa wale wa kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya Africa Mashariki (EAC).” Hata hivyo nchi hizo hazikujumuisha Somalia ambapo hatua za awali za kuwapa idhini wakimbizi kurejea ‘kwa hiari’ zilibadilika kuwa za kuwalazimisha na hata kutumia nguvu. Hii ni licha ya hali ya usalama nchini Somalia na Sudan Kusini kusalia kuwa mbaya wala zisizofaa wakimbizi kurejea kwao- bila shaka kulikuwa na hofu ya wao kushikwa wateswe au hata kuuawa.

Kenya iliwahi kutisha kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab 2016 na 2019 ikidaiwa kuwa maficho ya wanachama wa kundi la ugaidi la Al-Shabaab. Mamlaka nchini Kenya haijawahi kutoa ushahidi wowote kuunga mkono au kutetea madai hayo. Aidha miongoni mwa wakimbizi waliomo kwenye kambi ile hakuna hata mmoja amewahi kushikwa na kushtakiwa kwa makosa ya kuwa na uhusiano na magaidi.

Mwezi Mei, 2021, raia wa Uturuki Selahaddin Gülen, ambaye alikuwa ameomba hifadhi nchini Kenya-kukimbilia mafichoni, alirejeshwa kwa lazima nchini Uturuki tena katika hali ya kutatanisha. Alikuwa ameingia Kenya Oktoba Mwaka 2020, Gülen alizuiliwa na maafisa wa uhamiaji kwa sababu ya ilani kutoka mtandao wa kimataifa wa polisi –Interpol, iliyotoka Uturuki. Mamlaka nchini Kenya Ilianzisha mpango wa kumwondoa nchini lakini baadaye maafisa wakabadilisha utaratibu na kuamua kumfurusha Kenya.

Tarehe 3, Mei, 2021, wakati wa mojawapo ya taratibu za kufika mbele ya idara ya Upelelezi wa Jinai jijini Nairobi kufungamana na maagizo ya Mahakama, Gülen aliripotiwa kutojulikana alipo. Raia mwingine wa Uturuki ambaye alikuwa ameandamana na Gulen kuelekea katika makao makuu ya idara ya Upelelezi(DCI) ambaye pia alitoweka kwenye shughuli ile baadaye alionekana akiachiliwa huru na mamlaka nchini Kenya tarehe 5 Mwezi Mei. Tarehe 31 Mwezi Mei, serikali ya Uturuki ilitoa picha ya Gülen akiwa na pingu mikononi jijini Ankara –Uturuki. Uturuki ilisema kwamba Gulen alikuwa amekamatwa na maajenti wa idara ya ujasusi ya Uturuki katika nchi ya kigeni na sasa alikuwa mikononi mwa chombo cha Uturuki kinachokabiliana na ugaidi. Kuondolewa nchini kwa lazima kwa Gulen na hali alikuwa mtu aliyesajiliwa kwa kuomba hifadhi ili awe mafichoni, ilikiuka jukumu la Kenya la kuwasaidia watu wanaotorokea usalama chini ya kanuni za kimataifa.

Ufurushaji wa Lazima

Tarehe 5 Februari, 2021, shirika la serikali liliwafurusha kwa lazima bila kutoa notisi kwa watu takribani 3,500 wa jamii ya Wanubi kutoka makazi yao kwenye eneo la Kibos, Kaunti ya Kisumu. Jamii ya Wanubi nchini Kenya inaaminika kutoka kwa vizazi vya wanajeshi waliosafirishwa kwa lazima kutoka Sudan na Serikali ya kikoloni ya Uingereza karne iliyopita. Kwa sasa inakadiriwa kwamba zaidi ya Wanubi 100,000, wameshindwa kupata uraia wa Kenya na kubaki bila utaifa. Polisi waliokuwa na silaha walitumia vitoza machozi kuwalazimisha wakazi kutoka katika nyumba zao licha ya amri ya mahakama kusitisha ufurushaji huo, vilevile sitisho la muda la rais kwa ufurushaji mnamo Mei 1, 2020, wakati wa Janga la Korona. Mtoto alikwama ndani ya takataka ambapo aliuliwa na tinga ambalo lilibomoa nyumba yao.

Haki za Wanawake na Wasichana

Katika ripoti ya Septemba 2021 kuhusu dhuluma za kijinsia (GBV), Shirika la Human Rights Watch liligundua kwamba Kenya, sawa na nchi nyingine duniani kote, ilirekodi ongezeko la unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana wakati wa masharti ya kuzuia ueneaji wa Korona yaliyositisha shughuli zote na kuendelea kwa marufuku ya kuwa nje usiku. Licha ya historia ya awali kuonyesha ongezeka la matukio ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana wakati wa majanga, Serikali ya Kenya ilishindwa kuweka mikakati ya kusaidia na kukabili unyanyasaji wa kingono na dhuluma za kijinsia GBV; kuchunguza na kushughulikia kesi ipasavyo; na kuhakikisha waathiriwa wanapata matibabu kwa wakati unaofaa, huduma za kisaikolojia na kijamii, huduma za ulinzi na usaidizi wa kifedha. Mwezi Mei, Rais Uhuru Kenyatta alitoa ahadi ya kuhakikisha nchi inakomesha dhuluma za kijinsia ifikapo 2026, akiahidi kutenga dola milioni 23 za Marekani kufikia 2022 , ili kuongezeka hadi dola milioni 50 ifikapo 2026.

Ni jukumu la Serikali ya Kenya kuzuia, kupinga, na kutoa suluhisho ya kukabili dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana wakati wote, ikiwa ni pamoja na wakati wa majanga na katika mazingira ya binadamu. Kwa kuzingatia janga la Korona ambalo lingalipo, serikali inapaswa kuangazia mapungufu haya na kubuni mfumo imara wenye misingi ya utetezi wa haki ili kushughulikia dharura zinazohusiana na dhuluma za kingono na GBV kuelekea uchaguzi mkuu ulioratibiwa 2022.

Haki za Mahusiano ya Jinsia Moja LGBTI

Mnamo Septemba 23, Bodi ya Kudhibiti Filamu nchini (KFCB) ilipiga marufuku filamu iliyokuwa na maudhui ya usenge kwa jina, "I am Samuel," ikisema filamu hiyo ilijaribu "kukuza ndoa za jinsia moja. Hiyo ni filamu ya pili yenye maudhui ya mapenzi ya jinsia moja kupigwa marufuku nchini Kenya, kufuatia uamuzi wa 2018 wa kuzuia kuonyesha filamu ya "Rafiki, " hadithi ya mapenzi ambayo ilikuwa filamu ya kwanza ya Kenya kuonyeshwa kwa mara ya kwanza katika tamasha ya filamu ya Cannes. Marufuku ya "Rafiki" ("friend" katika Kiswahili) baadaye ilibatilishwa na mahakama, na filamu hiyo ikaruhusiwa kuuzwa kwa watazamaji wa Nairobi," kisha baadaye marufuku ikarejeshwa.

Sehemu ya 162 ya Sheria za Uhalifu nchini Kenya inatoa adhabu kuhusu mahusiano ya jinsia moja hadi kifungo cha miaka 14 gerezani. Mahakama Kuu ilikataa pingamizi la kikatiba la kutaka kuondoa marufuku hiyo mnamo Mei 2019. Wanaharakati wamekata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa misingi kwamba kifungu cha 162 kinakiuka haki za usawa, kutobaguliwa, utu wa kibinadamu, usalama, usiri na afya, licha ya kulindwa kulindwa chini ya katiba ya Kenya. Kwa sasa wanasubiri kesi hiyo kusikilizwa katika Mahakama ya Rufaa.

Wahusika Wakuu wa Kimataifa

Kwa sasa Kenya inashikilia nafasi mbili muhimu za uongozi wa kimataifa na kikanda. Mnamo Januari, Kenya ilianza kuhudumu muhula wake wa miaka miwili ya mwanachama asiyekuwa wa kudumu katika Baraza la Usalama katika Umoja wa Mataifa (UNSC). Rais Uhuru Kenyatta alichukua hatamu za kuwa mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) mwezi Februari. Kenya ikiwa na vikosi vyake nchini Sudan Kusini na Somalia, ilijiunga na mataifa mengine katika UNSC mwezi Julai ili kuidhinisha Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Afrika kufuatilia madai ya ukatili uliofanywa katika eneo la Tigray nchini Ethiopia. Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika Umoja wa Mataifa UN Martin Kimani alihimiza pande ambazo zinazozana katika eneo la Tigray kusitisha mapigano. Alisema Kenya ilikuwa inatazamia uchunguzi wa kina ili wahusika wachukuliwe hatua.

Kenya ilipata usaidizi mkubwa wa kukabili athari za Janga la Korona (Covid-19) kutoka kwa washirika wa kitaifa na wa kimataifa. Marekani, Uingereza, Uchina, Umoja wa Ulaya na nchi binafsi za Ulaya kama vile Ujerumani zilitoa msaada wa nyenzo, kiufundi na kifedha ili kusaidia Kenya kukabili janga hili. Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa namna mbalimbali zimetoa misaada ya kifedha na miradi kwa Kenya tangu mwanzo wa janga hili. Mnamo Juni 2021, Benki ya Dunia iliidhinisha msaada wa kifedha wa dola milioni 750, kwa sehemu kusaidia Kenya kukabili janga la Korona.