Skip to main content

Tanzania

Matukio ya 2019


Mkazi wa Buguruni atoa kura yake katika kituo cha kupigia kura wakati wa uchaguzi wa ndani katika jiji la Dar es salaam, Tanzania, Novemba 24, 2019. - watanzania wataelekea kupiga kura kupiga kura katika uchaguzi wa ndani ambao umepigwa na vyama vya juu vya upinzaji nchini madai ya kudanganya kulingana na media za ndani.

ERICKY BONIPHACE/AFP via Getty Images

Rekodi ya haki za binadamu ya Tanzania imeendelea kuporomoka chini ya Rais John Magufuli, ambaye alichaguliwa mnamo mwaka 2015. Serikali iliondoa baadhi ya makatazo katika kuchapisha takwimu binafsi, lakini imeendelea kuminya vyombo vya habari na wakosoaji wa serikali, kufutia usajili makundi ya asasi za kijamii, kuwakamata waandishi wa habari, kuminya uhuru wa kiraia, na kukandamiza haki za wanawake na watoto.

 

Uhuru wa Kujieleza na wa Habari

 

Serikali ya Tanzania imekandamiza vyombo vya habari, asasi za kiraia na raia wakosoaji wa serikali. Mwezi Februari, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ililifungia gazeti la The Citizen kwa siku saba kwa kukiuka Sheria ya Huduma ya Vyombo Vya Habari, ikilishutumu kwa kuchapisha makala mbili zilizo na upendeleo. Moja ilihusu wasiwasi wa mbunge wa Marekani Bob Mendez juu ya “mmomonyoko wa taratibu wa uhuru wa kiraia nchini Tanzania”, na makala nyingine ilihusu shilingi ya Tanzania kuporomoka ikilinganishwa na dola ya Marekani.

 

Tarehe 25 Aprili, mamlaka katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam walimkamata na kisha kumrudisha alikotoka Wairagala Wakabi, mkurugenzi wa shirika lililo na makazi yake nchini Uganda, Collaboration on International ICT Policy in East and Southern Africa (CIPESA), alipokuwa akielekea kupokea tuzo ya haki za binadamu.

 

Tarehe 29 Julai, 2019, askari waliovalia nguo za kiraia walimkamata mwandishi nguli wa habari za kiuchunguzi Erick Kabendera akiwa nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Baadae alishitakiwa kwa makosa yasiyo na dhamana ikiwa ni pamoja na utakatishaji fedha, kukwepa kodi na kuongoza genge la uhalifu. Kabendera amekuwa akiandikia magazeti mengi ya kimataifa habari zilizokosoa siasa za Tanzania, ikiwa ni pamoja na The East African, The Guardian na The Times of London.

 

Tarehe 22 Agosti, polisi walimkamata Joseph Gandye, mwandishi wa Watetezi TV, jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na polisi. Gandye, alikuwa amechapisha taarifa ya kiuchunguzi juu ya ukatili wa polisi mjini Mafinga Iringa kusini mwa Tanzania tarehe 9 Agosti. Tarehe 23 Agosti, polisi walimwachia Gandye bila ya kumfungulia mashtaka yoyote.

 

Mwaka 2018, bunge lilipitisha Kanuni za Maudhui za sheria ya Huduma za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta huku zikiipa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mamlaka makubwa  kutoa leseni kwa blogu, mitandao na maudhui mengine ya mtandaoni.

 

 Mwezi Januari, Mahakama Kuu mjini Mtwara ilitupilia mbali ombi la mashirika mbalimbali ya kiraia  ikiwa ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), viongozi wa Baraza la Habari Tanzania, na Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) waliokuwa wanapinga kanuni hizo.

 

Mwishoni mwa mwaka 2018, Bob Chacha Wangwe alikata rufaa ya kesi yake ya mwaka 2017 iliyohusu uchapishaji wa taarifa za uongo chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao kwa kukosoa kupitia ukurasa wake wa Facebook mwenendo wa uchuguzi  wa Zanzibar wa 2015. Mahakama ya jijini Dar es Salaam ilimuhukumu kwenda jela kwa muda wa miezi 18 au kulipa faini milioni 5 za KItanzania, sawa na $2,175. Mwezi Machi, Bob Chacha Wangwe alishinda rufaa yake Mahakama Kuu iliyokuwa ikipinga hukumu ya awali, huku Mahakama Kuu ikisema hapakuwa na ushahidi wa kutosha.

 

Mabadiliko ya Kisheria

 

Mwezi Juni, bunge lilirekebisha Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015  ambayo mwanzoni ilitamka kuwa kosa kuchapisha takwimu ambazo hazijapitishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Sheria iliyorekebishwa iliondoa kipengele cha kosa la jinai kuchapisha taarifa huru za takwimu na kuruhusu kwamba kila mtu ana haki ya kukusanya na kusambaza taarifa hizo, ikiwa ni pamoja na zile zilizo kinyume na  zile za Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

 

Mwezi Machi, Mahakama ya Afrika Mashariki iliamua kwamba Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ilikiuka mikataba ya Afrika Mashariki na kuitaka serikali ya Tanzania kuirekebisha ili iendane na mkataba huo. Kufuatia hukumu hii, serikali ilionyesha utayari wa kufanya majadiliano na wadau wa vyombo vya habari juu ya sheria za vyombo vya habari lakini haikubadilisha sheria hiyo.

 

Wapinzani wa Serikali na Wakosoaji Wengine

 

Serikali imeendelea kuwadhibiti wanasiasa wa upinzani. Mwezi Januari, Bunge lilipitisha mabadiliko ya sheria ya Vyama Vya Siasa ya mwaka 2002, ambayo yalimpa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka makubwa ya kutaka taarifa kutoka vyama vya siasa, kuwafukuza wanachama wa vyama vya siasa, na kuzitaka aidha taasisi au watu binafsi kupata ruhusa kutoka kwa Msajili kutoa elimu ya uraia, vinginevyo kufanya kosa la jinai likiwa na adhabu aidha ya kufungwa jela au kutoa faini.

 

Viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hivi sasa wanakabiliwa na mashitaka ya uchochezi na kufanya mikutano ya hadhara “kinyume na sheria” mnamo Februari 2018. Tarehe 7 Machi, Mahakama Kuu iliamuru kwamba wanasiasa wa Chadema Freeman Mbowe na Esther Matiko, ambao walikuwa wamewekwa rumande tangu Novemba 23, 2018, kwa kushindwa kufika mahakamani katika kusikilizwa kwa kesi yao, kuachiwa huru na kurudishiwa dhamana yao.

 

Mwezi Mei, watu wenye silaha walimteka Mdude Nyagali, mkosoaji maarufu na mwanaharakati wa upinzani, alipokuwa akitoka kazini Mbozi kusini mwa Tanzania usiku wa Mei 5, kwa mujibu wa waraka kutoka chama cha Chadema. Nyagali alipatikana tarehe 9 Mei, eneo la Inyala, takribani kilometa 150 kutoka Mbozi, akiwa amejeruhiwa vibaya na kushindwa kuzungumza.

 

Utambulisho wa Jinsia na Ulengwa wa Mapenzi

 

Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998  ya Tanzania inatamka kujamiana kwa hiari kwa wapenzi wa jinsia moja kuwa ni kosa linalobeba adhabu ya hadi kifungo cha maisha. Serikali imevifunga vituo kadhaa vya huduma kwa wasagaji, wasenge, wanaojamiiana na jinsia zote na wale waliobadili jinsia pamoja na makundi mengine maalumu na kupiga marufuku usambazaji wa vilainishi, vifaa vinavyozuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi .

 

Ijapokuwa katika mkutano wa Novemba 17 na maofisa waandamizi wa  Benki ya Dunia  Rais Magufuli aliahidi kwamba Tanzania isinge “tekeleza vitendo vyovyote vya kibaguzi vinavyohusiana na unyanyasaji na/au ukamatwaji wa watu, kutokana na ulengwa wao wa kimapenzi,” ukamataji kwa sababu ya ulengwa wa kimapenzi umeendelea kufanyika.

 

Mwezi Aprili, serikali iliifungia CHESA, shirika linalohudumia jamii ya mashoga (LGBT), pamoja na mashirika mengine kama Kazi Busara na Hekima (KBH Sisters), na Shirika la Maendeleo Tanzania (AHA Development Organisation  in Tanzania), kutokana na madai kwamba mashirika haya yalikiuka sheria, maadili na mila za Kitanzania. Mwezi Septemba, naibu waziri wa mambo ya ndani aliwataka polisi kuwakamata “wanaohamasisha mapenzi ya jinsia moja.” Serikali halijatimiza ahadi yake kwa wahisani wa kimataifa juu ya kuacha rasmi upimwaji wa kulazimishwa wa haja kubwa, mbinu ya kidhalilishaji „inayopima” dalili za ushiriki wa mapenzi ya jinsia moja.

 

Haki za Watoto

 

Mwaka 2017, Rais Magufuli  alipiga marufuku wasichana wajawazito na kina mama watoto kuendelea na shule .  Polisi wamekuwa wakiwakamata wasichana wajawazito na familia zao kuwalazimisha wawataje wanaume au wavulana waliowapa mimba, huku shule zikiwalazimisha wasichana kupima ujauzito. Mwezi Juni,  Asasi za Kiraia za Tanzania ziliwasilisha malalamiko yao kwa Wataalamu wa Kamati ya Afrika ya Haki na Ustawi wa Mtoto, wakitaka sera hii ifutwe.   Baada ya mazungumzo kati ya serikali na Benki ya Dunia juu ya mkopo wa shule za sekondari, serikali iliahidi kutafuta namna ya kuwaruhusu wasichana wajawazito kurudi na kuendelea na shule.

 

Mwezi Agosti, serikali ya Tanzania’s iliwapiga marufuku waalimu  wa shule za msingi kuingia darasani na fimbo.

 

Mwezi Oktoba, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilikubali hukumu ya mwaka 2016 ya Mahakama Kuu ikiielekeza serikali kuongeza umri wa ndoa kisheria  hadi miaka 18 kwa wasichana na wavulana pia. Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971 imeweka umri wa chini wa ndoa kwa wasichana kuwa miaka 15 ikiwa na ruhusa ya wazazi, na miaka 18 kwa wavulana, na kuruhusu ndoa kati ya watoto wa miaka 14 ikiwa mahakama ikiridhika kwamba kuna mazingira maalumu, ambayo hayako wazi, yanayolazimisha ndoa hiyo.

 

Haki za Wanawake

 

Mnamo Septemba 2018, Rais Magufuli alibeza uzazi wa mpango, akiwataka wanawake kuacha kutumia dawa za uzazi wa mpango. Wiki mbili baadae, serikali ilipiga marufuku matangazo ya radio na televisheni yaliyokuwa yakihamasisha utumiaji wa uzazi wa mpango. Mwezi Machi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto waliwaandikia wakuu wote 18 wa taasisi zilizo na wajibu wa masuala ya uzazi wa mpango nchini Tanzania, wakiwataka kurudisha matangazo hayo kwenye vyombo vya habari.

 

Haki za Walemavu

 

Katika kukabiliana na mauaji na ukataji wa viungo wa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), hasa watoto, serikali ya Tanzania ilitenga “makazi ya muda”, au shule za kulala kwa watoto walio na ulemavu wa ngozi. Wakati makazi haya yamesaidia kupunguza idadi ya mashambulizi, yamekuwa na athari nyingine kubwa zaidi kwa watoto wenye ualbino. Makazi yamewafanya kujitenga na familia na jamii zao na kuwatenga katika kupata elimu na watoto wengine katika shule za kawaida.

 

Wakimbizi

 

Kati ya Septemba 2017 na Oktoba 31, 2019, Wakimbizi wa Burundi 78,380 walirudishwa kwao kutoka Tanzania chini ya makubaliano ya kuwarudisha kwa hiari yaliyofanywa kati ya Tanzania, Burundi, na Shirika la Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa (UNHCR). Mwezi Machi 2018, Tanzania na Burundi ziliweka lengo la kuwarudisha wakimbizi wa Burundi wapatao 2,000 kwa wiki chini ya makubaliano yao.

 

Mwezi Agosti 2019, mamlaka za Tanzania na Burundi zilitangaza mpango wa kuwarudisha wakimbizi wote wa Burundi 183,000 wanaoishi katika kambi tatu zilizopo Kigoma, kaskazini magharibi mwa Tanzania, kwao Burundi kufikia mwisho wa mwaka 2019. Kati ya Agosti na Oktoba, maofisa wa Tanzania walitoa vitisho hadharani, wakafunga na soko la kambi ya wakimbizi,  na wakibadilisha mara kwa mara vigezo kwa mashirika ya misaada yanayofanya kazi zake kambini.

 

Oktoba  15, mamlaka za Tanzania ziliwanyanyasa zaidi ya watafuta hifadhi 200 wasiosajiliwa wakiwataka kurudi kwao Burundi huku wakiwatisha kuzizuia hadhi zao za kisheria Tanzania.

 

Wadau Wakuu wa Kimataifa

 

Mahakama ya Afrika Mashariki bado ni mhimili muhimu wa haki za binadamu nchini Tanzania, ikifanya maamuzi muhimu kwa raia na taasisi zinazofanya shughuli zake nchini.

 

Mwezi Novemba 2018 Benki ya Dunia ilishikilia dola milioni $300 (Pauni milioni £232) za dola milioni $500 zilizokuwa mkopo wa Tanzania, zikisema ni kutokana na katazo la wasichana wajawazito kurudi shuleni. Mwezi Septemba, Benki ya Dunia ilipitisha mkopo wa dola milioni $450 kwa ajili ya matumizi ya chakula na kuinua maisha ya watu, elimu, na huduma za afya Tanzania, ikisema ni kutokana na kurekebishwa kwa Sheria ya Takwimu na ahadi ya serikali kuwawezesha wasichana  wote kumaliza elimu yao.

 

Mwezi Agosti, Ubalozi wa Marekani na Uingereza jijini Dar es Salaam ilieleza kusikitishwa kwao juu ya kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu bila kushitakiwa kwa mwandishi wa habari Erick Kabendera bila kufuatwa vyema kwa sheria.