Skip to main content

Kenya

Matukio ya 2018

Riot police fire teargas canisters to disperse supporters of Kenyan opposition leader Raila Odinga of the National Super Alliance (NASA) coalition protesting against the treason charges on lawyer Miguna Miguna in the streets of Kisumu, Kenya February 6, 2018.

© 2018 James Keyi/Reuters

Kutokuwepo kwa uwajibikaji dhidi ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu, uliotekelezwa haswa na vikosi vya usalama, umesalia kama changamoto kubwa mwaka wa 2018. Uchaguzi wa Urais wa mwaka wa 2017 ulidhihirisha operesheni dhalimu za polisi katika ngome za upinzani. Polisi waliwapiga na kuwafyatulia risasi angalau wafuasi 100 wa upinzani pamoja na wengine wasio na hatia. Wanawake wengi na wasichana walibakwa and kudhulumiwa kimapenzi na polisi wakati wa operesheni hizo.

Mkataba wa amani wa mwezi Machi 2018 baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga, ulipunguza joto la kisiasa, lakini wakati wa chapisho hili, mamlaka husika haikuwa bado imechukuwa hatua mwafaka kuhakikisha kwamba polisi wanawajibikia vitendo vyao vya unyama.

Kenyatta amenukuliwa mara nyingi akiahidi hadharani ya kuwa ataheshimu uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari. Hatahivyo, mazingira wanayofanyia kazi wanahabari na watetezi wa haki za kibinadamu bado ni hatari. Katika mwaka wa 2017 na mwanzo wa 2018, polisi waliwatisha wanahabari na mabloga, wakawakamata na kuwatia nguvuni wanahabari, na kufunga angalau vituo vitatu vya runinga.

Unyanyasaji uliotekelezwa na vikosi vya usalama

Utafiti wa Human Rights Watch ulibaini kwamba polisi na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali walisababisha vifo vya wafuasi wa upinzani zaidi ya 100 jijini Nairobi na kule Magharibi mwa Kenya wakati wa ghasia za uchaguzi. Ijapokuwa mauwaji hayo na dhulma zingine zimenakiliwa vizuri na mashirika ya haki za kibinadamu, mamlaka husika katika serikali ya Kenya hazijafanya uchunguzi wowote.

Mnano Novemba mwaka wa 2017, Independent Policing Oversight Authority (IPOA), ambayo ni mamlaka huru ya kuchunguza maswala ya polisi, ilisema imechunguza angalau visa viwili vinavyohusiana na uchaguzi wa mwaka 2017, lakini haikufanikiwa kuwatambua wahusika wa mauaji kwa kukosa ushahidi. IPOA ilipendekeza uchunguzi wa wazi katika mauwaji ya Samantha Pendo, mtoto wa miezi sita kule Kisumu na kufidiwa kwa familia yake na ile ya Stephanie Moraa aliyekuwa na umri wa miaka 9, ambaye mashahidi walisema alifyatuliwa risasi na polisi alipokuwa amesimama nje ya nyumba yao mjini Nairobi.

Mnamo Julai, mwendesha mashtaka mkuu ya umma alimshtaki afisa wa polisi na mauwaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Meru, Evans Njoroge, baada ya uchunguzi wa IPOA. Afisa huyo alikua anasubiri kesi yake kuendelea wakati habari hii ilipochapishwa. Evans alifyatuliwa risasi tarehe 10 Machi, 2018 kwa karibu sana upande wa nyuma wa kichwa wakati wa maandamano yaliyowahusisha wanafunzi wa chuo kikuu cha Meru kule Mashariki mwa Kenya walipokuwa wakilalamikia usimamizi mbaya wa chuo hicho. Visa hivyo vya uchunguzi ni vichache kwa sababu mamlaka imeshindwa kuchunguza na kuwasilisha kesi mahakamani zinazohusiana na visa vya mauwaji yanayoendelezwa na polisi humu nchini.

Mwanzo wa mwaka wa 2018, uchunguzi uliofanywa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, ulidhihirisha kwamba askari wa kulinda misitu (Kenya Forest Service) walitumia nguvu kupindukia dhidi ya watu wa jamii ya Sengwer, jamii yenye makao yao katika mkoa wa bonde la ufa. Mamlaka iliwafurusha kwa nguvu kutoka katika msitu wa Embobut mwisho wa mwaka wa 2017 katika jitihada za kuulinda msitu wa Mau ambao ni chemichemi kuu ya maji nchini. 

Uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari

Ijapokuwa rais Uhuru Kenyatta aliahidi kulinda uhuru wa vyombo vya habari, polisi pamoja na maafisa wakuu serikalini wamewavamia na kuwatisha wanahabari wanaoandika kuhusu ‘maswala tata’ kama uchaguzi, ufisadi na usalama.

Katika kipindi cha uchaguzi wa 2017, polisi na maafisa wengine wa serikali waliwahujumu na kuwatisha wanahabari na mabloga. Mwanzo wa mwaka wa 2018, Mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya Communication Authority of Kenya walivifunga angalau vituo vitatu vya runinga- KTN, NTV, CITIZEN na Inooro- kwa kukiuka amri ya serikali ya kutopeperusha sherehe ya kumuapisha Odinga mnamo Januari 30.

Mnamo Januari 6, msemaji wa naibu wa Rais, David Mugonyi alitishia kushinikiza mwanahabari Justus Wanga wa Daily Nation kufutwa kazi kwa kuchapisha habari iliyodhihirisha mgawanyiko baina ya Kenyatta na Ruto juu ya uteuzi wa baraza la mawaziri.

Mnamo tarehe 26 Machi, vyombo vya habari nchini Kenya viliripoti kwamba maafisa wa kupambana na ghasia waliwajeruhi wanahabari wakiwemo Stephen Letoo wa Citizen TV na mpiga picha wa NTV, Robert Gichira, walipokuwa wakiripoti msukosuko ulioibuka wakati wa kumfurusha Miguna Miguna ambaye alikua wakili wa upinzani. Mmoja wa maafisa wa polisi alimzaba kofi mwanahabari wa KTN Sophia. Dennis Itumbi, ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Kenyatta alinukuliwa kwenye mtandao siku hiyo hiyo akiwapongeza polisi ‘kwa kuwa imara’ katika uwanja wa ndege.

Rais Kenyatta, mnamo Mei tarehe 16, alitia sahihi she ya uhalifu wa iliyo haramisha “habari za uongo au zisizo thibitishwa” na kuweka faini kali. Ijapokuwa mahakama kuu baadae ilihalalisha vipengee kadhaa kwa kuwa kinyume cha katiba, vipengee vingine vimeleta makosa mapya na ghadhabu kali, na kukandamiza uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari. 

Vitisho kwa watetezi wa haki za kibinadamu na wapinzani wa kisiasa

Mashirika ya Haki za Kibinadamu na watetezi wa haki za kibinadamu ambao wanaikosoa serikali, haswaa wale ambao wanahusika na maswala ya utendakazi, udhalimu wa vikosi vya usalama, na uchaguzi, wanaendelea kupokea vitisho na kuwekewa vikwazo, ikiwemo uhuru wa kujumuika. Human Rights Watch ilibaini ya kuwa kati ya Agosti 2017 na Machi 2018, polisi pamoja na maafisa wengine wa serikali waliwalenga angalau watetezi wa haki za kibinadamu 15 na waathiriwa wa visa vya udhalimu wa polisi mjini Nairobi na eneo la Magharibi katika kaunti ya Kisumu. Walikabidhiwa na hofu ya kutiwa mbaroni, kupewa onyo la kutosambaza ujumbe kwenye mtandao kuhusu udhalimu wa polisi wakati wa msimu wa uchaguzi, nyumba na ofisi zao kuvunjwa, na tarakilishi pamoja na vifaa vingine kuchukuliwa na polisi.

Mnamo Septemba, mwanaharakati mmoja aliyenakili dhulma za polisi kule Nyalenda, Kisumu alisema kuwa polisi walimuonya kupitia simu dhidi ya kusambaza picha na kanda za video za dhulma hizo na wakamshtumu kwa kuwaharibia sifa yao. Polisi walivamia ofisi yake mwezi wa kumi na kumuamrisha kusalimisha zile picha na kanda za video zilizoonyesha dhulma hizo wakati wa kipindi cha uchaguzi.

Mnamo tarehe 30, Januari mamlaka ilihalalisha na kuharamisha shughuli za vuguvugu la upinzani National Resistance Movement (NRM), ambalo lilikuwa  mmojawapo ya nguzo za muungano wa upinzani  NASA. Kuharamishwa huko kuliweka wazi ari ya serikali kuwasaka na kuwakamata wanasiasa na mawakili waliohusika katika sherehe ya kumuapisha Odinga. Serikali iliendesha harakati ya kuwakamata kiholela na kuwaweka kizimbani bila ya kuwafungulia mashtaka, na baadaye  kumfurusha mmoja wao kutoka nchini.

Mnamo Februari 2018, mamlaka ilimnyang’anya wakili wa upinzani, Miguna Miguna uraia wake wa Kenya na kumfurusha hadi  nchini Canada hatua iliokiuka amri zilizotolewa na mahakama ambazo zilimtaka Miguna arudishiwe uraia wake wa Kenya na kugeuza uamuzi wa kumfurusha nchini. Mamlaka iliwakamata na kuwashtaki wanasiasa wengine wa upinzani akiwemo Tom kajwang, Babu Owino na George Aladwa kushiriki katika mkutano usio halali na kufutilia mbali vyeti vya kusafiri vya Zaidi ya wanasiasa 100 wa upinzani.

Baada ya uamuzi wa mahakama ya upeo uliofutilia mbali uchaguzi wa urais, maafisa wakuu serikalini, akiwemo Kenyatta waliwatisha na kuwahujumu majaji.

Serikali bado inaendelea kupuuza kilio cha mashirika ya kijamii cha kutekeleza Public Benefits Organizations (PBO) Act, 2013, sheria iliotiwa sahihi na Rais Mwai Kibaki mnamo Februari 2013 ili kulainisha usimamizi wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali na kuimarisha utendakazi. Badala yake, uongozi wa Kenyatta umejaribu mara mbili kupendekeza mabadiliko katika sheria hio kukabili kazi za mashirika ambayo yanapokea udhamini zaidi ya asilimia 15 ya fedha zao kutoka kwa ufadhili wa kimataifa. Pendekezo la kwanza la kubadili sheria lilikataliwa na bunge Disemba 2014 na la pili liliwekwa pembeni kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa 2017, lakini bado kuna uwezekano wa mamlaka hiyo kuyarejesha mapendekezo hayo ya kubadili sheria hiyo tena.

Kutokuwepo kwa uwajibikaji wa ubakaji na dhulma za kimapenzi

Human Rights Watch ilinukuu visa vya ubakaji na dhulma za kimapenzi wakati wa operesheni za polisi kule Magharibi mwa kenya na Nairobi katika msimu wa uchaguzi.

Wanawake wengi walisema kuwa walibakwa na maafisa wa polisi wenye sare rasmi au wanaume waliovalia sare rasmi, wengi wao wakiwa wamebeba bunduki, vitoa machozi, fimbo na walikua wamevaa sare rasmi za kupambana na ghasia. Katika kisa kimoja, msichana alifariki baada ya kubakwa. Mwanamke mwenye umri wa miaka 27, aliyehojiwa, na aliyekuwa amejifungua Agosti 27 alibakwa siku nne baadae. Wanawake wengi na wasichana walisema kuwa waliathirika na kulemazwa au kuwa na shida zingine za kiafya.

Ijapokuwa shirika linalosimamia huduma za polisi Kenya Police Service na IPOA walikuwa wameahidi kuchunguza kesi hizi, kumekuwa na hatua chache zilizopigwa katika kuwashitaki na kuwaadhibu waliohusika na vitendo hivyo. Wengi wa manusura hawakupokea matibabu baada ya kunajisiwa ama kupewa mashauri.

Tishio kwa maisha ya watu na ya ziwa Turkana

Kupungua kwa viwango vya maji katika ziwa Turkana baada ya ujenzi wa mabwawa na ukuzaji mimea katika sehemu ya chini ya bonde la mto Omo nchini Ethopia kunaendelea kuhatarisha maisha ya watu nusu millioni wenye makao yao nchini Ethopia na Kenya. Mnamo Juni, Shirika la umoja wa mataifa linalosimamia elimu, sayansi na Utamaduni United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization (UNESCO) liliiweka mbuga ya wanyama pori ya ziwa Turkana miongoni mwa sehemu ambazo zinakabidhiwa na changamoto za kuangamia (list of endangered World Heritage Sites). UNESCO’s World Heritage Committee ilieleza wasiwasi wake kuhusu mabadiliko na madhara yalioletwa baada ya kujengwa kwa bwawa la Gibe III kwa mazingira ya ziwa Turkana.

Maumbile ya kijinsia na Utambulisho wa kijinsia

Kenya inaadhibu mahusiano huru ya kingono baina ya watu wa jinsia moja kwa adhabu ya miaka 14 jela. Kesi ya kikatiba kupinga marufuku hiyo bado imesalia katika mahakama kuu. Mnamo Oktoba, mahakama iliamrisha marufuku iliowekewa filamu ya ‘Rafiki’ na bodi ya filamu nchini Kenya Film Classification Board kutolewa kwa siku saba. Filamu hio ilihusu hadithi ya wapenzi wawili wa kike ambao baba zao ni mahasimu wa kisiasa.

Wadau wakuu wa kimataifa

Kenya inaendelea kuchangia pakubwa katika kanda ya Afrika Mashariki na imedumisha mahusiano ya karibu ya kisiasa na kiuchumi na Marekani, Uchina na Mataifa ya Ulaya.

Wakati ambapo hakuna kesi inayoendelea katika mahakama ya jinai, ( International Criminal Court) kesi zinazohusu jinai na mauwaji ya watu kinyama zilizofanywa wakati wa machafuko ya kisiasa ya 2007-2008 nchini Kenya, serikali bado haijawasalimisha watu watatu wanaotuhumiwa walihitilafiana na mashahidi wa kesi uko ICC.

Kama ilivyokua, uchaguzi wa 2007 ulipingwa sana, uchaguzi wa Agosti 2017 ulivutia umaakini wa dunia nzima. Mnamo Januari 2018, Antonio Guterres aliye katibu mkuu wa Umoja wa mataifa UN alimtuma aliyekuwa Rais wa Nigeria Olesegun Obasanjo kukutana na Kenyatta na Odinga, katika azma ya kupunguza msisimko wa kisiasa. Mnamo Machi 9, Kenyatta na Odinga walikubali kufanya kazi pamoja kupunguza joto la kisiasa.

Kati ya Oktoba na Machi 2018, balozi wa Marekani nchini Kenya Robert Godec, pamoja na wakuu wa balozi zingine Kenya, walikisihi chama tawala cha Jubilee na kile cha upinzani NASA kuchukua hatua kumaliza vurugu na joto la kisiasa lililofuata baada ya uchaguzi wa urais uliozozaniwa sana.

Mashirika yasio ya kiserikali yaliwakosoa wanadiplomasia kwa kukiunga mkono chama tawala na kwa kuhimiza upinzani kukubali kushindwa na kumaliza maandamano, badala ya kulaani kile kilichotajwa kuwa mfumo wa uchaguzi uliompendelea rais ya Kenyatta.