Skip to main content

Kusubiri kimbunga: Virusi vya Korona barani Afrika

Maradhi yanatisha kusambaratisha kambi za wakimbizi na maeneo ya miji yenye idadi kubwa ya watu.

Licha ya kuwa virusi vya Korona vinaingia barani Afrika polepole kuliko ilivyokuwa katika mabara mengine, mkurugenzi wa Afrika wa shirika la haki la Human Rights Watch Mausi Segun ameelezea hofu kwamba maradhi hayo hivi karibuni yatatatiza pakubwa nchi za Afrika. Anasema sababu moja ni unyonge kwenye miundo misingi ya afya ya umma na matibabu katika nchi za Afrika na vilevile ni vigumu kuwatenga watu walioambukizwa kwenye mitaa ya mabanda katika miji yenye idadi kubwa ya watu. Aidha katika kambi za wakimbizi lipo hilo tatizo. Segun amezungumza na Amy Braunschweiger kuhusu jinsi serikali za Afrika zinaweza kukabili ueneaji wa virusi vya Korona – kwa namna zote, njia safi na njia zisizosafi – na vilevile namna ambapo kutumia njia zinazotii haki za binadamu kutachangia katika kuhakikisha raia wengi wa Afrika wanaepuka maradhi hayo.

Jambo lipi linampa mtu wasiwasi sana kuhusiana na kuenea virusi vya Korona barani Afrika?

Nchi nyingi za Afrika tulizomo na shughuli zina mifumo dhaifu ya afya ya umma. Zinakosa miundo misingi ya matibabu maana mifumo mingi haitoshelezi mahitaji ya raia katika nchi hizo.  Hata ni bahati nzuri kwamba msimu huu wa kuenea virusi vya Korona, virusi hivyo havijaenea kwa haraka Afrika. Ni hali inayozipa serikali nyingi za Afrika muda wa kuandaa miundo misingi ya kukabili maradhi yakifika katika nchi zao. Cha kusikitisha ni kwamba hatujaona juhudi kama hizo katika nchi nyingi. Bado hatuoni mipango haswa ya kutayarisha njia za kupima maradhi na kuyatibu, na tunajua vipo visa vingi vya virusi hata kuliko inavyoripotiwa. Ueneaji wa virusi hivyo pia unafika Afrika wakati ipo mikumbo mingine ya maradhi mfano ukambi na kipindupindu. Hali hii itaongeza makali ya athari za virusi vya Korona kwa jamii za Afrika. Kuna pia ukosefu wa maji safi ya kufanya usafi katika nchi nyingi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara. Ni ukosefu unaoathiri hospitali nyingi pia.

Hali kama hii inatia wasiwasi maana nchi tajiri duniani zimehangaishwa na ueneaji wa virusi vya Korona. Unaweza kujiuliza maswali mengi kuhusu ueneaji ukigonga Afrika kwa kasi ile hali itakuwa namna gani.

Je, serikali za Afrika zimeshughulikia maambukizi ya Korona kwa namna zinazokiuka haki za binadamu?

Ni wajibu wa serikali kuwaelimisha raia kuhusu mikumbo ya maradhi mapya katika jamii na vilevile kutia bidii ya kukomesha ueneaji wa haraka. Serikali pia ina jukumu la kumtunza anayeugua, kuhakikisha hakuna ubaguzi wa wagonjwa huku wale wanaolemewa na maradhi wakiangaliwa zaidi.

Baadhi ya serikali za Afrika zimekuwa polepole katika kushughulikia ueneaji wa virusi vya Korona huku nyengine, awali wakati habari za maradhi zilichipuka, zilipuuza na kudai ni maradhi yanayokabili jamii za mbali wala sio waafrika. Katika nchi nyingi za Afrika, kukosa kutenga fedha za kufadhili sekta za afya kumeathiri uwezo wa serikali nyingi wa kufuatilia na kujua visa vipya, ndio maana tunapata ukosefu wa mipango ya kupima na kutibu. Vilevile kuna wahudumu wachache wa afya katika nchi nyingi za Afrika kuwatibu wale wanaoambukizwa.

Hadi kufikia wakati wa kurekodi visa viwili vya kwanza tarehe 31 mwezi wa Machi, serikali ya Burundi ilikuwa imedai kwamba haingekumbwa na virusi vya korona kwa sababu inalindwa na mwenyezi mungu. Huku wataalamu wakionya kwamba nchi ilihitaji kuanza kuwapima watu wake na kwamba hospitali zake na maeneo ya kuwatenga wenye virusi hazikuwa safi ifaavyo huku yakijaa watu, serikali ilikosa kuelewa haraka. Sudan kusini nayo haikuwa na visa vya virusi (wakati wa kuandaa ripoti hii) – hata hivyo haimanishi kwamba ndio uhalisia haswa kwamba haina kabisa.

Tumepata habari za serikali kadhaa kutumia nguzu za kupita kiasi kwenye utaratibu wa kuwatenga watu. Nchini Uganda, watu waliokuwa wakirejea kutoka nchi ambazo zilikuwa zimekumbwa na virusi vya Korona walikuwa wakizuiwa punde wakitua nchini humo. Wangewekwa kwenye hoteli kwa lazima, huku wakitakiwa kulipia gharama za hoteli hizo kwa siku 14 hivi. Gharama ingepanda hadi dola 1,000 za Amerika kwa mtu mmoja. Baadhi ya watu wamelazimishwa kujitenga kwa kulala kwenye sebule za hoteli ama viwanja vya ndege, hali inayotatiza harakati za kukabili ueneaji wa Korona. Watu hao wangechanganyika na wengine wanaosafiri na hivyo kuchangia katika ueneaji wa virusi.

Nchini Kenya, polisi walimuuwa kwa kumpiga risasi mvulana wa umri wa miaka 13 tarehe 30 Mwezi Machi, wakidaiwa kutekeleza marufuku ya kutoka nje kuanzia saa moja usiku. Vilevile polisi walitumia nguvu ya kupita kiasi mjini Mombasa na maeneo mengine ya nchi kwenye juhudi za kutekeleza marufuku hiyo.

Nayo serikali ya Ethiopia ilizima huduma za internet na huduma za simu kwa muda wa miezi mitatu katika eneo la Oromia magharibi. Serikali imekuwa ikifanya oparesheni za kuzima ghasia katika eneo hilo. Hatua hiyo iliwafanya mamilioni ya watu katika eneo hilo kushindwa kupata habari za kuwepo maradhi hatari duniani hadi wakati serikali ilirejesha huduma hizo tarehe 31 mwezi Machi.Ethiopia ilichukua hatua hiyo baada ya makundi ya haki kutoa shinikizo kwamba msimu wa maradhi mabaya yafaa watu wote wawe wakipata habari za ueneaji ili kuepuka maambukizi.

Nchini Afrika kusini, tumepata habari za polisi kufyatua risasi zisizo haswa na vilevile kuwafukuza watu kwa kuwapulizia maji ya malori ya polisi. Walengwa wamekuwa watu wasio na makwao hasa wakiwa kwenye foleni za kugawiwa chakula. Polisi wamekuwa wakiwaambia “endeni nyumbani!” Hawa ni watu wasio na maboma ya kwenda, hawana makao hivi kwamba hatua ya majuzi ya kuwaweka kwenye shule, makanisa, viwanja vya michezo na maeneo ya kuegesha magari inakiuka kanuni ya watu kujitenga na wenzao msimu huu wa virusi vya Korona. Hali hii inazikumba jamii za kuhamahama ambapo  watu wake wamekuwa wakitengwa kwa kulazimishwa ili wasalie mahala fulani.

Je hali ya kuwapuuza watu maskini msimu huu inaathiri vipi watu wengine katika jamii?

Maradhi haya yanahatarisha maisha ya kila mtu. Hata hivyo, baadhi ya watu katika jamii wanaweza kujiepusha kwa wepesi kuliko wengine. Watu wengi walio maskini hufanya kazi muhimu kwa jamii lakini zenye ujira mdogo. Hao ndio watu wanaochuna mboga na nafaka za chakula mashambani,  wanaziuza kwenye masoko, ndio madereva wa mabasi, ndio husafisha hospitali, au kufanya kazi za yaya manyumbani. Kumaanisha kwamba sote tunaunganishwa kwa namna msimu huu. Kwa hivyo iwapo serikali hazitapata njia za kuwafadhili na kusaidia harakati za kujitafutia za watu wadogo, hakuna mtu hata mmoja katika jamii ataweza kujitenga yeye mwenyewe kutokana na kuenea kwa virusi vya Korona.

Zipo njia ambapo serikali zimeshughulikia ueneaji wa virusi vya Korona kwa namna inayotii haki za binadamu?

Serikali kadhaa zilichukuwa hatua za haraka kukabili ueneaji wa virusi kwa kuweka marufuku kwa usafiri – Sudan ilianza kuwapima wasafiri waliokuwa wakiingia nchini tangu mwisho wa mwezi Januari. Baadhi ya nchi zinatoa huduma za afya kwa namna, bila utaalamu haswa lakini ni huduma za mwanzo mwanzo. Nchini Nigeria katika jimbo la Lagos, serikali inawapa watu vifaa vya matumizi ya kinyumbani, chakula, sabuni, mafuta na kadhalika- walengwa ni mitaa ya watu wa mapato ya chini na taasisi husika.

Serikali zinafaa kuelewa kwamba uchache wa pesa kwa watu wenye mapato ya chini au wanaoishi katika mitaa ya mabanda ni changamoto kuu kwa jamii msimu huu. Wasipofanya kazi kwa siku moja au mbili watakosa chakula. Serikali zinazochukuwa hatua za kutimiza mahitaji ya kila siku ya watu kama hao zinatoa picha nzuri na ni mfano unaofaa kuigwa.

Msimu wa virusi vya Korona unaathiri vipi nchi zinazokumbwa na mizozo na mapigano?

Katika nchi zenye mizozo mfano Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika Kati, Mali, Burkina Faso, na Nigeria- eneo la Kaskazini, raia wanakabili changamoto kuu. Hii ni hali inayozikumba nchi zinazowahifadhi wakimbizi pia kama vile Sudan, Sudan kusini, Ethiopia, na Kenya. Nchi hizi ambazo tayari zinakumbwa na ukosefu wa miundo misingi na mifumo ya kijamii hazina uwezo wa kutosha wa kukabili ueneaji wa virusi vya Korona. Idadi kubwa ya watu wasiokuwa makwao na waliofukuzwa makwao na ukosefu wa usalama ni changamoto inayotatiza huduma za afya na matibabu kwa watu, hasa virusi vikienea katika jamii za nchi hizo.

Nchini Burkina Faso, idadi ya raia waliohama makwao wakitoroka mapigano imeongezeka kwa asilimia 1000 mwaka uliopita. Zaidi ya watu 765,000. Kwa sasa Burkina Faso ina idadi kubwa sana ya visa vya maambukizi ya Korona katika eneo la Afrika Magharibi . Kukiwa na watu wasio na makwao na wakimbizi wanaoishi kwenye makao kwa kusongamana miongoni mwa jamii tofauti,  juhudi za serikali za kukomesha au hata kukabili ueneaji wa virusi zinatatizwa pakubwa. Serikali zinazokumbwa na mazingira kama haya zinalazimika kuhakikisha watu hawasongamani, zihakikishe ipo nafasi baina ya watu kwenye makao halafu zianze kutoa maeneo maalum ya kuwatenga hasa walioambukizwa.

Hekaya na habari za kupotosha, ikiwemo imani zisizo na msingi kwamba maradhi ya Korona yanawalenga tu watu wa namna fulani wala sio waafrika, zinaweza kuchangia katika kuongezeka kwa vitisho dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya misaada. Imani hizo pia zinatatiza utendakazi wa wafanyakazi wa mashirika ya misaada  katika kutoa huduma za kuokoa maisha na kuwalinda raia.

Ni nani barani Afrika yu katika hatari zaidi ya kukumbwa na virusi vya Korona?

Kila mtu yu hatarini.  Katika baadhi ya maeneo duniani, watoto hawamo katika hatari ya kukumbwa au hata kufariki kwa Korona. Lakini hatuwezi kusema kwa uhakika iwapo hali ni iyo hiyo barani Afrika. Afrika ina matatizo ya ukosefu wa lishe kwa watoto, maambukizi mbadala, mfano minyoo na maradhi mengine ya kuambukizwa yanaweza kufanya watoto kuwa hatarini zaidi msimu huu wa kuenea kwa virusi vya Korona.

Kwa namna, tutarajie kwamba yale ambayo tumeyaona katika maeneo mengine yatarejelewa barani Afrika.  Lakini tunahofia kwamba virusi vya Korona vitasambaa kupitia maisha ya magerezani katika nchi za Afrika ambapo wafungwa huishi kwa kusongamana. Serikali, mfano  Sudan Kusini zimeanza kuwaachilia wafungwa, yafaa zianze kupunguza idadi kwenye magereza kwa kuhakikisha waliomaliza vifungo wanaachiliwa haraka huku waliotiwa kifungoni bila kufwata taratibu zifaazo wanaachiliwa.  Idadi kubwa ya wafungwa barani Afrika ni wale ambao wangali wana kesi kortini. Wafungwa ambao wamo jela kwa makosa yasiyo ya jinai, huu ni wakati wao kuachiliwa mapema.

Tunatatizwa pia na makao ya watu waliotoroka makwao, mitaa ya mabanda mijini, ambapo watu wengi, wakiwemo wazee   na wengine wenye matatizo mbali mbali ya afya huishi na familia zao. Hali hiyo inafanya iwe vifungu kutekeleza sharti la kuwatenga watu msimu huu wa virusi vya Korona. Tunatatizwa pia na watu wanaoishi na ulemavu, hasa waliofungiwa  au kuzuiwa katika taasisi mbali mbali. Swala la changamoto zinazowakumba wahudumu wa afya vilevile – wengi wao wakiwa wa kike  – na vilevile wazee, wanawake kwa ujumla, na wafanyakazi katika nchi zisizokuwa zao asili, wengi wakiwa wale ambao hawajanakiliwa popote, watapata ugumu kupata huduma za afya zinazohitajika msimu huu. Shule zimefungwa, kwa hivyo kusalia nyumbani kwa muda mrefu kunahatarisha maisha ya hasa wasichana maana wanakabili tishio la kubakwa ama kutolewa kwa ndoa za mapema. Vilevile, kinyume na ilivyo katika nchi tajiri, masomo kupitia njia za mitandao ya internet au hata kupata mafunzo nyumbani ni nadra kufanyika kwa wanafunzi barani Afrika. Hata hivyo, huduma zilizoboreka za umeme, kuwepo mitandao ya internet kwa kiwango fulani kwenye maboma ya watu, simu na mawasiliano mengine, vinaweza kuwa njia mbadala za kuendelea mafunzo kwa wanafunzi ambao wako nyumbani kwa sasa maana haijulikani watarejea shuleni lini.

Hata hivyo jambo ambalo ni vyema kulitaja hasa kuhusu nchi nyingi za Afrika ni kwamba, kutokana na marufuku kwa usafiri, watu tajiri katika nchi za Afrika na vilevile maafisa wakuu serikalini leo hii wanashindwa kusafiri nchi za nje kutafuta matibabu. Hii ni hali ambayo huenda ikachangia katika kuibuka msukumo mpya kwa serikali za Afrika kuboresha zaidi sekta za afya katika nchi za Afrika. 

Mahojiano haya yamefupishwa na kuhaririwa

Your tax deductible gift can help stop human rights violations and save lives around the world.

Topic