Baada ya kuingia ofisini Oktoba 2015, Rais John Pombe Magufuli alidhamiria kuondoa tatizo la rushwa serikalini na kuongeza uwajibikaji kwa manufaa ya wananchi wa kawaida, lakini badala yake amezuia uhuru wa msingi kupitia sheria na matamko kandamizi. Waandishi wa habari wakosoaji, wanasiasa, watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati wa asasi za kiraia na maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa wamekumbana na aina mbalimbali za vitisho na kuwekwa vizuizini bila sababu za msingi kunakofanywa na mamlaka za serikali.   

Wakati serikali imepiga hatua nzuri katika kutanua wigo wa upatikanaji elimu ya sekondari bure, kwa upande mwingine imetekeleza marufuku ya kibaguzi dhidi ya wanafunzi wenye mimba. Zaidi imeendelea kukwamisha mchakato wa mabadiliko ya sheria yanayoongeza umri wa ndoa kuwa miaka 18 kwa watoto wa kiume na wa kike.  

Uhuru wa Kujieleza

Mamlaka zimekuwa zikiwakamata bila sababu za msingi au wakati mwingine kuwatisha na kuwasumbua wanaharakati wa haki na baadhi ya wanachama maarufu wa vyama vya upinzani ambao walikuwa wakikosoa serikali au rais.

Desemba 13, 2016, polisi walimkamata Maxence Melo, mtetezi maarufu wa haki za binadamu na mmiliki wa mtandao wa kijamii Jamii Forum, ambao ni tovuti binafsi ya kuibua maovu na kutoa taarifa, na Mike William, ambae ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Jamii media, ambayo ndiyo inayohodhi tovuti hiyo. Tovuti hiyo huchapisha makala na mijadala inayoweka hadharani vitendo vya rushwa katika sekta ya umma na kukosoa vitendo vya serikali.

Polisi walifanya msako katika ofisi za Jamii Forum na nyumbani kwa Melo bila kuwa na kibali. Inaripotiwa kuwa walichukua nakala kadhaa za nyaraka. Desemba 16, 2016, Mahaka ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam ilifungua mashtaka dhidi ya Melo, chini ya sheria tata ya Makosa ya Mtandao Tanzania, mashtaka yakiwa ni pamoja na kukwamisha upelelezi kwa kukataa kutoa majina ya wachangiaji wa Jamii Forum wasiotaka majina yao kujulikana, na “kuendesha tovuti ambayo haijasajiliwa Tanzania.” Kesi yao ilianza kusikilizwa mwezi Agosti 2017 na inaendelea mpaka wakati taarifa hii inaandikwa.

Mwezi Machi, polisi mkoani Morogoro, takribani kilometa 200 magharibi mwa Dar es Salaam walimkamata Emmanuel Elibariki, mwanamuziki mashuhuri wa mtindo wa kufokafoka anaejulikana kama Ney wa Mitego, kufuatia kutoa nyimbo ambayo inaelezwa kumtusi rais. Aliachiwa bila mashtaka.

Mwezi Julai, mkuu wa wilaya ya Dar es Salaam aliamuru kukamatwa kwa Halima Mdee, mbunge na kiongozi wa Bawacha, baraza la wanawake la chama cha upinzani Chadema. Mdee alikosoa maamuzi ya rais kupiga marufuku wasichana wenye mimba kuendelea kusoma katika shule za umma. Polisi walimkata kwa makosa ya kumtusi rais.

Mwezi Agosti, polisi walimkamata Ester Bulaya, mbunge wa Bunda kwa tiketi ya Chadema, kwa kufanya shughuli za kisiasa nje ya jimbo lake. Katika tukio tofauti, polisi walimkamata Godbless Lema, mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, na Salum Mwalimu, makamu katibu mkuu wa chama Zanzibar, ikiwatuhumu wanasiasa hawa kwa uchochezi.

Mwezi Septemba,watu wasiojulikana walimshambulia kwa risasi na kumsabibishia majeraha Tundu Lissu, mbunge ambaye alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa rais, huko Dodoma. Lissu, Mwanasheria mkuu wa Chadema, na rais wa chama cha wanasheria Tanzania (Tangayika Law Society), alikamtwa na polisi mara kadhaa mwaka 2017, ikiwa ni pamoja na kutoa “hotuba za chuki” na “maneno ya matusi ambayo yanaweza kupelekea chuki ya kikabila.”

Mwezi Oktoba, polisi walimkamata Zitto Kabwe, kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, na kumshtaki kwa uchochezi, kwa misingi ya kukiuka Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Takwimu ya 2015, ambayo inasema ni makosa kutoa takwimu ambazo hazijaidhinishwa na Tume ya Taifa ya Takwimu.

Oktoba 17, polisi walivamia semina iliyoandaliwa na Mpango wa Madai ya Mkakati Afrika (ISLA), shirika la Afrika linalosimamia haki za wanawake na jinsia. Kamanda wa polisi wa mkoa wa Dar es Salaam aliagiza kukamatwa kwa wanasheria na wanaharakti 12 bila sababu za msingi, ikiwa ni pamoja na raia wawili wa Afrika Kusini, mmoja kutoka Uganda na tisa kutoka Tanzania, kwa mashtaka ya uongo ya “kuchochea mapenzi ya jinsia moja.” Polisi waliwaachia Oktoba 26, na kuwafukuza nchini wanasheria wote wa kigeni siku moja baadae. Kesi dhidi ya wanasheria wa kitanzania inaendelea kuwa wazi hadi wakati taarifa hii inaandikwa.

Novemba 14, maafisa wa serikali ya Tanzania jijini Dar es Salaam waliwazuia Human Rights Watch kufanya mkutano na waandishi wa habari kuzindua ripoti juu ya unyanyasaji wa watumishi wa ndani wahamiaji wa Kitanzania walioko Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Juni 25, Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba alitishia kufuta usajili wa mashirika ambayo yalikuwa yakipinga kauli tata ya rais aliyotoa Juni 22 kupiga marufuku wasichana na kina mama wadogo kuwepo katika shule za umma, na kutishia kuwafungulia mashtaka au kumfukuza nchini mtu yeyote anaefanya kazi kulinda haki za wasagaji, mashoga, wanaovutiwa na jinsia mbili, na waliobadili jinsia (LGBT).

Septemba, Bunge la Tanzania lilipitisha Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na ya Posta (Maudhui ya Kimtandao), ambayo inalenga kudhibti maudhui yanayotumika katika mitandao ya kijamii, na kuweka faini kali kwa watumiaji binafsi na watoa huduma za mitandao.

Uhuru wa Vyombo vya Habari

Serikali imefungia au kutishia vituo binafsi vya redio na magazeti, imesitisha kuonyeshwa mubashara kwa mijadala ya bunge, na kuagiza kufunguliwa mashtaka kwa takriban watu 10 juu ya maneno waliyoandika katika mitandao ya kijamii. Mwezi Machi, Rais Magufuli alitoa onyo hadharani kwa vyombo vya habari “kuwa makini, jiangalieni.” 

Mwezi Machi, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye ndio kiongozi wa shughuli zote za kiserikali katika mkoa, alivamia akiwa na askari wenye silaha, ofisi za Kampuni ya Clouds FM, kituo binafsi, na kuagiza kurushwa kwa picha za video za kashfa kumuhusu mchungaji mmoja. Kituo hicho kilikataa kurusha video hiyo.

Mwezi Juni, mamlaka zilifungia gazeti binafsi la Mawio kwa miaka miwili kwa sababu ya kuchapisha makala iliyowahusisha marais waliopita na tuhuma za kushindwa kusimamia mikataba ya madini. Mwezi Septemba, serikali ilifungia gazeti la Mwanahalisi, gazeti la kila wiki, kwa kipindi cha miaka miwili, kwa madai ya “uandishi usio na maadili” na “kutishia usalama wa taifa” kwa kuchapisha makala ya kuhimiza maombi juu ya Tundu Lissu, mwanachama wa chama cha upinzani. Mwezi Oktoba, mamlaka zilifungia Raia Mwema, gazeti la kila wiki, kwa siku 90 kwa kuchapisha makala inayosemekana kukosoa utawala wa Magufuli.

Haki za Wanawake na Watoto

Mwezi julai 2016, Mahakama ya Katiba Tanzania ilitoa maamuzi kuwa ndoa za watoto ni kinyume cha katiba na kuagiza serikali kuweka umri wa miaka 18 kama umri wa chini kwa ndoa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu maamuzi hayo kutolewa. Maamuzi haya ni ya kesi iliyofunguliwa Januari 2016 na Msichana Initiative, shirika la haki za wasichana, ikipinga sheria za kibaguzi za ndoa Tanzania. Mwezi Septemba, Mwanasheria mkuu wa Tanzania, George Masaju, alikata rufaa ya maamuzi hayo.   

Mwezi Desemba 2016, serikali iliondoa ada na gharama nyingine kwa shule za msingi na sekondari. Hatua ambayo iliongeza kiwango cha usahili kwa shule za sekondari, lakini wanafunzi masikini bado wanaandamwa na vikwazo, ikiwa ni pamoja na mwendo mrefu kufika shule na gharama.

Wasichana wengi wanakumbana mara kwa mara na unyanyasaji wa kijinsia na unyonyaji kutoka kwa walimu shuleni. Shule zinakosa ulinzi wa kutosha na mfumo wa siri wa kutoa taarifa.  

Adhabu za viboko kwa wanafunzi bado ni jambo la kawaida, linalotekelezwa kisheria katika shule za sekondari Tanzania, jambo ambalo linapingana na viwango vya kimataifa.

Wasichana pia wanakumbana na ubaguzi shuleni. Maafisa wa shule wanaweza kuwafukuza shule wasichana wenye mimba au walioolewa. Mwezi Mei, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliwasilisha muongozo wa kujiunga tena na shule ili kurekebisha kanuni na kuhakikisha kwamba wasichana wanaweza kurudi mashuleni baada ya kupata mimba. Bunge la Tanzania halikupitisha muongozo huo.

Maelfu ya wanawake wa Kitanzania wanaofanya kazi za ndani huko Mashariki ya Kati wanakumbana na uvunjifu wa haki za kazi na aina nyingine za unyanyasaji. Tanzania haina sheria za kuwalinda wafanyakazi wahamiaji wakiwa ughaibuni, na udhaifu huu unachochea unyanyasaji wa wafanyakazi.  

Muelekeo wa Kimapenzi na Utambulisho wa Jinsia

Katikati ya 2016, serikali ilianzisha msako na uvunjifu wa haki za watu wa LGBT na watetezi wao. Maafisa waandamizi wa serikali walitishia kuwakamata mashoga na wafuasi wao katika mitandao ya kijamii na kufuta usajili wa mashirika “yanayochochea” mapenzi ya jinsia moja. Walizuia usamabazaji wa vilainishi, kuvamia na kufunga vituo na kliniki binafsi zinazotoa huduma kulenga watu hawa, ikiwa ni pamoja na wanaume wanaojihusisha na mapenzi na wanaume wenzao, wanawake wanaojiuza, na watu wanaotumia madawa ya kulevya.

Mwezi Disemba 2016, polisi jijini Dar es Salaam walivamia semina ya kujikinga na virusi vya ukimwi (HIV) iliyolenga makundi maalum ya watu, na kuwashikilia kwa muda mfupi washiriki nane. Huko Zanzibar, polisi iliwazuia wanaume tisa kwa siku kadhaa kwa tuhuma za kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, na kuwalazimisha kufanyiwa vipimo vya njia ya haja kubwa, aina ya ukatili.

Mwezi Machi, polisi walimkamata mtu mmoja, 19, aliyetuhumiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja kutokana na picha alizoweka kwenye ukurasa wake wa Instagram na kumfanyia vipimo kwa njia ya haja kubwa. Wanaharakati kadhaa walikamatwa kwa kufanya vikao. Mwezi Julai, Rais Magufuli alisema kwamba “hata ng’ombe hawakubaliani na mapenzi ya jinsia moja. Mwezi Septemba, polisi Zanzibar waliwakamata watu 20 katika semina ya wazazi wa watu wenye mahitaji maalumu na kuwatuhumu juu ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.

Baadhi ya mashirika yameripoti kwamba misako hii imepelekea wanaume walioathirika na virusi vya Ukimwi (HIV) kushindwa kupata dawa za kupunguza makali, wakati wanaume wengine wanaojihusisha na mapenzi na wanaume wenzao wameacha kupata vipimo na huduma za kujikinga.

Wanaotafuta Makazi na Wakimbizi

MWaka 2017, Tanzania ilipokea zaidi ya wakimbizi 240,000 ambao waliingia nchini kutokea Burundi kuanzia Aprili 2015, kutokana na machafuko ya kisiasa huko Burundi. Mwezi Julai, Rais Magufuli aliagiza kusitishwa kwa usajili na kupatiwa kwa uraia kwa maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi, na kuwaaasa hadharani wakimbizi kurudi Burundi kwa ridhaa yao.

Watumishi Muhimu wa Kimataifa

Tanzania iliwafukuza papo kwa hapo wakuu watatu wa mashirika ya Umoja wa mataifa, ikiwa ni pamoja na Awa Dabo, mkurugenzi mkazi wa Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP). Iliripotiwa kwamba UNDP walikuwa wakosoaji wakubwa wa namna uchaguzi wa Zanzibar ulivyofanyika.

Mwezi Juni, Tanzania ilijitoa katika Mpango wa Ubia wa Uwazi Serikalini, mpango wa kimataifa unaolenga kuchochea uwazi katika serikali, na kuboresha utoaji wa huduma, mwitikio wa serikali, kupambana na rushwa na kujenga uaminifu mkubwa.

Mwezi Agosti, wataalamu watatu wa haki wa ukanda wa Afrika waliandika barua ya pamoja kuomba rufaa kwa rais wa Tanzania kuhusu tamko lake Juni 22 juu ya wasichana wenye mimba.

Mwezi Julai, mtaalamu wa kujitegemea kutoka UN anaehusika na upatikanaji wa haki za binadamu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, Ikponwosa Ero, alitembelea Tanzania, alipongeza hatua za serikali kupunguza mashambulio dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, lakini aligundua kwamba watu wenye ulemavu wa ngozi wanaishi katika “mazingira hatarishi.” Pia alielezea wasiwasi wake juu ya matumizi ya shule kama vituo vya ulinzi kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi.

Mwezi Septemba, Kamati ya UN ya Haki za Watu wenye Ulemavu ilisikiliza kesi ya mtu mmoja mwenye ulemavu wa ngozi ambae alishambuliwa na watu wawili, na hakupata fidia kutoka serikalini kwa mashambulizi aliyopata. Kamati ilihitimisha kwamba serikali ilishindwa kuchukua hatua za makusudi kulinda vitendo vya mashambulio na kuchunguza kiumakini na kuadhibu wahusika. Kamati vile vile iliitaka serikali kuharakisha mashtaka ya mashambulio dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kufanya vitendo vya kutumia viungo vya mwili wa binadamu kwa uchawi kuwa kosa kisheria.