Skip to main content

Tanzania

Matukio ya 2021

Watu wakiangalia runinga inayomuonesha Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan baada ya kuapishwa kuwa Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania kufuatia kifo cha ghafla cha Rais John Magufuli, Dar es Salaam, Tanzania mnamo Machi 19, 2021.

© 2021 STR/AFP via Getty Images

Rais Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Kwanza Mwanamke wa Tanzania Machi 19 kufuatia kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021. Magufuli alifariki ikiwa ni miezi mitano katika awamu yake ya pili kama Rais.

Rais Hassan amechukua hatua kukabiliana na baadhi ya masuala ya haki, lakini serikali iliendelea kuzuia uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa raia, kukamata waandishi wa habari na wakosoaji wa serikali kinyume na sheria, kutekeleza sheria za kibaguzi dhidi ya wanafunzi wajawazito mashuleni na kukandamiza haki za wanawake na watoto. Mamlaka pia hazijafanya uchunguzi wa maana juu ya matukio ya unyanyasaji yaliyotawala uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Sheria ya Tanzania ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 bado inaendelea kutoa adhabu ya hadi kifungo cha maisha kwa wapenzi wa jinsia moja.

Uhuru wa Kujieleza na wa Vyombo vya Habari

Ingawa Rais Hassan aliahidi kuondoa vikwazo vilivyopo kwa vyombo vya habari mnamo Aprili 6, mamlaka zimeendeleza ukandamizaji wa vyombo vya habari uliokuwa ukifanywa na utawala wa Magufuli.

Vyombo vya habari na vikundi vya haki za binadamu viliripoti kuwa mnamo Aprili 12 polisi waliwakamata waandishi wa habari Dickson Billikwija na Christopher James na kuwaweka kizuizini kwa saa tatu katika majengo ya Manispaa ya Temeke kwa maelekezo ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke.

Mnamo Aprili 21, 2021, maafisa watatu wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ), kikundi cha mgambo wenye silaha na kinachoendeshwa na Serikali ya Zanzibar walimshambulia Jesse Mikofu, mwandishi wa gazeti binafsi la Mwananchi baada ya kuwapiga picha wakiwaondoa kwa nguvu wafanyabiashara wa sokoni eneo la Darajani katika Mji Mkongwe.

Mnamo Agosti 11, 2021, serikali ililifungia gazeti la Uhuru, gazeti linalomilikiwa na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuchapisha habari inayoeleza kuwa Rais Hassan hana nia ya kugombea kiti cha Urais 2025, na kuwa gazeti la kwanza kufungiwa chini ya Rais Hassan.

Mnamo Septemba 5, 2021, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ililifungia gazeti binafsi la Raia Mwema kwa siku 30 kwa “kuchapisha mara kwa mara taarifa zisizo sahihi na uchochezi wa makusudi.” Gazeti hilo lilichapisha makala iliyomhusisha mtu mmoja aliyefyatua risasi na kuwaua watu wanne nje ya Ubalozi wa Ufaransa na chama cha CCM.

Marekebisho ya Sheria

Mnamo Aprili 21, Waziri wa Katiba na Sheria Palamagamba Kabudi aliliambia Bunge kwamba Tume ya Kurekebisha Sheria ilikuwa ikifanya kazi ya kupitia Sheria ya Uhalifu wa Kiuchumi na Makosa ya Kupanga, ambayo iliondoa dhamana kwa baadhi ya makosa ikiwemo utakatishaji fedha na ambayo serikali huko nyuma ilitumia kuwaweka kizuizini wakosoaji wa serikali na waandishi wa habari.

Mamlaka zimeanza mchakato wa kurekebisha kanuni za maudhui ya mtandaoni na maudhui ya redio na runinga ambayo ni sehemu ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta. Kanuni za sasa zinaipa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) nguvu kubwa ya kutoa leseni kwa blogu, tovuti na maudhui mengine ya mtandaoni na kuzuia watangazaji wa redio na runinga kufanya kazi na watangazaji wa kigeni bila ya uwepo wa afisa kutoka mamlaka ya mawasiliano au idara nyingine ya serikali.

Wapinzani wa Serikali na Wakosoaji Wengine

Mnamo Januari 5, mahakama jijini Dar es Salaam ilitoa amri ya kuachiwa kutoka gerezani kwa mwanaharakati wa haki za binadamu Tito Magoti na mtaalam wa teknolojia ya mawasiliano Theodory Gyan baada ya kulipa faini ya Shilingi Milioni 17.3 (US$ 7,500). Magoti na Gyan walikaa kizuizini kwa miaka miwili kwa mashitaka ya uhalifu wa kiuchumi ikiwemo utakatishaji fedha na kuendesha vikundi vya uhalifu. Mnamo Disemba 20, 2019 polisi walimkamata Magoti baada ya kumlaghai kwa kumuita katika “mkutano” kupitia ujumbe wa simu kutoka kwa Gyan, mshirika wake.

Mnamo Juni 22, Mahakama Kuu ilipindua maamuzi ya Septemba 2020 ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ya kumsimamisha mwanasheria wa haki za binadamu na mkosoaji wa serikali Fatma Karume kufanya kazi za sheria Tanzania Bara.  Kusimamishwa kwa Karume kulitokana na tuhuma za utovu wa nidhamu baada ya kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliofanywa na Rais Magufuli.

Mnamo Julai 21, polisi jijini Mwanza, kaskazini mwa Tanzania walizingira hoteli waliyofikia wanachama wa chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema na kuwakamata wanachama 11 akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe kabla ya kufanya mkutano wa kujadili marekebisho ya katiba ya nchi. Siku moja kabla ya mkutano huo mamlaka jijini Mwanza zilitangaza kuzuia “mikusanyiko isiyo ya lazima” kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Uviko-19. Baadae mamlaka zilimshtaki Mbowe kwa makosa ya uhujumu uchumi, njama na ufadhili wa vitendo vya kigaidi na kumuweka kizuini kabla ya kesi.

Mwaka 2012, serikali ilianzisha mchakato wa katiba mpya lakini mchakato ulisimama mwaka 2015 baada ya Rais Magufuli kuingia ofisini na kuweka bayana kuwa mchakato wa kupitia katiba haukuwa kipaumbele katika utawala wake na kueleza kuwa serikali yake itajielekeza zaidi katika miradi ya maendeleo. Mnamo Juni 29, Rais Hassan aliendelea na sera hii, na kueleza vyombo vya habari kuwa kabla ya nchi kujielekeza kwenye mchakato wa kurekebisha katiba kwanza apewe nafasi ya kurekebisha uchumi.

Mnamo Septemba 22, mkurugenzi wa mashtaka aliondoa mashtaka ya uchochezi dhidi ya mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu, mhariri wa gazeti Simon Mkina, mchapaji wa magazeti Ismail Mehbood na mwandishi wa habari Jabir Idrissa Yunus juu ya kichwa cha habari “Mchafuko yaja Zanzibar”katika gazeti la Mawio mwaka 2016.

Haki za Wakimbizi

Mwaka 2021, Human Right Watch ilipokea ripoti za uhakika kuhusu vitisho, unyanyasaji na ukamatwaji wa wakimbizi kutoka Burundi unaofanywa na vyombo vya ulinzi vya Tanzania. Mamlaka nchini Tanzania pia ziliwarudisha kwa nguvu maelfu ya wakimbizi kutoka Msumbiji waliokimbia machafuko kaskazini mwa jimbo la Cabo Delgado mwaka 2020 na 2021.

Mwezi Julai, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu zilieleza kusikitishwa kwa namna Tanzania ilivyowarudisha kwa nguvu zaidi ya wakimbizi 9,700 kutoka Msumbiji katika mpaka wa Negomano kati ya Januari na Juni bila ya kufanya tathmini ya mahitaji yao ya ulinzi wa kimataifa. Wengi wao walikuwa wanakimbia machafuko na katika mji wa pwani wa Palma kufuatia mashambulizi ya vikundi visivyokuwa vya serikali mwezi Machi 2021. Kuwarudisha wakimbizi hao kulikiuka kanuni za kutokurejeshwa uhamishoni chini ya vigezo vya kimataifa na sheria za kikanda za wakimbizi.

Haki za Wanawake

Mnamo Agosti 23 katika sherehe za kuwapongeza timu ya Taifa ya mpira wa miguu wanaume, rais alitoa maoni ambayo yalionyesha kumkejeli “mwanamke” na jinsia ya wachezaji wanawake wa mpira wa miguu, maoni hayo yalilaaniwa vikali na wanaharakati.

Haki za Watoto

Novemba 24, 2021, Wizara ya Elimu Tanzania iliondoa marufuku iliyokuwa inawakataza wanafunzi wenye watoto kuendelea na masomo katika shule za umma.

Mwezi Juni 2017, Magufuli alitangaza rasmi kupiga marufuku wanafunzi wajawazito na wale waliojifungua kuhudhuria shule za umma. Sambamba na makubaliano yake na Benki ya Dunia ambayo yalikuwa ni sehemu ya mkopo wa Dola za Marekani Milioni 500 ($500million) kwa program ya serikali ya Kukuza Ubora wa Elimu ya Sekondari, serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa itawaruhusu wanafunzi ambao ni wajawazito au waliojifungua kujiandikisha katika program ya maalumu ya elimu iliyotambuliwa kama “njia mbadala wa elimu”. Hata hivyo, vituo hivi havifikiki kirahisi kutokana na umbali mrefu ambao unamlazimu mwanafunzi kusafiri kuvifikia na kwa kuwa kuna gharama wanatoza tofauti na shule za umma za msingi na sekondari ambazo hazina ada.

Wakati wa uandishi wa ripoti hii, serikali ilikuwa bado haijafuta ndoa za utotoni, kumaanisha mamlaka zilikuwa bado hazijatekeleza hukumu ya 2016 ya Mahakama Kuu ya kurekebisha Sheria ya Ndoa na kuongeza umri halali wa ndoa kuwa miaka 18 kwa wasichana na wavulana.