Skip to main content

Kenya

Matukio ya 2017

Wakazi wa Mathare, Nairobi, watoroka huku polisi wakifukuza waandamanaji wa upinzani, tarehe 12 Agosti.

© 2017 Thomas Mukoya/Reuters

Mnamo Agosti 8, Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya ilimtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa Uchaguzi wa Urais kwa muhula wa pili, wakati upinzani pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yakiyatilia shauku matokeo hayo yakidai udanganyifu na wizi wa kura. Uchaguzi huo pia ulikumbwa na shutma za matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa vyombo vya dola ambayo yaliwalenga waakazi, haswa katika ngome za upinzani jijini Nairobi, na maeneo ya Pwani na Magharibi mwa Kenya.

Mnamo tarehe 1 Septemba, Mahakama ya Upeo ilifutilia mbali matokeo ya uchaguzi huo baada ya Mgombea wa Muungano wa National Super Aliance (NASA), Raila Odinga kuwasilisha kesi katika mahakama hiyo kupinga matokeo hayo.

Kufuatia uamuzi huo, chama tawala cha Jubilee kilijibu kwa kutoa vitisho na kuwasuta majaji wa Mahakama hio ya Upeo., Pamoja na hayo, chama hicho kilianzisha juhudi za kuzifanyia mageuzo sheria za uchaguzi kwa jitihada za kudhoofisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya wanaowajibika kwa makosa ya uchaguzi.

Uchaguzi mpya ulifanyika mnamo Oktoba 26, huku Raila Odinga akiwa amejiondoa katika kinyang’anyiro hicho siku chache kabla. Uhuru alitangazwa mshindi, na Mahakama ya Upeo ikatupilia mbali kesi zote zilizokuwa zimewasilishwa kupinga kutangazwa kwa ushindi wa Kenyatta.

Kutowajibishwa kwa makosa ya ukatili na unyanyasaji uliofanyika wakati wa machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 -2008 nchini (PEV) bado unaendelea, baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutupilia mbali kesi zilizokuwa zimewashilishwa dhidi ya Kenyatta, naibu wake William Ruto, na wengine wanne.

Serikali bado haijabuni ratiba ya mpango wa kuwafidia wale wote ambao waliathirika na ghasia za kisiasa ambao iliahidi kubuni mnamo mwaka 2015 kuwasaidia waathirika wa machafuko hayo ya baada ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2007 -2008. Ingawa imechukua hatua za kuwasaidia baadhi ya waathirika wa vurugu hizo za kisiasa za 2007 kama vile waakimbizi wandani kwa ndani waliopoteza makao yao (IDPs), serikali haijawasaidia waathiriwa wa visa vya ubakaji ambao bado wanahitaji matibabu na msaada wa kifedha.

Washukiwa watatu wanaotakikana kufika mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai tangu mwaka 2013 na 2015 kwa tuhma za kuvuruga mashahidi katika mojawepo ya kesi bado hawajakamatwa na kukabidhiwa Kortini na serikali. Kesi zimewasilishwa katika Mahakama nchini Kenya kupinga vibali vya kukamatwa au kusalimishwa kwa watatu hao.

Kupungua kwa viwango vya maji katika Ziwa Turkana nchini Kenya baada ya kujengwa kwa mabwawa na upanzi katika mashamba kwenyeeneo la bonde la Omo nchini Ethiopia kunahatarisha maisha ya watu takriban nusu milioni nchini Ethiopia na Kenya.

Ukatili wa Vikosi vya Usalama Dhidi ya Raia

Mashirika yasio ya kiserikali ya kitaifa na kimataifa ya kutetea haki za kibinadamu yalikusanya takwimu zinazoonyesha visa kadha vya ukiukwaji wa haki na ukatili unaotekelezwa na vikosi vya usalama katika oparesheni za kijeshi na za kudumisha sheria kati ya mwaka 2016 na 2017 nchini kote. Katika Kaunti ya Laikipia iliyoko katika Bonde la Ufa, ambapo wafugaji wanaotafuta malisho kwa ajili ya mifugo wao wanakinzana na wamiliki binafsi wa mashamba makubwa , Shirika la Human Rights Watch lilibaini kuwa mnamo Juni mwaka wa 2017 kuwa maafisa wa Polisi na Wanajeshi walituhumiwa kuwa waliwapiga na kuwaua wafugaji hao kutoka jamii wa Pokot na mifugo yao.

Mauaji yaliyotekelezwa na maafisa wa Polisi katika mitaa ya mabanda ya Mathare na makaazi mengine ya mabanda kama vile Dandora, Kayole, Huruma, Eastleigh, Kibera, na Kariobangi hayakuchunguzwa hadi wa leo. Mnamo mwezi Mei 2017, ripoti ya shirika moja la kutetea haki za kibinadamu la Mathare Social Justice Centre, ilionyesha kuwa kati ya mwaka 2016 na 2017, maafisa wa polisi waliwaua kiholela angalau vijana 57 wakike na wakiume.

Vikosi vya Usalama vya Kenya pia vimetuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, yakiwemo mauaji ya kiholela, kutoweka kwa wale wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na kundi la wapiganaji waliojihami wa Al-Shabab walio na ngome yao nchini Somalia, na shughuli za polisi zenye ukatili ambazo zinawalenga zaidi jamii ya Wasomali wenye asili ya Kenya na wale wasio toka Kenya na Waislamu kwa jumla. Katika barua kwa Rais Uhuru Kenyatta mnamo Desemba 2016, mashirika ya haki za kibinadamu ya Kitaifa na yale ya Kimataifa, likiwemo Shirika la Human Rights Watch, yalihoji kuwepo kwa haja ya kubuniwa kwa tume ya kuchunguza mauaji haya na kutoweka kwa washukiwa. Hadi sasa Rais hajaitikia mwito huu na hakuna hatua iliyochukuliwa.

Ukatili wa Vikosi vya Usalama Wakati wa Uchaguzi Mkuu

Uchaguzi wa Mwezi Agosti na ule wa Mwezi Oktoba 2017 ulishuhudia visa kadha vya ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu. Mwanzoni mwa Mwezi Agosti, Meneja wa kitengo cha Teknolojia katika Tume ya Uchaguzi, Chris Musando, alitekwa nyara na mwili wake ukapatikana siku mbili baadaye katika kitongoji cha jiji la Nairobi. Muungano wa Upinzani, NASA, ulitaja mauaji hayo kuwa yenye lengo la kuvuruga mfumo wa teknolojia ilikuwemp wa kupiga , kuhesabu na kutangaza matokeo ya kura.

Katika kipindi kabla na baada ya Uchaguzi wa Mwezi wa nane , Polisi na vikosi vingine vya usalama vilitumia nguvu kupita kiasi kuwakabili waandamanaji, hasa katika ngome za Upinzani. Maandamano hayo yalizuka baada ya madai ya Raila Odinga kuwa kura za uchaguzi wa Agosti 2017 zilikuwa zimeibiwa.

Polisi pia walifanya oparesheni ya nyumba kwa nyumba, wakiwapiga na kuwafyatulia risasi watu wa kiume, japo pia waliwapiga wakike walipokataa kuwaelezea walipokuwa wamejificha washukiwa wakiume walioshiriki katika maandamano. Inakisiwa kuwa angalau watu 67 walipigwa risasi au kupigwa hadi kufariki kote nchini, mamia zaidi walijeruhiwa wakati wa operesheni hizi.

Kulikuwa na ripoti za kusikitisha za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia wakati wa operesheni za polisi huko Kisumu na Nairobi. Wakati wa kuchapisha ripoti hii, Halmashauri inayoangazia utendakazi wa Polisi; Independent Policing Oversight Authority (IPOA) ilikuwa imeanzisha uchunguzi wa visa sita vya mauaji pekee kati ya visa vyote viilivyoripitiwa.

Uhuru wa Kujieleza na Ule wa Vyombo vya Habari

Kwa miaka mitano iliyopita, mamlaka nchini Kenya imetumia hatua za kisheria, utawala, na zisizo rasmi za kuzuia utendakazi wa vyombo vya habari. Katika kipindi cha kabla ya Uchaguzi wa 2017, waandishi wa habari ,na wanablogu wanalio ripoti kuhusu masuala tata kama vile ardhi, rushwa, na usalama walikabiliwa na vitisho, kutishiwa, kukamatwa kiholela, na kushambuliwa. Angalau waandishi wawili walikamatwa kabla na baada ya uchaguzi wa Agosti. Mnamo Juni 18, maafisa wa polisi walimkamata mwandishi wa habari wa gazeti la Daily Nation Walter Menya na kumuachilia bila kumfungulia mashtaka baada ya siku mbili. Polisi walidai kuwa Menya alidai kupewa rushwa. Shirika la Nation Media Group lilimtetea kwa kusema kuwa alikuwa akilengwa kwa kuripoti kuhusu jinsi maafisa wa serikali walivyokiuka sheria za Kampeini za Uchaguzi bila kutokujali.

Mnamo Agosti 12, polisi waliwakamata waandishi wa habari za Televisheni, Duncan Khaemba, na Otieno Willis, ambao walishukiwa kimakosa kuwa wamevaa magwanda ya kuzuia risasi bila kuwa na vibali.

Kukamatwa kwao kunakisiwa kuwa kulilenga kuwazuia kutekeleza wajibu wao wa kuyafichua ukatilia wa Polisi dhidi ya raia.Mnamo mwezi Mei, Shirika la Human Rights Watch, lilirekodi angalau visa 50 vya waandishi wa habari na wanablogu ambao walikabiliwa na dhulma katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kote nchini Kenya, ikiwemo kupigwa na kutishwa. Angalau waandishi wawili waliripotiwa kuuliwa na watu wasiojulikana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Katika visa vingine vilivyoripotiwa, mamlaka nchini Kenya yaliondoa matangazo au kutolipia ada ya kupeperushwa kwa matangazo yake ili kushinikiza vyombo vya habari vya kibinafsi kutochapisha ripoti za kuishutumu serikali.

Licha ya kupokea malalamishi rasmi kutoka kwa waandishi wa habari na waandishi wa blogu, polisi hawajafuatilia mara kwa mara mashambulizi au vitisho na washukiwa hawajakamatwa au kuwajibishwa kamwe.

Vitisho Dhidi ya Mashirika Yasio ya Kiserikali

Mashirika yasio ya Kiserikali yanayohusika na masuala mbalimbali, hususan uwajibikaji, uhaini unaotekelezwa na vikosi vya usalama, na uchaguzi, yanaendelea kukabiliwa na vitisho visivyo kuwa na msingi , vikwazo, ikiwemo vya kupokonywa leseni kutoka kwa mamlaka ya kusimamia mashirika hayo.

Mnamo Desemba 2016, mamlaka nchini Kenya yalisitisha mpango wa elimu ya musuala ya upigaji wa kura kwenye mfumo wa kieletroniki, "Kenya Electoral Assistance Program, KEAP 2017”, mpango wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 20 uliofadhiliwa naUSAID, na kutekelezwa na International Foundation for Electoral Systems (IFES) na uliokusudiwa kutoa mafunza kwa raia kuhusu uchaguzi. Bodi ya kuyasimamia mashirika yasiyo ya kiserikali ilidai kuwa shirika la IFES halikuwa limesajiliwa rasmi. IFES ilikanusha madai haya, lakini ikasitisha utekelezaji wa mpango huo. Mnamo Agosti 14, bodi ya kuyasimamia mashirika yasiyo ya kiserikali ilitangaza kuipokonya leseni Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya; Kenya Human Rights Commission (KHRC) - mojawapo wa Tume anzilishi za kutetea haki za kibinadamu katika taifa hili.

Ilikisiwa kuwa bodi hiyo iliafikia uamuzi huo baada ya kubaini kwamba tume hiyo ilikwepa kulipa ushuru. Tume hiyo pia ilikosolewa kwa kuwaajiri wataalamu bila vyeti halisi na pia kuficha kile ambacho bodi hiyo ilisema ni marupurupu haramu kwa makamishna wa bodi ya tume hiyo. Hata hivyo kaimu waziri wa Masuala ya Usalama wa Taifa, alisitisha utekelezwaji wa uamuzi wa bodi hio

Mnamo Agosti 16, maafisa wa polisi na wale wa Halmashauri ya Mapato ya Kenya; Kenya Revenue Authority (KRA) walizuru ofisi za shirika lingine lisilo la kiserikali AfriCOG, ambalo linajihusisha na masuala ya utawala bora na ambalo lilikuwa limewasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2013 ambao Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi. Mawakili wa AfriCOG waliwazuia maafisa hao kuingia katika ofisi hizo.

Mnamo Novemba, bodi inayosimamia mashirika yasiyo ya kiserikali ilizitaka na kuziamuru mashirika ya Inuka Kenya, Taasisi ya Katiba na shirika la haki za Binadamu la Waislam; Muslims for Human Rights (MUHURI), kufika mbele yake kwa tuhma kuwa mashirika hayo hayakuwa na hati za usajili sahihi. Maafisa wa mashirika haya walisema waliamini kuwa vitisho vya kufutiliwa mbali kwa usajili wao vililenga kuwazuia kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Mwezi Oktoba Mahakamani.

Haki za Wakimbizi

Mwezi Februari, Mahakama Kuu ya Kenya ilisimamisha amri ya serikali ya kufunga kambi ya wakimbizi ya Daadab, ambayo ni hifadhi kwa wakimbizi 240,000 wengi wao wakiwa wenye asili ya kisomalai. Idadi ya wakimbizi katika kambi hii imepungua kwa kiwango kikubwa kutoka 465,000 walioishi huko mwaka 2011, kutokana na vitisho vya serikali vya kufunga kambi hiyo na kupunguzwa kwa huduma na mgao wa chakula na Shirika la masuala ya wakimbizi la Umoja wa Mataifa- UNHCR.

Yapata wakimbizi 32,000 walirudi Somalia mnamo 2017. Serikali ya Kenya ilitangaza mwezi Mei 2016 kwamba itafunga kambi hiyo na kuwarejesha makwao kwa nguvu wakimbizi kutoka Somali, wakiwashtumu wakimbizi hao kwa kuwapa hifadhi magaidi. Ilivunjilia mbali Idara ya Wakimbizi, ambayo ilikuwa ikihusika na usajili wa wakimbizi wapya.

Mwezi Januari , mwanasheria wa haki za binadamu, Samuel Dong Luak, na mwenzake, Aggrey Idris, walitekwa nyara na watu wasiojulikana jijini Nairobi na inadaiwa kuwa walirejeshwa kwa nguvu nchini Sudan Kusini ambapo walikuwa katika hatari ya kuteswa na kudhulumiwa.

Serikali ya Kenya ilishindwa kuzuia au hata kuvichunguza visa hivi na vinginevyo vya aina hii vya kurejeshwa nchini Sudan Kusini kwa wakimbizi na watetezi wa haki za kibinadamu nchini humo waliokuwa wamekimbilia hifadhi nchini Kenya.

Muelekeo wa Kimapenzi na Utambulisho wa Jinsia

Kesi za Kikatiba zilizowasilishwa Mahakamani kuhusu sheria za Kenya zinazo haramisha mapenzi ya jinsia moja na matumizi ya kufanyiwa uchunguzi wa lazima katika sehemu nyeti ya nyuma baado hazijaamuliwa. Shirika la Madaktari la Kenya limeshtumu kufanyiwa uchunguzi huo kwa washukiwa. Mwanasheiria Mkuu nchini Kenya alibuni jopo mnamo Mei 2017 kuangalia upya marekebisho katika sera kuhusu watu ambao jinsia yao haijatambulika kisheria.

Watumishi Muhimu wa Kimataifa

Kenya baado inaendelea kushikilia nafasi muhimu katika ukanda huu katika jitihada za kukabiliana na Ugaidi ambazo zinaungwa mkono na Marekani, Uingereza na Muungano wa jumuia ya Ulaya, pamoja na Umoja wa Mataifa. Kenya inachangia wanajeshi wake kujiunga na kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda Amani huko Sudan Kusini (UNMISS). Mnamo Novemba 2016, Umoja wa Mataifa ulimfuta kazi Kamanda wa Kikosi cha Kenya huko Sudan Kusini (UNMISS), hatua ambayo iliisababisha Kenya kuyaondoa majeshi yake yote nchini humo.

Mnamo Januari 2017, Kenya ilikubali kuyarejesha tena majeshi yake baada ya mazungumzo baina ya Rais Kenyatta na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres huko Addis Ababa, Ethiopia.

Jumuiya ya Kimataifa ilitumia rasilimali nyingi kufuatilia Uchaguzi wa Agosti 2017 na kutathmini uwezekano wa kuzuka ghasia na ukiukwaji wa haki za kibinadamu. Umoja wa Afrika, Muungano wa jumuiya ya Ulaya, Muungano wa nchi za Madola (Commonwealth), na mashirika mawili ya Marekani, Taasisi ya Taifa ya Kidemokrasia (National Democratic Institute NDI), na The Carter Cente walituma wajumbe kuufuatilia Uchaguzi huo wa Agosti, ambao waliwapunguza waangalizi wao kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha Uchaguzi mpya wa Oktoba 26.

Waangalizi wa Kimataifa kwa ujumla walikuwa makini sana katika kuuhalalisha uchanguzi wa Oktoba 26 kuliko walivyokuwa wakati wa uchaguzi wa Agosti 8, na , pia hawakutuma pongezi kwa Kenyatta kwa ushindi huo.

Licha ya dukuduku kutolewa kuhusu uwazi na usimamizi wa uchaguzi huo ulivyoendeshwa, Ubalozi wa Uingereza na Marekani nchini Kenya ulihimiza upinzani kukubali kushindwa na pia kukubali matokeo hayo. Afisi ya Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Haki za Binadamu iliwatuma wajumbe wa kufuatilia masuala haya katika sehemu kadhaa nchini Kenya katika uchaguzi wa Agosti na Ule wa Mwezi Oktoba, na kuvihimiza vikosi vya Usalama kutotumia nguvu wanapokabiliana na raia au waandamanaji.