Kimeandikwa na Juliane Kippenberg na Jane Cohen
Kila mwaka, mamilioni ya watu kote ulimwenguni huathiriwa kutokana na hali mbaya mno ya mazingira. Athari hizi ni kwa namna ya magonjwa, vifo vingi na hata wengine hupoteza njia zao za kuchuma riziki.
Mara nyingi uharibifu wa mazingira ukiangaziwa katika kiwango cha kimataifa, athari wake huangaliwa kuhusu maumbile tu.
Kingine ni kuwa athari za umwagaji wa sumu ama chemikali katika mazingira kiholela na janga litokanalo na uchimbaji wa madini hupuuzwa. Athari hizi ni kwa haki za binadamu kama vile haki ya uhai, ile ya kupata chakula na maji safi.
Kwa mfano, katika mkoa wa Henan, mashariki mwa Uchina katika mwaka wa 2011, maji katika mito yalikuwa mekundu kama damu kutokana na uchafu na moshi mwingi uliotanda angani karibu na viwanda vya kuyeyusha risasi (lead) na kutengeneza betri. Ingawa uchumi wa eneo hili unategemea viwanda hivi kwa kiwango kikubwa, hali hii husababisha wasiwasi mwingi kuhusu uchafuzi wa mazingira.
Ripoti ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ya mwaka wa 2011 – “My Children Have Been Poisoned” ilionyesha kwamba hali ya afya katika Henan na hali mbaya ya mazingira vilevile imesababisha ukiukaji wa haki za binadamu na kuwanyima raia wa Henan haki nyingi za binadamu zinazotambuliwa kimataifa kama vile haki ya afya, ya kupinga kitu kwa njia ya amani na hali hii imetatiza ukuaji kimwili na kiakili wa maelfu ya watoto.
Kwa bahati mbaya, serikali na mashirika ya kimataifa mara nyingi hayachanganui vilivyo maswala ya mazingira kwa kuzingatia au kujumuisha haki za binadamu wala hazijumuishi maswala ya mazingira pamoja na ya haki za binadamu katika sheria au taasisi mbalimbali. Lakini mashirika haya na serikali inapaswa kufanya hivyo bila kuhofia kuwa kufanya hivi kutatatiza maendeleo na ulinzi wa mazingira
Kusema kweli, kujumuisha haki za binadamu hakutatiza malengo haya mawili badala yake kutaimarisha uwajibikaji wa serikali katika majukumu yake. Hatua hii pia itawapa waathiriwa njia au vyombo vya kutetea haki zao pamoja na kupinga uharibifu wa mazingira. Watataka wasikilizwe, washiriki kikamilifu katika mijadala ya umma yanayohusu changamoto katika mazingira na watumie korti huru panapohitajika kutimiza uwajibikaji na kupata fidia kulingana na usemi mkongwe wa kisheria, hakuna haki bila fidia.
Vyombo vinavyotetea haki za binadamu kama Hati Ya Ziada Kwa Mkataba Juu Ya Haki Za Binadamu Kuhusu Haki Za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (Addition Protocol to the American Convention on Human Rights in the Area of Economic, Social and Cultural Rights), Mkataba Wa Kiafrika Juu Ya Haki Za Binadamu na Haki za Watu (the African Charter on Human and Peoples’ Rights) na Hati Ya Ziada Juu Ya Haki Za Wanawake (Additional Protocol on the Rights of Women) – vinatambua haki ya mazingira yenye afya (ama mazingira yanayofaa kulingana na Mkataba Wa Kiafrika-African Charter iliyoanza kutumiwa katika mwaka wa 1981).
Pia ni zaidi ya miongo miwili toka azimio lililofanywa katika Mkutano Mkuu Wa Umoja Wa Mataifa (United Nations General Assembly) litambuliwe. Azimio hili linasema kuwa kila mtu ana haki ya kuishi kwenye mazingira yanayofaa kwa afya na maslahi yake.
Katika mwaka wa 2001 Tume ya Kiafrika Juu Ya Haki Za Binadamu Na Watu (African Commission on Human & Peoples’ Rights) ilifanya uamuzi uliofungua ukurasa mpya katika haki za binadamu. Uamuzi wenyewe ulidhihirisha kuwa uwajibikaji kwa kukiuka haki za binadamu pamoja na haki ya mazingira yenye afya unawezekana. Tume ilipata kuwa, serikali ya kijeshi ya Nigeria kwa ushirikiano na kampuni ya mafuta ya Shell zilisababisha uharibifu wa mazingira kwa kabila la Ogoni wanaoishi katika eneo la Niger Delta.
Tume iligundua kuwa serikali ilikiuka haki inayolindwa na Mkataba Wa Kiafrika (Africa Charter) kwa kutochukua hatua zilizofaa ili kulilinda kabila la Ogoni dhidi ya madhara kutokana na uzalishaji wa mafuta. Serikali pia haikutoa ripoti wala kuruhusu utafiti ufanywe juu ya hatari za kiafya zilizoweza kutokea au zile halisi ama za kweli zilizosababishwa na shughuli za mafuta miongoni mwa wanajamii wa Ogoni.
La kushangaza vilevile ni kuwa tume pia ilipata kwamba haki ya kuishi ilikiukwa kwa viwango vya juu kupita kiasi, uchafu na uharibifu wa mazingira ambayo kwa pamoja uliharibu ardhi na mashamba yaliyotegemewa na kabila la Ogoni kuendelea kuishi.
Licha ya maamuzi kama haya, serikali ama mashirika bado hayawajibiki vilivyo katika maswala ya haki za binadamu na mazingira jambo ambalo linadhihirishwa na idadi ya madhara kwa mazingira yanayotendeka kote duniani bila fidia.
Mashirika ya kimataifa yanayotetea haki za binadamu yanahitaji kuimarisha sheria na mfumo au utaratibu kuhusu haki ya kuishi katika mazingira yenye afya pamoja na kuweka rasmi uhusiano kati ya haki za binadamu na mazingira. Mojawapo ya hatua zinazohitajika ni kama kubuni utaratibu wa kufuata ili kuhakikisha uwajibikaji jambo linaloweza kutoa suluhisho ya kufaa kwa mamilioni walioathiriwa kutokana na uharibifu mbaya zaidi wa mazingira.
Haki ya Kuishi na ya Afya
Chini ya sheria ya kimataifa kuhusu Haki za Binadamu, serikali zina wajibu mwingi katika kulinda haki za kuishi za raia yao.
Azimio La Haki Za Binadamu Kote Ulimwenguni(Universal Declaration of Human Rights), Makubaliano Ya Kimataifa Juu Ya Haki Za Kiuchumi Na Kijamii Na Kiutamaduni(International Covenant on Economic and Social and Cultural Rights-ICESCR) na Mkataba Juu Ya Haki Za Watoto (Convention on the Rights of the Child -CRC) zote zinaweka haki ya kupata hali nzuri sana ya afya iwezekanayo chini ya mkataba huu wa ICESCR. Haki hii inajumuisha wajibu wa kuboresha afya ya mazingira, kuwalinda wananchi dhidi ya hatari za kiafya katika mazingira, kuhakikisha mazingira ya kazi yenye afya na kulinda haki ya kupata chakula na maji safi.
Na serikali nyingi bado zinakosa kuheshimu na kudumisha haki hizi kila mara.
Shirika la Human Rights Watch limeandika kuhusu hali mbaya zitokanazo na kuzipuuza haki hizi na baadhi ya serikali katika maeneo mengi duniani. Katika eneo la Zamfara, kaskazini mwa Nigeria kwa mfano, zaidi ya watoto 400 wameaga dunia kutokana na sumu za risasi (lead) toka mwaka wa 2010. Hii ni mojawapo tu ya hali zile mbaya zaidi kuwahi kunukuliwa katika historia. Inatokana na mavumbi yaliyochanganyika na risasi(lead) kutokana na uchimbaji wa dhahabu kwa kiwango kidogo.
Serikali ya Nigeria ilikawia kulishughulikia swala hili la ajabu licha ya kuona au kujua fununu ya kuwepo kwake. Kwa ufupi, katika filamu, A Heavy Price (2012), shirika la Human Rights Watch limeonyesha jinsi watoto wanavyoendelea kuishi na kucheza katika makao machafu na kukumbana na risasi(lead) katika viwango vya juu vinavyohatarisha maisha yao na hata vinaweza kusababisha ulemavu maishani ikiwa sio kifo.
Kwa bahati mbaya hali katika nchi ya Nigeria sio tofauti na nchi nyingine kuwa baadhi ya serikali hukabiliana na shida za kimazingira kwa kuzikana, au kutoa majibu yasiyoridhisha pamoja kukosa mantiki kisha hukosa kusuluhisha uharibifu wa mazingira, kulazimisha au kutekeleza sheria, kuzuia au kutibu madhara ya afya yatokanayo na uharibifu ule.
Haki ya Kujua, Kupinga na Kutafuta Haki
Sheria za kimataifa pia hulazimisha serikali kuhakikisha haki ya raia ya kujua, kushiriki katika shughuli za kisiasa, kupinga kwa njia ya amani, na kupata haki.
Haki hizi zinazolindwa na Makubaliano Ya Kimataifa Juu Ya Haki Za Raia Na Kisiasa (International Covenant on Civil and Political Rights-ICCPR) inahakikisha kuwa raia wanashiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maisha yao.
Katika hali halisi, baadhi ya serikali mara nyingi hukosa kuwaelezea wananchi wake kuhusu mambo muhimu juu ya afya katika mazingira hivyo basi hukiuka haki yao ya kujua. Kwa mfano kule Japan, serikali ilikosa kuwapa wakazi wa wilaya ya Fukushima habari muhimu juu ya viwango vya mnunurisho (radiation) katika chakula na mazingira baada ya wilaya hii kukumbwa na msiba wa kinuklia mnamo Machi mwaka wa 2011 hali iliyowafanya waandishi wa habari wa eneo hili kukiamini chochote walichoambiwa bila ushahidi wowote. Shirika la Human Rights Watch lilipokea habari hii kutoka kwa daktari mmoja.
Na hata katika nchi zile zinazo mipango madhubuti ya kuhakikisha uwazi na kushiriki kwa watu husika, ukweli mara nyingi si ya kutamanisha wala kutia moyo. Serikali katika nchi nyingi pamoja na kukosa kutoa habari kwa raia wao, vilevile zinawakandamiza wanaodai uwazi na fidia kirasmi.
Shirika la Human Rights Watch limerekodi hatua mbalimbali za serikali dhidi ya wanaopinga na hata wale wanaotaka tu habari kama vile vitisho, kukamatwa, kufungwa jela na hata kuuawa.
Utafiti wetu wa mwaka wa 2011 katika mikoa minne kule Uchina, kwa mfano, ulibainisha kuwa serikali iliwazuilia waliopinga uchafuzi kutokana na risasi(lead) kutoka kwenye viwanda na hata wazazi waliowatafutia wanao matibabu pia walizuiliwa. (My Children Have Been Poisoned).
Katika nchi ya Ufilipino vilevile shirika la Human Rights Watch limeandika kuhusu kuuawa kwa wanaharakati watatu wa mazingira tangu mwaka wa 2011. Wanaume hawa waliupinga vikali uchimbaji wa madini na shughuli za kawi ambazo walisema zilihatarisha mazingira na baadaye zingaliwalazimu wenyeji wa mikoa ya Bukidnon no Cotabato kaskazini kuhama.
Mpaka sasa, hakuna yeyote aliyeadhibiwa na ushahidi unadokezea kuhusika kwa vikosi vingine chini ya usimamizi wa wanajeshi.
Nayo nchi ya Kenya katika mwaka wa 2010 iliweka katika katiba yake haki ya kuishi katika mazingira yenye afya, shirika la Human Rights Watch limekuwa likifanya kazi na mwanaharakati wa mazingira ambaye ametishiwa maisha zaidi ya mara moja na hata kukamatwa kwa kutafuta habari na fidia kutoka kwenye kiwanda kimoja ambacho kimechafua hewa na maji karibu na jiji la Mombasa.
Kusimamia Biashara
Leo hii biashara ndizo zinachangia zaidi shida katika mazingira. Hata kama ni zile za kimataifa, za kitaifa au zile ndogo, zote zina jukumu la kuhakikisha kuwa oparesheni zao hazisababishi wala hazichangii ukiukaji wa haki za binadamu. Kauli hii inapatikana katika Kanuni Za Umoja Wa Mataifa Ya Kuongoza Biashara Na Haki Za Binadamu
(U.N Guiding Principles on Business and Human Rights). Jukumu hili mara nyingi linakosa kutimizwa. Unaweza pia kusoma makala “Without Rules: A Failed Approach to Corporate Accountability” katika juzuu hii.
Kwa mfano katika migodi ya Porgera kule Barrick Gold katika nchi ya Papua New Guinea, tani 14,000 za majitaka humwagwa kila siku kwenye mto mmoja hatua iwezayo kusababisha uharibifu wa mazingira na hali mbaya ya afya kwa wakazi. Unaweza kusoma makala ya,Gold’s Costly Dividend, 2011kwa mengi.
Katika Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh, kampuni kama 150 za ngozi huhatarisha maisha ya wenyeji kwa maji machafu kutoka kwenye viwanda. Maji haya yana chemikali kama salfa, kromiamu na ammonia na nyingine zinazosababisha magonjwa ya ngozi, vipele na kuhara miongoni mwa matatizo mengine ya kiafya (Toxic Tanneries, 2012).
Kampuni pamoja na wawekezaji wa kigeni, wanunuzi wa kimataifa, wauzaji wa rejareja wana jukumu la kuhakikisha kuwa hawachangii moja kwa moja ukiukaji wa haki za binadamu.
Muuzaji wa mshipi uliotengenezwa kutokana na ngozi iliyotibiwa na kukaushwa kwa asidi katika jiji la Dhaka anapaswa kuwa mwangalifu katika utaratibu wake ili ahakikishe kuwa hachangii ukiukaji wa haki za binadamu hata kama si moja kwa moja aidha wanunuzi wa kimataifa wahakikishe kuwa wagawaji wao hawakiuki sheria za usalama na afya pia hawamwagi sumu wala hawatupi taka zozote ovyo katika mazingira.
Serikali nazo zinapaswa kuidhibiti vilivyo sekta ya kibinafsi jambo ambalo mara nyingi baadhi ya serikali zinasitasita kulitekeleza maanake sheria kuhusu uhifadhi wa mazingira zinaingilia maslaha ya sekta hii (ya kibinafsi) na inachukuliwa kuwa hatua kama hii inarudisha nyuma maendeleo na ukuaji kiuchumi.
Aidha katika nchi ya Kanada katika mwaka wa 2010, bunge liliutupilia mbali mswada ambao ungeiruhusu serikali kufuatilia athari kwa mazingira na haki za binadamu shughuli za viwanda kutoka nchini humo vinavyochimba madini kote ulimwenguni.
Kwa kufanya hivi, nafasi nzuri ilipotezwa kwa kuwa kampuni nyingi za utafutaji na uchimbaji madini zinatoka Kanada.
Sekta hii ilichangia asilimia 21 ya bidhaa nje za nchi hii pamoja na kuingiza dola ya Marekani bilioni 36 kutokana na uchimbaji wa madini vile vile katika mwaka ule.
Kule Bangladesh ambako viwanda vya ngozi vinachafua hewa, maji na udongo, utafiti wetu uligundua kuwa serikali ilikosa kuzitekeleza sheria kuhusu mazingira na ajira, isitoshe, imepuuza kwa mwongo mmoja uamuzi wa korti ulioiamuru ihakikishe kuwa viwanda vya ngozi vimeweka vifaa vya vya kutosha vya kusimamia takataka.
Afisa mmoja wa serikali aliliambia shirika la Human Rights Watch kuwa sekta ya viwanda vya ngozi havisimamiwi ipasavyo kwa sababu wenyewe ni matajiri sana pamoja na kuwa wanasiasa wenye nguvu nyingi.
Na katika nchi ya India kwa mfano, uchunguzi uliofanywa na Human Rights Watch katika mwaka wa 2012 kwenye majimbo ya kusini kama Goa na Karnataka (Out of Control), ulibaini kuwa uchunguzi uliofanywa awali na ambao ulifikiriwa kuwa huru na wa kweli kuhusu jinsi miradi ya uchimbaji wa madini ungaliathiri mazingira, mara nyingi ulikuwa na dosari au upungufu fulani pia uliidhinishwa na kampuni zinazochimba madini ambazo zilitaka au zilitafuta kibali au leseni kutoka kwa serikali ya India ili zianze shughuli zao za uchimbaji.
Ufisadi vilevile wakati mwingine hutatiza udhibiti na ulinzi wa mazingira. Human Rights Watch limeonyesha jinsi sera juu ya ukataji wa miti umetatizwa na ufisadi unaoendeshwa hadharani (Wild Money, 2009) hivyo basi mbao nyingi hukatwa kule kinyume na sheria, na kukiuka sera zilizotarajiwa kuwalinda wenyeji pamoja na mazingira.
Walioathirika Kabisa
Uharibifu wa mazingira huwaathiri mno wanyonge na wanaobaguliwa kama watu maskini wanaoishi vijijini, waliohamishwa, wanawake, makabila yenye watu wachache na wenyeji ambao ni nadra kwao kupata nafasi au ushawishi mkubwa wa kisiasa wa kuweza kuikosoa ama kuiwajibisha serikali.
Haki za wenyeji zinaweza kukiukwa kwa kiwango kikubwa iwapo serikali au kampuni kubwa za kimataifa zitanyakua ardhi zao kwa kujifanya kuwa zinaleta au zinafanya maendeleo ya kiuchumi. Kulingana na Azimio La Umoja Wa Mataifa Juu Ya Haki Za Wenyeji(UN Declaration on The Rights of Indigenous Peoples), wenyeji ama wazawa wanaweza tu kuhamishwa kwa hiari yao, kama wamefahamishwa ipasavyo tena mapema na baada ya kulipwa fidia ya kutosha kwa ajili ya ardhi zao, mali nyingine na kazi zao. Na kama shirika la Human Rights Watch lilivyobainisha, njia hii haifuatwi aghalabu.
Katika nchi ya Uhabeshi vilevile, utafiti wa shirika la Human Rights Watch la 2011 liligundua kwamba wenyeji walihamishwa kwa nguvu kutoka Bonde la Omo ambalo lilikuwa njia yao ya kimsingi ya kuchuma riziki kwa ajili ya kupata nafasi ya mashamba makubwa makubwa ya miwa. Serikali imetumia usumbufu, fujo na kuwakamata kiholela ili kuilazimisha mipango yake kwao na kuwaacha wenyeji wa eneo hili pamoja na mwanamume mmoja kutoka kabila la Mursi kustaajabu na kusema “Ni nini kitakachotokea baa la njaa likizuka” mto ukikauka na ardhi pia imechukuliwa? (What Will Happen If Hunger Comes? 2012).
Kikundi kingine kinachoweza kuathiriwa na madhara yatokanayo na uchafuzi wa mazingira ni watoto ingawa ulinzi wa afya ya watoto ni wajibu muhimu katika sheria ya kimataifa. Chemikali zenye sumu zina madhara makali kwa watoto ambao mwili wao inayokua huingiza sumu zile kwa urahisi kuliko miili ya watu wazima na kusababisha madhara yatakayodumu kwa muda mrefu au hata milele, ulemavu ama kifo.
Watoto kutoka jamii maskini, wasiobahatika ama waliotengwa haswa wanaweza kuwa katika hali ya hatari kubwa kwa kuwa familia zao hazina ushawishi wa kisiasa wala habari.
Shirika hili la Human Rights Watch katika utafiti wake juu ya ajira kwa watoto kwenye migodi ya dhahabu katika eneo la Mail limebaini kuwa watoto kuingiliana na zebaki ambayo ni chuma chenye sumu ni swala ambalo halijashugulikiwa katika kiwango cha kitaifa wala kimataifa (A Poisonous Mix 2011). Wachimbaji wa dhahabu katika eneo hili ni miongoni mwa wachimbaji karibu milioni 15 ambao huchimba kwa matumizi au ufundi wao mdogo.
Shirika hili la Human Rights Watch vilevile limeandika kuhusu jinsi watoto na watu wazima kutoka jamii ya Roma ambao wametengwa tena ni wachache walihamishwa baada ya vita vya mwaka wa 1999 kule Kosovo na kupewa makao kwa miaka kwenye kambi chafu ya wakimbizi. Kambi hii ilichafuliwa na risasi kule Kosovo Kaskazini. (Kosovo: Poisoned by Lead, 2009).
Watoto haswa walidhuriwa kwa urahisi kwa sumu za risasi. Umoja wa Mataifa ulijua kuhusu hali hii bali halikuwahamisha hadi pahali salama kwa muda wa zaidi ya miaka mitano. Lilikosa mpangilio imara ya afya pia ilisitisha matibabu kwa watoto bila sababu zozote za kiafya.
Watoto katika nchi tajiri pia wanaweza kuathiriwa na mazingira yenye sumu. Marekani, kwa mfano katika sekta ya kilimo, watoto wanaajiriwa na wengi wao wanatoka katika jamii za wale wasio wenye asili ya Marekani.
Watoto hawa wanafanya katika mashamba yanayonyunyiziwa mara nyingi dawa za kuwaua wadudu.
Na serikali ya Marekani bado haijapiga marufuku ajira hatari ya watoto katika mashamba na badala yake imeipa kipaumbele maslahi ya kilimo biashara kuliko sheria kali dhidi ya utumiaji wa kiuadudu kwenye mashamba yale.
Changamoto na Nafasi Nzuri Zilizopo Duniani Kote.
Hatua za serikali dhidi ya uharibifu wa mazingira mara nyingi zina upungufu kwa vile haziambatani na hali mbaya itokanayo na mabadiliki katika hali ya hewa, uchafuzi wa mazingira na matatizo mengine ya kimazingira kuhusu haki za binadamu.
Katika mwezi wa sita mwaka wa 2012, mkutano unaoitwa Rio + 20 uliwaleta pamoja zaidi ya marais na viongozi mbalimbali wa serikali 100 na jumla ya watu 45,000 katika mkutano mkubwa zaidi kuwahi kufanywa na umoja wa mataifa.
Hata hivyo ukubwa wa mkutano huu ulizidi mno matokeo yake. Viongozi wale wa dunia walikosa fursa ya kuziba pengo ulioko kati ya maendeleo na uhifadhi wa mazingira hata walikaribia kuondoa kabisa mambo ya haki katika hati ya mwisho kwa mfano katika makala yafuatayo, “The Future We Want”.
Sheria na utaratibu za kimataifa ni vyombo muhimu vya kulinda mazingira lakini zinaegemea zaidi maswala ya kiufundi, utoaji wa uchafu, na utaratibu kama makubaliano ya Stockholm ya mwaka wa 2004 juu ya Vichafuzi vya Kiogani Visivyokoma (Convention On Persistent Organic Pollutanta) mara nyingi yanakosa kushughulikia vilivyo au yanakosa kabisa kuyashughulikia athari kwa afya na haki za binadamu zitokanazo na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande mwingine mashirika ya fedha ya kimataifa yakilenga kuboresha maendeleo, hatua zao wakati mwingine hukiuka haki za binadamu na huchangia uharibifu zaidi wa mazingira. Sera za Benki ya Dunia juu ya uhifadhi, zinazonuia kuzuia uharibifu wa kijamii na kimazingira katika miradi yake inahitaji serikali zichanganue athari za miradi fulani kwa mazingira bali hazihitaji uchanganuzi kamili juu ya athari kwa haki za binadamu.
Kwa Benki Ya Dunia kuziandika upya sera hizi kwa njia ya kisasa itakuwa nafasi muhimu ya kuurekebisha upungufu huu.
Lakini habari zote si mbovu
Mashirika yasiyo ya serikali, mashirika mengine ya umma, na jamii za waathiriwa yameleta mafanikio kiasi katika juhudi zao za kutetea uwajibikaji. Kule Burma, maandamano ya wazi yaliyofanywa na mashirika ya umma dhidi ya madhara mabaya ambayo yangalifanywa na bwawa la Myitsone katika mto wa Irawaddu yaliisukumiza serikali ya Burma katika mwaka wa 2011 na kuuhairisha utekelezaji wake. Mradi huu ungekuwa mojawapo wa vituo vikubwa zaidi duniani vya kuzalisha umeme kwa maji.
Na katika mwaka wa 2012, Baraza La Haki Za Binadamu La Umoja Wa Mataifa (UN Human Rights Council) liliteua kwa mara ya kwanza mtaalam wake huru anayeshughulikia maswala ya haki za binadamu. Baadhi ya haki zilizolengwa ni kama kuishi katika mazingira salama, safi, yenye afya kila wakati. Mojawapo ya kazi muhimu kabisa ya mtaalam yule itakuwa kusaidia kuyaainisha yaliyomo katika haki za binadamu na kuipigia debe ndani ya Baraza La Haki Ya Binadamu La Umoja Wa Mataifa na nje ili kuihakikishia heshima, ulinzi na itimizwe.
Hatua nyingine yenye manufaa na itakayosaidia ni kuwa mnamo Novemba mwaka wa 2012 nchi zilizoko Marekani Kusini ziliutayarisha mwongozo wa kuufikia mkataba wa pamoja utakaowahakikishia raia wao upataji wa habari juu ya mazingira, kushirikishwa na haki.
Mwongozo kama huu tayari upo Ulaya kwa kuwa serikali nyingi za Ulaya na Asia ya Kati zimeiidhinisha makubaliano ya Aarhus ya mwaka wa 2001 inayozuungumzia upataji wa habari, kushirikishwa kwa umma na upataji wa haki katika maswala ya mazingira.
Makubaliano haya ndiyo ya kwanza na ya kipekee kuwahi kukusanya na kutayarisha sheria kama hii inayohusu mazingira.
Vile vile kuna nafasi za baadaye zitakazotumiwa kutetea haki za binadamu katika mambo ya mazingira kama vile katika mazungumzo kuhusu mkataba wa dunia juu ya zebaki.
Shirika la Human Rights Watch limeshiriki kwenye mazungumzo haya kule Kenya na Uruguay katika miaka ya 2011 na 2012 mtawalia. Pia katika mikutano ya nchi zilizoko Kusini mwa Marekani na bara la Afrika. Katika shughuli zetu zote za kutetea haki tumehimiza kuwa maswala ya haki za binadamu zipewe kipaumbele haswa haki ya afya na ile ya kuwalinda watoto dhidi ya ajira yenye hatari.
Katika mazungumzo kule Uruguay, serikali zilikubali kujumuisha vigezo maalum katika mkataba kwa manufaa ya watoto walioathiriwa na zebaki katika migodi midogo ya dhahabu.
Tena ilikubaliwa kwamba serikali lazima zibuni mikakati ya afya kuhusu zebaki kwa jamii zilizoathiriwa kutokana na uchimbaji wa madini kwa kiwango kidogo.
Huku mkataba bado hauzungumzii haki za kibinadamu na mkakati imara ya kijumla juu ya zebaki, hatua spesheli kuhusu uchimbaji wa dhahabu ni jambo zuri.
Hatua Gani Itahitajika Siku Za Usoni
Hata kama serikali zitatekeleza sheria na ulinzi wa mazingira, mara nyingi zinapuuza athari mbaya za matatizo ya mazingira kwa haki za binadamu, pamoja na athari kupita kiasi kwa wanyonge na waliotengwa.
Kinachokosekana ni utaratibu mpana unaochanganua athari za haki za binadamu na kuzilinda haki za afya, chakula, maji na njia za kuchuma riziki ambazo ndizo haki za kimsingi kuhusu uchumi pamoja na haki za raia na za kisiasa kama vile ile ya kupata habari, kushiriki, kujieleza kwa njia ya huru na kufidiwa kwa wananchi wote. Serikali zisipowajibishwa kuna uwezekano kwamba hazitarekebisha maeneo yaliyochafuliwa au wekwa sumu pia hazitahakikisha kuwa haki imetekelezwa kwa wale ambao haki zao zilikiukwa.
Taratibu dhabiti za uwajibikaji zitakazohakikisha kuwa serikali, taasisi za fedha za kimataifa, biashara mbalimbali, washiriki wa kibinafsi ni lazima wawajibike kwa vitendo vyao kwa kuzingatia uwazi, kutoa habari kamili, kushiriki, na kujieleza kwa njia huru zinahitajika. Vigezo hivi vinahitajika kushughulikia athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira kwa haki za binadamu. Vilevile kunahitajika haja ya utaratibu kabambe wa kuwadhibiti watu au mashirika mbalimbali inayojumuisha usimamizi wa serikali ili kuzuia kufanya kazi miradi inayoharibu mazingira. Walioharibu mazingira lazima wawajibike, watengeneze upya na wachukuliwe hatua za kisheria.
Baraza La Haki ya Binadamu pamoja na serikali zile ambazo hazijatambua haki ya mazingira yenye afya zinapaswa kufanya hivyo hatua ambayo itasaidia kuimarisha uwajibikaji na kuelewa matokeo ya kukiuka haki za binadamu kupitia kwa uharibifu wa mazingira.
Mikataba ya kimataifa juu ya mazingira na malengo ya maendeleo yanayokubaliwa au tayarishwa kote ulimwenguni yanapaswa kubuniwa kwenye msingi wa sheria za kimataifa juu ya haki za binadamu na kusimamiwa kimataifa na kitaifa.
Ushirikiano kati ya mashirika ya mazingira na yale ya haki za binadamu utakuwa wenye maana sana kwa kuendeleza malengo haya kwa sababu ni kutokana na ushirikiano tu wa kitaifa na wa kimataifa ndiko maendeleo ya kukabiliana vilivyo na wanaoharibu mazingira, wanaowadhuru wengine na wale wanaozikiuka haki muhimu za binadamu yatatimizwa.
Juliane Kippenberg ni mtafiti mwandamizi katika kitengo cha Haki za Watoto naye Jane Cohen vilevile ni mtafiti katika kitengo cha Afya na Haki za Binadamu.